Kocha Mkuu wa Young Africans, Nasredden Nabi ametoa sababu za kushindwa kumtumia Mshambuliaji kutoka DR Congo Heritier Makambo.
Makambo alirejea Young Africans wakati wa usajili wa msimu huu 2021/22, baada ya kuvunja mkataba wake na klabu ya AC Horoya ya Guinea.
Kocha Nabi amesema Mshambuliaji huyo anashindwa kutumika kwenye kikosi cha kwanza kutokana na ubora unaendelea kuoneshwa na Mshambuliaji mwenzake kutoka DR Congo Fiston Mayele ambaye tayari ameshafunga mabao mawili.
Hata Hivyo Kocha huyo kutoka nchini Tunisia anaamini Makambo atapata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza, kutokana na kikosi chake kukabiliwa na michezo mingi msimu huu, ili kufikia lengo la kuwa Mabingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
"Makambo atacheza tu, katika michezo ijayo kwani kuna michezo mingi mbele, lakini kwa sasa kilichotokea kinafahamika, timu ya ushindi huwa haibadilishwi mara kwa mara, Mayele anafanya vizuri sana ndio maana anatumika zaidi kuliko Makambo”
“Lakini pia ukiangalia kuna sheria ya kutumia wachezaji nane wa kimataifa kwenye mechi moja, hivyo wakati mwingine naye ataonekana,” amesema Kocha Nabi.
Kwa mara ya kwanza Makambo alitumika kwenye mchezo wa ‘Siku ya Wananchi’ dhidi ya Zanaco FC ya Zambia, na alifunga bao la kufutia machozi, baada ya Young Africans kukubali kichapo cha mabao 2-1.