Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Galiwango: Huyu Aucho, nyie acheni tu!

Disani Galiwango Rf Disani: Huyu Aucho, nyie acheni tu!

Thu, 27 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Disani Galiwango ni moja ya mabeki wa kushoto wenye wasifu mkubwa katika Ligi Kuu Bara wakiiongezea thamani na kudhihirisha kukua kwake, ikikamata nafasi ya sita barani Afrika na kuendelea kuvutia wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kukiwasha Tanzania.

Beki huyo wa kushoto ni raia wa Uganda anayecheza Kagera Sugar aliyojiunga nayo mwanzoni mwa msimu ulioisha dirisha kubwa kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Vipers ya Uganda aliyomalizana nayo baada ya kudumu kwa miaka minne.

Katika msimu wake wa kwanza, Galiwango amemwondoa katika kikosi cha kwanza beki mkongwe na nahodha wa Kagera Sugar, David Luhende na katika mechi 18 za kwanza, alicheza mechi 16 ikiwemo moja ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Pamba.

Akizungumza nasi, Gwaliwango amemtaja kiungo wa Yanga, Khalid Aucho akisema ni mtu sana na aliyechangia kwa kiasi kikubwa kufika alipo, bila kumsahau kocha mkuu wa Kagera Sugar, Fred Felix ‘Minziro’, kivipi? Tiririka naye...!

AZIOTA SIMBA, YANGA

Galiwango ambaye mwaka 2019 alikuwa kwenye kikosi cha Uganda kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) kule Misri, anasema yuko Kagera Sugar akijitafuta ili kupata timu kubwa ya daraja la Simba na Yanga ili arejee katika kikosi cha taifa cha The Cranes.

“Kwa sasa nafikiria kupata timu nzuri kama Yanga na Simba ama kwenda nje ili nirudi timu ya taifa ambako nimepoteza namba. Ligi ya Tanzania ni shindani sana tofauti na nilikokuwa nacheza mwanzo (Uganda),” anasema Galiwango.

“Nikiwa hapa nahitaji kuwa na mwendelezo kila mechi na nimejifunza kucheza kwa kufuata maelekezo ya walimu na kuwasikiliza wachezaji wenzako. Hapa watu wanapenda sana soka tofauti na nchini kwetu.”

LOMALISA, TSHABALALA

Licha ya kukiri soka la Tanzania limepiga hatua na kuna ushindani mkubwa, lakini beki huyo wa kushoto anasema bado hajaona mchezaji anayemvutia katika nafasi hiyo Ligi Kuu Bara.

Galiwango ni kama anatofautiana na mashabiki na wadau wengi wa soka ambao wanavutiwa na kiwango cha mabeki wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba), Joyce Lomalisa na Nickson Kibabage (Yanga).

Pia Ligi Kuu Bara ina utajiri wa mabeki wa kushoto akiwemo mkongwe, David Luhende (Kagera Sugar), Yahya Mbegu (Singida FG) na Paschal Msindo wa Azam.

“Kwa Tanzania bado sina mchezaji ninayemkubali ama anayenikosha katika beki ya kushoto ambayo mimi ninacheza, ninawakubali zaidi mabeki wa nje, Luke Shaw (Manchester United) na Marcelo aliyekuwa Real Madrid,” anasema beki huyo.

AUCHO NA MINZIRO

Licha ya kupita mikononi mwa makocha wengi, Galiwango anasema kocha wa Kagera Sugar, Fredy Felix ‘Minziro’ ni kocha mzuri kwa sababu ameibadilisha timu hiyo na huwezi kucheza kikosi chake kama hauko fiti.

Galiwango anamtaja nyota mwenzake wa Uganda, Khalid Aucho kuwa ni mchezaji mkubwa ambaye anavutiwa na namna anavyojituma na kuishi akiwa ndani na nje ya uwanja.

