Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana, amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameialika bungeni timu ya wasichana ya mpira wa miguu ya Fountain Gate, baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika kwa Shule za Sekondari wiki iliyopita nchini Afrika Kusini.
Chana amesema sambamba na mualiko huo ambao utafanyika Aprili 13, 2023 jijini Dodoma, pia wizara yake itatoa zawadi ya Sh milioni 10 kwa mabingwa hao.
Balozi Dk Chana amewapokea mabingwa hao leo Aprili 11, 2023 jijini Dar es Salaam, ambapo ameupongeza uongozi wa timu hiyo chini ya Mkurugenzi, Japhet Makau kwa kuendelea kuthibitisha ubora wa benchi la ufundi kwa kufanya maandalizi sahihi ya timu na kupata matokeo chanya.
"Nakumbuka mara ya mwisho mliniahidi kutwaa ubingwa wa CECAFA tulipokutana Chamazi katika mashindano ya ukanda wetu wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, na kweli mkatwaa ubingwa huo, mara ya pili tulipokutana tarehe 31, Machi 2023 mkaniahidi kutwaa ubingwa wa Bara zima la Afrika katika mashindano yaliyofanyika Afrika Kusini na kweli mkatekeleza ahadi yenu," amesema Balozi Chana.
Kwa upande wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema zawadi ya Dola 300,000 waliyopata mabingwa hao imeelekezwa iende katika ujenzi wa miundombinu ya michezo katika shule hiyo.