Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fufa yazindua mpira kumuenzi sokwe Zakayo

Fufaaaa Fufa yazindua mpira kumuenzi sokwe Zakayo

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (Fufa), limezindua mpira mpya utakaotumika katika Ligi Kuu nchini humo (UPL) uliopewa jina la Zakayo kwa heshima ya kumuenzi sokwe maarufu wa Uganda aliyekufa mwaka 2018.

Zakayo alikuwa sokwe wa kwanza kuishi muda mrefu katika Hifadhi ya Wanyama ya Entebbe alimoishi tangu mwaka 1964, na alikuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii na wageni nchini humo.

Sokwe aliyeitwa Zakayo

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika jengo la Fufa Mengo, jana, Februari 16, 2024, Rais wa Fufa, Moses Magogo alieleza kwamba wazo hilo litasaidia shirikisho hilo kuboresha chapa yake mpya ya 'Janzi'.

"Janzi ni chapa ya biashara iliyosajiliwa ambayo itasaidia Fufa kuepuka madalali. Sote tunajua kuwa watengenezaji wa vifaa kadhaa hawana viwanda, bali hutengeneza na kutuuzia wapate faida," amesema Magogo.

Janzi ni moja ya kampuni iliyoshiriki katika utengenezaji wa mpira wa Zakayo na pia inazalisha jezi, mifuko ya kusafiria, track suit, kofia, vikombe na miavuli nchini Uganda.

Katibu mkuu wa Fufa, Edgar Watson alifichua kwamba sababu ya kuuita mpira huo Zakayo ni kumuenzi Sokwe huyo aliyewahi kuwa maarufu na umetengenezwa kwa kuzingatia mitindo ya kisasa kwa maana ya umbo, muundo na uimara hasa unapojongea.

"Mpira huu utakaotumika katika ligi ulitengenezwa kwa kuzingatia urithi wetu kama Waganda. Jina rasmi la mpira ni Zakayo - sokwe maarufu mwenye historia ndefu iliyoanza 1963 katika mbuga ya kitaifa ya Semliki l, lakini baadaye alihamishiwa kwenye Mbuga ya Wanyama ya Entebbe alikoishi hadi akafa mnamo 2018," amesema Watson.

Mpira huo una sehemu ya rangi tatu zilizopo kwenye bendera ya Uganda ambazo ni nyeusi ikiwakilisha watu wa Uganda, njano jua na mazingira ya kitropiki nchini humo pamoja na nyekundu ikiwa na maana ya damu ya mashujaa waliopigania uhuru wa nchi hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti