Uongozi wa Tanzania Prisons umesema unaimani na kocha wao Fred Felix ‘Minziro’ kuwafikisha katika malengo wanayoyatarajia kwa msimu huu wa 2023/24 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kuibuka tetesi kuwa uongozi huo umempa kocha huyo mechi tatu asipofanya vizuri kibarua chake cha kukinoa kikosi cha timu hiyo kitakuwa mashakani baada ya kutofanya vizuri kwenye mechi tatu za ligi hiyo walizocheza wakiambulia alama moja huku wakishika mkia kwenye msimamo.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Enock Manguku amesema hakuna ukweli juu ya tuhuma hizo kwa sababu wanaimani na Minziro anaweza kuwafikisha kwenye malengo yao kwa msimu huu.
Amesema wanatambua ligi ni ngumu na ndio kwanza imeanza hivyo kupata alama moja kwenye michezo mitatu bado hakuwafanyi kumtimua kocha wao huyo.
“Pamoja kuwa hatukuanza vizuri lakini bado hatuwezi kumpa mtihani kocha, tunaimani naye na ataendelea kukinoa kikosi chetu kwa sababu ni mapema sana na ligi ndio imeanza na timu inatengeneza muunganiko kwa wachezaji wapya na wale wa msimu uliopita,” amesema Manguku
Amesisitiza kuwa bado Minziro ataendelea kukinoa kikosi cha timu hiyo na kwa sasa anaendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi zilizopo mbele yao ukiwemo mchezo unaofuata dhidi ya Simba SC.
Katika mchezo huo Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wakiwakaribisha Simba SC, Oktoba 5 huku wakiwa na kibarua cha kusaka pointi tatu muhimu kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.