Jumamosi ya Juni 10, 2023 Yanga imekanyaga aridhi ya Dar es Salaa ikiwa na shangwe, ikitokea mkoani Mbeya ambako ilikabidhiwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara, baada ya kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Prisons.
Baada ya kutua uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarege Nyerere (Teminal 2), wachezaji, viongozi na makocha wamezungumzia furaha ya mafanikio yao msimu huu.
Kwa furaha aliyokuwa nayo kocha wa timu hiyo, Nasredine Nabi amejikuta akizungumza Kiswahili kwa ufupi, akiwapongeza mashabiki wa Yanga, huku uso wake ukiwa umejaa tabasamu.
"Hongera sana Yanga, hongera mashabiki kwa ubingwa huu." kisha akaondoka zake.
Kwa upande wa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Arafat Haji amesema "Tuna furaha kuipa Yanga taji la 29, tunawapongeza mashabiki kwa ushirikiano wao."
WACHEZAJI
Winga wa timu hiyo, Farid Mussa amesema "Tuna furaha sana kuandika histori kubwa kwenye soka la Tanzania, tunawashukuru makocha, viongozi na mashabiki kwa ushirikiano wao.
Kwa upande wa beki Abdallah Shaibu 'Ninja' ambaye hakucheza kabisa msimu uliomalizika amesema "Nina furaha isiyoelezeka kutokana na mafanikio ambayo klabu yangu imepata."
Wakati huo mashabiki wakiomba kupiga picha za ukumbusho na wachezaji kama Fiston Mayele, Metacha Mnata na wengine wengi kulingana na nafasi wanazozipata.