TIMU ya Yanga imeingia hatua ya 16 ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ken Gold katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana.
Bao hilo pekee lilifungwa na Fiston Abdulrazak dakika ya 42 kwa penalti baada ya mchezaji wa Ken Gold kunawa mpira eneo la goli.
Ni mara ya kwanza kwa mshambuliaji huyo kufunga bao tangu kujiunga na Yanga katika usajili wa dirisha dogo, Januari, mwaka huu.
Katika mchezo huo Yanga ilimiliki mpira vipindi vyote na kutengeneza nafasi ila wapinzani wao walionekana kuwa makini kulinda lango lao na kucheza kwa kujihami hadi kumalizika kwa mchezo.
Pamoja na Yanga kutengeneza nafasi nyingi walishindwa kuzitumia kwa kukosa umakini lakini pia kipa wa Ken Gold, Adam John alikuwa makini kuokoa mipira mbalimbali kwenye lango lao.
Pia dakika ya 81, Carlos Carlinhos aliyeingia dakika ya 66 kuchukua nafasi ya Ditram Nchimbi alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga ngumi mchezaji wa Ken Gold.
Yanga inaungana na Simba, Kagera Sugar, KMC, Mwadui, JKT Tanzania, Polisi Tanzania, Ruvu Shooting, AFC na Rhino FC ambazo zimefuzu hatua ya 16.
Katika mchezo uliochezwa mapema Arusha katika Uwanja wa Agakhan, Polisi Tanzania iliifunga Kwamndolwa ya Tanga kwa mabao 4-0.
Mabao ya Polisi yalifungwa na Deusdedity Cosmas dakika ya 13, Daruwesh Saliboko dakika 26, Pius Buswita dakika ya 69 na George Mpole dakika ya 81.
Mechi nyingine zitakazochezwa leo Coastal Union itaikaribisha Ihefu FC katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga na Sahare all Stars dhidi ya Tanzania Prisons.