Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gakpo, Felix, Ramos, Mbappe Man United

Man U Pic Kylian Mbappe

Thu, 15 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Maisha yaendelee. Hicho ndicho Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag anachojaribu kuwaambia mastaa wake kwamba wanapaswa kukubaliana na hali halisi ya supastaa, Cristiano Ronaldo kuondoshwa kikosini na maisha lazima yaendelee.

Kocha huyo Mdachi alitoa maelezo hayo baada ya mshambuliaji wake matata kabisa duniani kusitishiwa mkataba wake huku ikifichuka wawili hao, kocha na mchezaji hawakuwa kwenye wakati mzuri huko Old Trafford.

Na sasa katika kuondoa jinamizi la Ronaldo kwenye kikosi hicho cha Man United na kuanza zama mpya Old Trafford, kocha huyo wa zamani wa Ajax, amepanga kukijenga upya kikosi chake kwenye safu ya ushambuliaji huku akipania kufanya usajili wa maana kuziba pengo hilo wakati dirisha la usajili wa Januari litakapofunguliwa.

Akizungumza akiwa na timu hiyo mazoezini Hispania kabla ya kurejea zao England kuendelea na msimu wa Ligi Kuu England utakaorejea mzigoni baada ya fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, Ten Hag alijaribu kusema kile ambacho mashabiki wangependa kusikia kwa sasa wakati miamba hiyo ikiachana na huduma ya mmoja wa washambuliaji magwiji duniani.

Alipoulizwa kuhusu kusajili straika mpya kwenye dirisha la Januari, Ten Hag alisema: “Ndiyo, lakini ni kama tu tutapata mchezaji sahihi. Tutafanya kila tunachoweza kwenye uwezo wetu. Tunafanya utafiti kwa kila hatua na kuona kama kuna nafasi ya kumpata mchezaji sahihi wa kumsajili.”

Ten Hag ameonyesha kuwa ni mwenye mafanikio makubwa kwenye dili za usajili licha ya mwanzoni mwa dirisha la majira ya kiangazi kuwashtua mashabiki wakati alipokuwa akihusishwa na mpango wa kuwanasa Adrien Rabiot na Marko Arnautovic.

Na badala yake alikwenda kuwanasa mastaa Casemiro, Antony, Lisandro Martinez, Tyrell Malacia na Christian Eriksen, ambao wote wamefanya vizuri tangu walipotua kwenye kikosi hicho huko Old Trafford.

Mashabiki wa Man United wanatarajia kuona mastaa wenye majina makubwa wakitua Old Trafford kwenye dirisha la Januari kuchukua mikoba ya Ronaldo, huku orodha ya wachezaji wanaosakwa na Man United ikitajwa hadharani.

Cody Gakpo

Kama mambo yasingekwenda tofauti kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, straika wa Uholanzi, Cody Gapko basi muda huu angekuwa staa wa Old Trafford. Man United ilishindwa kumsajili wakati huo, lakini kwa sasa inahitaji tena saini yake na huenda ikamchukua Januari baada ya kufanya vyema huko Qatar kwenye Kombe la Dunia 2022.

Hata hivyo, winga huyo wa PSV Eindhoven bei yake inaweza kuwa juu zaidi baada ya kile alichokifanya Qatar, ambako alifunga mabao matatu. Huduma yake inaweza kugharimu Pauni 55 milioni, lakini kwa umri wa Gapko haitakuwa tatizo kwa Ten Hag kunasa saini yake kwa sababu ni mchezaji anayempa uhakika wa kumtumia kwa muda mrefu.

Joao Felix

Felix mwanzoni hakutazamwa kuwa kwenye mipango ya Kocha Ten Hag, ambaye hapendi kutumia pesa nyingi kwenye usajili, lakini Mreno huyo wa Atletico Madrid saini yake inaweza kuwa kitu muhimu zaidi kwenye kikosi cha Man United.

Bosi wa Atletico amefichua, Felix na Diego Simeone hawana uhusiano mzuri, hivyo klabu hiyo haitamzuia fowadi huyo wa Ureno kama ataamua kuondoka. Atletico ililipa Pauni 106 milioni kupata saini yake akitokea Benfica mwaka 2019, lakini kwa sasa huduma yake haiwezi kupatikana kwa pesa nyingi hivyo, kitu kinachoipa Man United uhakika wa kumnasa.

Ilimhitaji kwenye dirisha lililopita, lakini baada ya kutumia Pauni 80 milioni kumsajili Antony iliachana na Felix ikisubiri mwakani.

Goncalo Ramos

Straika wa Benfica, Goncalo Ramos alimbadili Cristiano Ronaldo kwenye kikosi cha Ureno huko kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar na sasa Man United inataka saini yake akavae buti za gwiji huyo.

Kinachoelezwa ni kwamba Man United ilikuwa inamfuatilia mshambuliaji huyo kabla hata hajafunga hat-trick dhidi ya Uswisi kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar na hivyo sasa huenda ikahangaika kunasa saini yake kwenye dirisha la Januari. Kwa kiwango cha Ramos huko Qatar bila ya shaka kitakuwa kimeongeza thamani yake jambo ambalo Benfica itatumia kama fursa kumuuza kwa bei kubwa.

Kylian Mbappe

Ten Hag atapendezwa na Man United kutotumia pesa nyingi kwenye dirisha la Januari, lakini mambo yanaweza kuwa tofauti kwenye dirisha lile kubwa la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kama kuna mchezaji ambaye hakuna timu itasita kutoa pesa nyingi kunasa huduma yake basi ni Kylian Mbappe, ambaye kwa miamba mingine ya Ligi Kuu England, Manchester City hawezi kwenda huko kwa sababu imeshamsajili Erling Haaland. Paris Saint-Germain imejaribu kumbakiza Mbappe kwa kumpa dili nono kabisa la miaka mitano, lakini jambo hilo bado halijamaliza minong’ono ya mchezaji huyo kuondoka kwenye kikosi hicho cha Parc des Princes.

Chanzo: Mwanaspoti