Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gallas: Huyu? Hafiki Krismasi

Gallas Pict Gallas: Huyu? Hafiki Krismasi

Wed, 7 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Nyota wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Ufaransa, William Gallas ameweka wazi ana wasiwasi kocha mpya wa timu hiyo, Enzo Maresca hatafika Sikukuu ya Krismasi na kibarua chake kitakuwa kimeota nyasi.

Maresca aliyejiunga na Chelsea akitokea Leicester City ambayo aliisaidia kuchukua ubingwa wa Championship na kupanda daraja Ligi Kuu England, yuko na kikosi hicho Marekani kwa maandalizi ya msimu ujao na huko imecheza mechi nne za kirafiki.

Katika michezo hiyo minne, chama hilo la Maresca limepata ushindi mechi moja dhidi ya Club America ya Mexico, ikitoa sare moja na Wrexham ya Wales na kupata vichapo viwili dhidi ya Celtic cha mabao 4-1 na mchezo wa mwisho dhidi ya Manchester City ikachapwa mabao 4-2.

Kutokana na mwenendo huo, Gallas amesema wasiwasi wake mkubwa ni kutokana na kile timu hiyo inaonyesha katika maandalizi ya msimu huko Marekani.

Akizungumza na tovuti ya Genting Casino, Gallas alisema: "Licha ya ukweli wapo katika maandalizi ya msimu na zile ni mechi za kirafiki, lakini bado ninapata wasiwasi ninapoangalia kikosi, mbali ya kutumia pesa nyingi bado kikosi hakionekani kuwa bora kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, bado kuna wachezaji wengi wanaohitaji kuongeza zaidi ubora tofauti na walivyo sasa. Enzo anaweza kufukuzwa kabla ya Krismasi, lolote linaweza kutokea katika soka."

Chelsea imetumia jumla ya Pauni 1 bilioni katika usajili wa wachezaji mbalimbali tangu tajiri Todd Boehly ainunue rasmi timu hiyo Mei, 2022.

Licha ya pesa hizo, mafanikio makubwa aliyopata kocha wao wa msimu uliopita Mauricio Pochettino ni kufuzu kucheza Uefa Conference League baada ya kumaliza nafasi ya sita katika msimamo wa ligi na mwisho wa msimu akafukuzwa.

"Lakini namwombea kila la kheri akae walau hadi msimu utakapomalizika ili apate nafasi ya kuonyesha kile anachoweza kufanya lakini ni ngumu, timu kama haina wachezaji wanaoweza kushinda katika Ligi Kuu itakuwa ni  changamoto sana kwake kubakia hadi muda huo," alisema Gallas.

Lejendi huyu pia anasema moja ya sababu zitakazochangia kufukuzwa kwa Enzo ni ukweli wamiliki wa timu za EPL hawana uvumilivu kabisa.

"Labda Arsenal walifanya hivyo kwa Mikel Arteta na Manchester United walioendelea kubakia na Erik ten Hag, lakini wengi hawafikirii juu ya mipango ya muda mrefu.

Makocha wengi katika kipindi hiki huwa wanadumu kwa miezi sita hadi mwaka tu, nina matumaini Chelsea itamvumilia Maresca japokuwa ni ngumu. Maresca ni kocha wa tano kuajiriwa na Chelsea tangu  Boehly aanze kuimiliki timu hiyo.

"Mwisho wa yote, hatma  yake itategemea na malengo ambayo amepewa na timu ikiwa wanataka kumaliza nafasi nne ama sita za juu lakini kitu ninachokiamini ni ikiwa itafikia mwisho wa mwaka halafu timu ikawa nje ya 10 bora ama kuwa vibaya, watamfukuza tu."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live