Mshindi wa Bao Bora la Mzunguko watano Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Mshambuliaji Fiston Kalala Mayele amesema wanahitaji wanazitaka alama tatu muhimu wa mchezo wa mwisho wa Kundi D, utakaowakutanisha na TP Mazembe mjini Lubumbashi mapema mwezi April.
Young Africans inayoongoza msimamo wa Kundi D kwa kufikisha alama 10, inahitaji kushinda mchezo huo ili kujihakikishia nafasi ya kubaki kileleni, kufuatia kufungana kwa alama na US Monastir ya Tunisia ambayo ilikubali kufungwa 2-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, jumapili (Machi 19).
Mshambliaji huyo kutoka DR Congo ameweka wazi kuwa kila mchezo ambao wanacheza katika michuano ya Shirikisho Barani Afrika ni muhimu kushinda ili kupata alama tatu ambazo wanazihitaji.
Mayele amesema wana mchezo mgumu dhidi ya TP Mazembe itakayokuwa nyumbani kwake Lubumbashi, lakini wanachohitaji ni kupata alama tatu, watakaposhuka katika Dimba la klabu hiyo nguli Barani Afrika.
“Kikubwa ni kupata pointi tatu iwe nyumbani ama ugenini, tunajua siyo kazi nyepesi ambacho tunakifanya ni kushirikiana na kupambana kupata matokeo mazuri kwenye mechi zetu ambazo tunacheza.”
Ikumbukwe kuwa bao la Meyele alilofunga dhidi ya US Monastir Uwanja wa Mkapa akitumia pasi ya mshikaji wake Kennedy Musonda limechaguliwa kuwa Bao Bora la Mzunguuko watano Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika.