Aliyekua Kocha Mkuu wa Klabu za Biashara United Mara na Kagera Sugar Francis Baraza, amesema Simba SC bado ina nafasi kubwa ya kutinga Hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Simba SC itacheza mchezo wa Mzunguko watatu wa Kundi C, dhidi ya Mabingwa wa Uganda Vipers SC Jumamosi (Februari 25), huku ikipoteza michezo miwili iliyopita dhidi ya Horoya AC (Guinea) na Raja Casablanca (Morocco).
Baraza amesema kwa namna anavoifahamu Simba SC, anaamini timu hiyo ina uwezo wa kupambana na kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi C, hivyo kinachotakiwa kwa sasa ni kuaminiwa kwa Kocha Robertinho na Wachezaji wake.
Kocha huyo kutoka nchini Kenya amesema mbali na kuamini hivyo, bado kuna kazi kubwa kwa Benchi la Ufundi na Wachezaji wa Simba SC kuhakikisha wanasahau yaliyopita na kuangalia mchezo unaofuata ambao wanapaswa kushinda.
“Nikizungumzia kiufundi kwa upande wa Simba kitu kimoja ni kumwamini kocha pamoja na timu yake kwa ujumla na kumpa sapoti yote maana bado kuna chance (nafasi) kubwa ya kusonga mbele, bado kundi lao liko wazi endapo itashinda mechi ya Vipers ya Uganda,”
“Simba ninavyo itambua ina uwezo mkubwa wa kumaliza katika nafasi ya pili ikiwa itaweka kando mechi zilizopita na kuangalia mechi zilizosalia. Nawashukuru viongozi wa Simba na Yanga kwa kufanya kila juhudi kuhakikisha timu timu zao zinafika hatua ya makundi, siyo kazi rahisi kama watu wanavyo fikiria.”
Kuhusu Young Africans, Kocha Baraza amesema timu hiyo inatakiwa kuendelea kupambana na kucheza soka zuri na lenye kiwango kama ilivyokuwa kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe, ili wafanikiwe kufikia ndoto za kuvuka Hatua ya Makundi.
“Kwa upande wa Yanga wasibweteke na matokeo dhidi ya TP Mazembe na kama itaweza kucheza vile ilivyocheza kama team, area zote ilicheza kwa kujiamini nidhamu ya hali ya juu na kutumia few chances walizo zipata inawapa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwa mechi zilizo salia,” amesema Baraza
Young Africans itacheza mchezo wa Mzunguko watatu wa Kundi D Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya AS Real Bamako Jumapili (Februari 26), katika Uwanja wa Machi 26 mjini Bamako.