Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Flora, binti wa miaka 25 anayemiliki timu

Svg Flora, Binti Flora, binti wa miaka 25 anayemiliki timu

Wed, 27 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

“Nilithubutu kwa ujasiri bila kujali umri wala kipato changu, kwani niliamini hakuna anayeijua ndoto yangu katika mpira na hakuna anayeweza kuiamini kwa haraka hadi nioneshe kwa vitendo,” ndivyo anavyosema mmiliki wa klabu ya soka la wanawake ya Ukerewe Queens, Flora Mchulo mwenye umri wa miaka 25.

Flora, aliyeanza kama mchezaji wa soka tangu akiwa shuleni ni mwanzilishi na mmiliki wa timu hiyo yenye maskani wilayani Ukerewe, Mkoa wa Mwanza inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Wanawake Bara (WFDL), ambapo msimu huu ilikaribia kidogo tu ipande Ligi Kuu, kwani iliishia nusu fainali na kukamata nafasi ya nne, huku Bunda Queens na Geita Gold Queens zikienda Ligi Kuu (WPL).

Mwanaspoti limefanya mahojiano na Flora ambaye ni mtaalamu wa maabara na mjasiriamali alifunguka namna ambavyo ndoto yake ilianza, alivyoikamilisha, changamoto alizopitia, anavyomudu kugawa majukumu na vikwazo mbalimbali vilivyokaribia kumkatisha tamaa na kutaka kuiuza timu hiyo.

NDOTO ILIVYOANZA

Mkurugenzi huyo anasema alikuwa mchezaji wa soka na pete tangu akiwa shule ya msingi hadi sekondari huku akiwa na ndoto ya kucheza soka la kimataifa lakini maono yake yaliyeyuka baada ya kukosa sapoti ya kuendelezwa, ndipo akiwa kidato cha tano akajiwekea malengo ya kuyatimiza maishani mwake.

“Niliandika kwenye diary yangu kwamba siku moja nianzishe timu ya mpira wa miguu ya wanawake au niwe kiongozi kwenye timu yoyote ya soka la wanawake, kwahiyo maisha yangu yote nilitembea na hayo mambo mawili na niliona watoto wa kike wana vipaji vya soka lakini hawapati fursa ya kuendelezwa ili kufikia malengo yao,” anasema Flora na kuongeza;

“Niliona mpira ni ajira, hivyo badala ya mtoto wa kike kukaa mtaani na kuzaa kabla ya umri wakati ana kipaji ni bora ahangaikie kipaji chake ili atimize ndoto zake, mwaka 2020 nilianza kampeni ya kutafuta wasichana wanaoshi katika mazingira magumu wenye vipaji vya soka.

“Mungu alisaidia nikapata wengi na nikapata kibali serikalini cha kuwasaidia, kuishi nao na kuwasaidia kielimu, nikatafuta mipira na mwalimu wa kuwafundisha tukapata usajili wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na huo mwaka tukashiriki Ligi Daraja la Kwanza Dodoma tukipewa sapoti ya wadau na viongozi mbalimbali wa serikali,” anasema Flora

NGUMU KUMILIKI TIMU

Mmiliki huyo anasema haikuwa rahisi kuanzisha timu hiyo kwani amepitia changamoto za kutokuwa na fedha za kutosha, ugumu wa kupata wachezaji wengi kutoka maeneo jirani wenye uwezo wa kutokea kwao kwenda kufanya mazoezi hivyo ikamlazimu kuwa na kambi ya kuwaweka pamoja ili kuwaepusha na vishawishi mbalimbali.

“Hatukuwa na vifaa vya michezo vya kutosha hasa jezi, mipira na viatu, hatukuwa na mdhamini wa kudumu ambaye angeibeba timu na kutusaidia kuiendesha, pia kulikuwa na changamoto ya uelewa wa watoto wa kike kucheza soka tulitumia nguvu kubwa kuwaelimisha wazazi hadi kukubali kuwaruhusu watoto wao,” anasema.

ANAVYOIENDESHA

Flora, anatumia vyanzo vyake vidogo vya mapato kuendesha timu hiyo na nguvu ya michango ya wadau.

“Mimi ni mjasiliamali nafanya biashara ya urembo na vifaa vya saluni na nina taaluma ya maabara (Medical Lab technician), pia, tunategemea msaada kutoka kwa wadau ambao kwa kiasi kikubwa wanajitoa sana kuisapoti timu yetu,” anasema.

ALIWEZAJE KATIKA UMRI HUO

Anasema licha ya kufikia hatua hiyo bado anakutana na vitu vingi vya kukatishwa tamaa ikiwamo kudharauliwa, kuchekwa, kunenewa mabaya na kuchonganishwa lakini anawasihi wasichana kujisimamia na kupambania ndoto zao mpaka mwisho bila kujali changamoto wanazopitia.

“Nilithubutu kwa ujasiri mkubwa bila kujali umri wala kipato kwa sababu niliamini ndiyo maana niliweza na nilipambana sana kwa moyo wa dhati na watu wakaona matokeo, ingawa siyo wote wanaoweza kukubali jitihada zangu lakini napambana mpaka sasa kuhakikisha ndoto ya kuifikisha Ukerewe Queens Ligi Kuu inakamilika,” anasema na kuongeza;

“Natamani kuwaona vijana wenzangu wanatimiza ndoto zao kupitia vipaji walovyojaliwa na Mwenyezi Mungu, natamani kuwaona wasichana wenzangu wanajisimamia na kupambana kwa bidii na kujikubali kwa wanachokipambania.”

INAVYOATHIRI MAHUSIANO

“Kupanga ni kuchagua ni kweli lakini ukishaamua kufanya vitu vya kijamii kama hivi basi ukiamua kuingia kwenye uhusiano uchague kwanza mwanaume mnayeendana, anayekubali harakati zako na anayekusapoti na hasa kwenye soka awe anajua na kupenda mpira hata walau kidogo,” anasema Frola na kuongeza;

“Nina mchumba na ananisapoti kwa kila jambo na muda wangu na-mantain vizuri bila kuathiri uhusiano wetu. Timu ina uongozi uliokamilika mimi ni mkurugenzi, yupo katibu wangu, benchi la ufundi limekamilika na kuna matroni, hivyo kila anatekeleza majukumu yake.”

KIDOGO AKATE TAMAA

“Mwaka jana nilikata tamaa sikuwa na maandalizi ya timu kutokana na shida ya kifamilia nikakosa fedha, lakini TFF walinisihi nifanye usajili ili nipeleke timu kwenye mashindano isishushwe daraja,” anasema na kuongeza;

“Nilipambana nikapata wachezaji wachache wakasafirisha kwenda Dodoma, nilikodi gari nikiwa na Sh300,000 dereva alitaka Sh900,000. Nilijitoa mhanga nikasema ni bora timu ifike mimi nikalale rumande, Mungu alisaidia kufika Singida nikaanza kupokea michango kutoka kwa wadau tukashiriki mashindano na kurudi salama.

“Baada ya kurudi viongozi wakawa wananipigia simu wanadai nimekula fedha ndiyo maana timu ikawa ya mwisho lakini hawakujua changamoto nilizopitia. Mwaka huu tumeshiriki tena na kuishia nusu fainali.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live