Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

GSM wananikumbusha jeuri ya Yussuf Manji

Manji Vs GSM GSM wananikumbusha jeuri ya Yussuf Manji

Mon, 11 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Nyakati zinakuja na nyakati zinakwenda. Ndio maisha ya mwanadamu. Hakuna nyakati zitakazodumu milele.

Ni kama zilivyokuwa nyakati za Wema Sepetu katika ulimbwende nchini. Kuna nyakati kila mwanamke alitamani kuwa kama Wema. Alitikisa kila mahali. Alitikisa wanaume na wanawake wenzake. Ndio Wema Sepetu.

Nyakati zake zikapita. Sasa kuna hawa kina Hamisa Mobeto na wengineo. Ni nyakati zao.

Ndivyo ilivyo katika soka. Wapo matajiri wengi wamekuja na kuondoka, ila ni wachache ambao wameacha alama kubwa za kukumbukwa. Ni kweli.

Pale Yanga amewahi kutokea tajiri mmoja anaitwa Abbas Gulamali. Alikuwa chizi wa soka. Alifanya vitu vya kushtua. Alisajili wachezaji wa gharama kubwa. Aliiweka timu kwenye hoteli za kisasa. Alitoa posho za maana kwa wachezaji. Yanga ikawa tishio kwelikweli. Gulamali ndio alimfanya Azim Dewji wa Simba aone ugumu wa kusimamia na kuendesha timu. Hakuweza kabisa kufanya alichokuwa anafanya Gulamali.

Hizi ndio nyakati zake. Watu wa Yanga wanamkumbuka mpaka kesho. Aliweka heshima kisha akaenda zake.

Baada ya miaka mingi akaibuka Bilionea, Yusuf Manji. Tajiri wa soka. Aliifanya Yanga kuwa tishio kwelikweli.

Manji akiwa mfadhili wa Yanga miaka ya 2006 -2012, alimwaga fedha za maana. Alisajili wachezaji wakubwa. Nani amesahau namna Manji alivyoweza kumtoa Juma Kaseja pale Simba na kumpeleka Yanga mwaka 2008.

Kaseja alikuwa ni Simba. Alikuwa mchezaji tegemeo sana pale Simba. Nani alifikiria kama angeweza kwenda Yanga? Hakuna. Kaseja alikuwa Simba na Simba ilikuwa Kaseja.

Nakumbuka kiongozi mmoja wa Simba aliwahi kuniambia Kaseja alipowaambia ofa aliyopewa na Yanga, walimruhusu kwa moyo mmoja kwenda. Ilikuwa ni fedha ambayo wasingeweza kumpa kwa wakati ule. Huyu ndiye Manji.

Kuna nyakati Manji alilipa viingilio ili mashabiki waingie bure kwenye mechi za Yanga. Alifanya kila anachoweza kuwafanya watu wa Yanga kuwa na furaha.

Alipokuwa mwenyekiti kuanzia 2012 alifanya makubwa zaidi. Alifanya usajili mkubwa. Aliiweka timu kwenye hoteli kubwa. Aliajiri watendaji wa maana. Yanga ikawa taifa kubwa. Ikatawala soka la Tanzania kwa kadiri ilivyojisikia. Hii ndiyo sababu wakati Manji anaondoka pale Yanga majonzi na masikitiko yalikuwa makubwa sana. Nani angefanya zile sajili kubwa tena? Hakuna. Yanga ikaishia kuwa timu ya kuchangishana fedha mitaani. Ilihuzunisha sana.

Ndiyo sababu leo nimeamua kuandika kitu kuhusu GSM. Wamenikumbusha zile nyakati za Manji.

Wamefanya uwekezaji mkubwa sana pale Yanga. Wameirejesha Yanga kuwa tishio tena. Waliikuta Yanga ikiwa imechoka kama nguo ya mzee masikini. Haikuwa na nyuma wala mbele. Yanga haikuwa na uwezo wa kusafiri vizuri. Haikuwa na uwezo wa kulipa mishahara kwa wakati. Haikuwa na uwezo wa kusajili wachezaji wakubwa tena. Ndiyo nyakati hizi tulishuhudia wachezaji wa ajabu wakicheza Yanga.

Nini kimetokea baada ya GSM kuingia pale Yanga? Ndiyo hiki tunachokiona sasa. Wameifanya Yanga kuwa kubwa tena, si tu hapa nchini, bali hata nje ya mipaka. Nani aliwaza kama Yanga ingecheza fainali ya mashindano ya CAF? Hakuna, ila kwa GSM imewezekana.

Ni gharama kubwa sana kusajili wachezaji wa maana. Mchezaji wa bei ya kawaida tu huwezi kumpata kwa chini ya Sh 200 milioni. Hebu fikiria hawa kina Aziz Ki, Maxi Nzengeli, Zouzoua Pacome, Yao Kouassi na wengineo wamesajiliwa kwa fedha kiasi gani? Ni pesa nyingi sana.

Leo Yanga inakaa kambini pale Avic Town, Kigamboni. Eneo fulani hivi la kitajiri. Inafanya mazoezi hapohapo. Inafanya mazoezi pale Gymkhana, Posta pia. Ni uwanja wa gharama kubwa lakini GSM amefanya kila kitu kiwezekane.

Leo hii Yanga ikienda kucheza mchezo wowote mkoani inakwenda kwa usafiri wa anga. Mishahara inatoka kwa wakati, na wachezaji wanapewa posho kubwa.

Ndiyo sababu Yanga imeweza kurejesha ufalme wake kwenye Ligi Kuu. Baada ya Simba kutawala kwa miaka minne ikiwa na jeuri ya fedha za Mohamed ‘Mo’ Dewji, alihitajika tajiri pale Yanga wa kuja kushindana naye.

Simba ya Mo Dewji ilifanya usajili mkubwa. Iliwaleta nchini kina Clatous Chama, Meddie Kagere, Luis Miquissone, Larry Bwalya na wengineo. Simba ilikuwa inatisha ndani na nje ya uwanja. Yanga ingewezaje kushindana na Simba hii bila kuwepo kwa mtu mwenye jeuri ya fedha? Ni ngumu.

Yanga isingeweza kushindana na Simba kwa zile fedha za kuchangishana mitaani. Isingewezekana. Ndiyo sababu nasema GSM anaacha alama kubwa pale Yanga. Historia itamkumbuka sana.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: