Klabu ya Yanga inahitaji ushindi katika mchezo wao wa marudiano dhidi ya Rivers United na mabosi wa klabu hiyo wameweka Sh milioni 300 mezani ambazo ni sawa na zile walizokuwa wapewe kama wangeifunga Simba kwenye mechi ya watani wa jadi.
Tajiri wa Yanga, Gharib Said akishirikiana na vigogo wengine wa Yanga wameweka mikakati mizito kuhakikisha rekodi inaandikwa bila kujali ushindi wa mabao 2-0 waliopata ugenini.
Taarifa hiyo imewashtua wachezaji wa timu hiyo kambini kwani ni kiwango kikubwa cha bonasi msimu huu tangu waanze mashindano ya CAF kuanzia Ligi ya Mabingwa Afrika hadi Kombe la Shirikisho wanaloendelea nalo sasa.
Msimu huu Yanga walikuwa wakivuna kuanzia sh 50 milioni kwa mchezo wa sare ugenini lakini pia sh 100 milioni kwa ushindi dhidi ya Real Bamako ya Mali hapa nyumbani lakini pia sh 150 milioni kule ugenini waliposhinda dhidi ya TP Mazembe na kuongoza hatua ya makundi.
Yanga waliahidiwa kiasi cha sh 450 katika mchezo dhidi ya Simba waliolala kwa mabao 2-0 ikiwa uongozi wa klabu ukitoa sh 150 milioni huku mfadhili wao GSM akitoa ahadi ya sh 300 milioni.
Tayari uongozi wa Yanga ulifanya hatua moja kubwa kabla ya kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Simba na hata Rivers ugenini wakilipa bonasi zao zote za mechi walizoshinda nyuma sambamba na mishahara hatua ambayo iliwapa mzuka wachezaji na kudhamiria kushinda ugenini dhidi ya Wanaigeria.
Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji alifichua kuwa kikao ambacho walikifanya nchini Nigeria dhidi ya wachezaji anaamini watatekeleza ahadi yao.
Arafat aliyeambatana na timu hiyo nchini Nigeria akiwa na rais wake Hersi Said alisema wachezaji wa timu hiyo waliitisha kikao maalum cha kusisitiza wanahitaji ushindi katika mchezo wa marudiano huku wakiwapa uongozi kazi ya kuwahamasisha mashabiki wao kuja kwa wingi uwanjani.
"Wachezaji tumewaambia hatutaki kusikia kitu zaidi ya ushindi katika hii mechi na tumewataka waachane na mawazo ya kushinda kule lakini nao wametuomba tuwaite kwa wingi mashabiki wetu,"alisema Arafat licha ya kutotaja kiasi cha fedha.
"Wanataka kuwaona mashabiki wao kwa wingi uwanjani kama ambavyo walijaa katika mchezo wa mwisho hapa nyumbani na ikiwezekana waongezeke ili waweke historia kwa pamoja wakitambua kwamba waliwaangusha mara ya mwisho walipocheza hapa nyumbani na sasa wanataka kuwafurahisha.
"Tunachukua kila tahadhari dhidi ya wapinzani wetu ili wasije kuharibu mipango yetu hapa nyumbani kwenye soka kila kitu kinawezekana kwamba kama tulishinda kwao nao wanaweza kuja kushinda hapa kama tukiwaruhusu kwa kufanya makosa, tunafanya vikao na makocha kuweka kila kitu sawa hili ni muhimu likaeleweka kwa watu wetu."
MAKOMANDOO Katika Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi kulikutwa makundi makubwa ya wanachama wa timu hiyo maalum kwa ulinzi wa timu yao maarufu kwa jina la makomandoo wakiwa wameuzingira uwanja huo kwa madai ya kulinda hujuma dhidi yao.