Mshambuliaji kutoka nchini Brazil na Klabu ya Arsenal Gabriel Jesus amesema aliamua kuondoka Manchester City wakati kocha Pep Guardiola alipomtoa machozi baada ya kumuacha nje ya kikosi kilichoanza katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Jesus alicheza chini ya Guardiola kwa miaka mitano katika uwanja wa Etihad kabla ya kujiunga na Arsenal msimu uliopita wa joto, hatua ambayo alisema ilimfanya ajisikie huru.
Akizungumza katika kipindi cha televisheni cha ESPN cha Denilson show, Jesus alisema mabadiliko katika maisha yake ya City yalikuja wakati wa mchezo wao wa nyumbani dhidi ya Paris Saint-Germain Novemba mwaka 2021 alipowekwa benchi.
“Kulikuwa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG nýumbani, ambapo alimweka Oleksandr Zinchenko kama 9. Jambo la kichaa,” alisema Jesus.
“Siku moja kabla, hakumtumia Zinchenko kwenye mazoezi, aliniweka mimi kama mshambuliaji… na hata Zinchenko aliniambia: ‘siku ile nilijisikia vibaya kwako.’
“Saa mbili kabla ya mchezo kuna mazungumzo ya timu, timu inakula, inapumzika kwa dakika 30 na kwenda mchezoni, akatuambia timu itakavyokuwa, hata sikula, nilienda moja kwa moja chumbani huku nikilia, nikampiga simu mama yangu na kumwambia: Nataka kuondoka.’
Jesus alichukua nafasi ya Zinchenko kipindi cha pili na kutengeneza bao la kusawazisha kabla kufunga bao la dakika za mwisho na kuipa City ushindi wa 2-1.
“Nilijisikia vibaya. Dakika tano baada ya Kylian Mbappe kufunga bao 1-0, Guardiola aliniita. Nilitoa pasi ya bao na kufunga, tuligeuza matokeo kuwa 2-1. Katika mchezo uliofuata Ligi ya Mabingwa wa ushindi wa 2-1 dhidi ya RB Leipzig, nilifikiri nitacheza, lakini sikucheza.
“Kulikuwa na mengi ya hayo kwa Guardiola. Ni ngumu sana. Hapo ndipo nilipoamua na sikutaka kubaki tena. Niliamua kuondoka.
Jesus alijiunga na City Januari 2017 kutoka Palmeiras ya Brazil na kushinda mataji 11 akiwa na klabu hiyo. Wakati wa msimu wake kwanza akiwa Arsenal, alifunga mabao 11 na kutengeneza mengine saba katika mechi 26 za ligi walipomaliza washindi wa pili nyuma ya City kwenye Ligi Kuu England.