“Nimefahamiana na Aucho muda mrefu tangu utotoni amenisaidia sana na kunielekeza, tumekuwa kama ndugu, nafikiri kinachomfanya kuwa bora ni jinsi anavyoishi maisha yake kwa nidhamu akiwa ndani na nje ya uwanja,” anasema beki huyo.

MAJERAHA

Mmwaga maji huyo kwa sasa anaendelea na matibabu ya mwisho ya nyama za paja nyumbani kwao Uganda ambayo aliyapata Februari 25, mwaka huu katika mchezo wa ligi dhidi ya Ihefu kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba ambao waliibuka na ushindi wa 2-1.

“Kwa sasa naendelea vizuri niko kwenye hatua za mwisho za kupona nafanya mazoezi ya viungo na mtaalam wa fizio hivi karibuni nitaungana na timu kwa ajili ya mechi zijazo,” anasema Galiwango.

SIRI NAMBA 3, 12

Nyota huyo akiwa Vipers alikuwa anapendelea kuvaa jezi namba tatu na baada ya kutua Kagera Sugar anavaa jezi namba 12, anasema namba hizo zina siri kubwa kwani zina bahati kwake.

“Jezi namba tatu ni namba yangu ya bahati lakini jezi namba 12 ni namba ya rafiki yangu (Yunus Sentamu) alikuwa anaivaa tukiwa wote Vipers ni mshikaji wangu sana. Jezi namba 12 pia ni siku ya kuzaliwa mtoto wangu wa kiume,” anasema.

PENALTI YA MAZEMBE

Moja ya matukio ya furaha anayoyakumbuka ni mwaka 2022 alipoiwezesha Vipers kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwaondoa vigogo, TP Mazembe kwenye uwanja wao wa nyumbani, Stade TP Mazembe, Lubumbashi.

Katika mchezo huo ulioamuliwa kwa penalti baada ya sare katika michezo miwili, Vipers iliyokuwa chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ilisonga mbele kwa ushindi wa penalti 4-2, huku Galiwango akifunga penalti ya pili na kupangwa kundi moja na Simba.

“Wakati mzuri kwangu ni niliposhiriki Ligi ya Mabingwa nikiwa na Vipers na kufunga penalti muhimu tukishinda ugenini mbele ya TP Mazembe ni tukio ambalo sitalisahau kwa sababu tulifuzu makundi kwa mara ya kwanza,” anasema.

MSIKIE KOCHA

Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Marwa Chambeli anasema Galiwango ni mchezaji wa kiwango cha juu anayewapa utulivu kikosini kutokana na uwezo wake wa kusoma mchezo na kuwasaidia wenzake kujifunza.

“Ni mfano wa kuigwa, ana nidhamu, anajielewa na yuko fiti kimwili anajua kusoma mchezo na matukio uwanjani tunajivunia sana kuwa naye kwenye timu. Alipata majeraha akaenda kwao kutibiwa ataungana na timu hivi karibuni,” anasema Chambeli.

WASIFU WAKE

Galiwango mwenye miaka 26 raia wa Uganda amezitumikia klabu za Simba FC (2016), Water FC (2027), Express (2018-2020) na Vipers (2019-2022) akizifungia jumla ya mabao 37 na assisti 30.

Katika timu ya taifa, kwa nyakati tofauti amecheza kikosi cha umri chini ya miaka 17, 20, 23 na timu ya wakubwa (The Cranes) akizitumikia kwenye jumla ya michezo 75 na assisti 12.

Ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi, mashuti ya mbali, kusoma mchezo na kunusa hatari na kuharibu mbinu za wapinzani

Mwaka 2020 alichukua tuzo ya beki bora wa kushoto wa Uganda, mchezaji mwenye asisti nyingi kwenye ligi ya nchi hiyo (2020), mchezaji bora wa mwaka wa Express (2019), kuchukua ubingwa wa Uganda mwaka 2021 akiwa na Vipers na kushiriki Ligi ya Mabingwa 2021.

Chanzo: Mwanaspoti