Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Friends of Simba wamerudi kazini

Kaburu Pic Data Friends of Simba wamerudi kazini

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tajiri na kipenzi cha mashabiki wa Simba, Mohammed Dewji ameteua wajumbe 21 wa Baraza la Ushauri ambao kati yao 13 ni kutoka kwenye kundi lenye nguvu la Friends of Simba.

Duru za ndani ya Simba zinasema kuwa uteuzi huo ambao vigogo saba waliwahi kuwa viongozi wa klabu hiyo, unalenga zaidi kuongeza nguvu kwenye mechi dhidi ya Yanga Jumapili pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba iliyoivua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Zamaleki ya Misri mwaka 2003, asilimia kubwa ya wajumbe hao ndio waliohusika chini ya kundi hilo lililoanzishwa mwaka 1999.

Vigogo hao waliibeba Simba katika nyakati zote ingawa mchakato wa mfumo wa uendesha ulipoanza miaka mitano nyuma kundi hilo lilipoteza nguvu, hii huenda ni mfumo huo ulipoanza kufanya kazi chini ya Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ambaye ni mwekezaji wa Simba.

Baada ya mchakato huo kuanza na kufanyika uchaguzi wa klabu mambo yalibadilika, Simba inaendeshwa na Bodi ya Wakurugenzi ambayo awali ilikuwa chini ya Mwenyekiti Mo Dewji ingawa kwasasa inaongozwa na Salim Abdallah ‘Try Again’.

Mo Dewji ambaye ni Rais wa Heshima ameteua wajumbe hao na kueleza kuwa pamoja na kupiga hatua lakini bado hawajafikia malengo yao hivyo kuongeza baraza hilo anaamini watafikia malengo. MO Dewji amekiri kuwa mojawapo ya majukumu yake kama Rais wa Heshima ni kuhakikisha Uongozi na Utawala bora kila wakati.

Kazi kubwa ya Baraza hilo ni kuishauri Bodi ya Wakurugenzi juu ya maendeleo ya Klabu, Uongozi na Utawala bora

Wajumbe walioteuliwa kutoka Friends ni Thomas Mihayo, Evans Aveva, Kassim Dewji, Musleh Al-Ruweh, Mohamed Nassor, Mulamu Ng’ambi, Prof Janabi, Hassan Kipusi, Geofrey Nyange, Gerald Yambi, Moses Kaluwa, Crescentius Magori na Juma Pinto.

Wengine ambao waliwahi kuwa viongozi wa klabu hiyo ni Hassan Dalali, Ismail Aden Rage, Swedi Mkwabi ambao hawa waliwahi kushika nafasi ya Mwenyekiti kwa nyakati tofauti, Faroukh Baghoza, Azim Dewji, Octavian Mshiu, Mwina Kaduguda na Idd Kajuna.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya uteuzi huo, Kaburu ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa klabu hiyo alisema; “Kwanza nashukuru na nimeupokea wito wa kuteuliwa, ndio hiki ni kikosi kazi lakini ifahamike hilo ni baraza tu la ushauri, tukiletewa jambo tutalijadili na kuwashauri, yote haya ni kuhakikisha tunaleta maendeleo ya klabu yetu, kama ilivyo kauli mbiu ya Simba Nguvu Moja.”

“Ukiangalia majina yalioitwa asilimia kubwa ni wanachama waandamizi wa Simba na wengi waliwahi kuwa viongozi, naamini kama tutapewa jambo tutalifanya vizuri, wote tunaifahamu kiundani timu yetu.”

Kauli yake iliungwa mkono na Dalali aliyesema; “Nashindwa kuzungumza mengi kwasababu bado sijapata barua, lakini nimefurahia uteuzi wao, Simba ni ya kila mtu ndio maana tumetoka matawi tofauti.”

Chanzo: Mwanaspoti