Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

'First 11' ya wachezaji wa kike kimataifa

Llllllll 'First 11' ya wachezaji wa kike kimataifa

Fri, 16 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ubora wa ligi ya wanawake Tanzania (WPL) unaonekana kukua na hilo linathibitishwa kutokana na mastaa kusajiliwa katika ligi kubwa Ulaya.

Mfano mzuri ni nyota wa Brighton, Aisha Masaka aliyesajiliwa msimu huu akitokea BK Hacken ya Sweden, Clara Luvanga, Opah Clement na wengineo.

Kwa wingi wao na ubora wanaoonyesha kwenye klabu zao, Mwanaspoti limekutengenezea kikosi cha wachezaji wa kike wanaokiwasha nje ya Tanzania.

Lakini ndani ya kikosi hicho kuna uhaba wa makipa ambao hakuna golikipa wa kike aliyetoka nje ya mipaka ya Tanzania hivyo tumepanga kulingana na idadi kama ifuatavyo.

1. Julietha Singano (Juarez, Mexico)

Anacheza beki wa kati lakini pia ana uwezo wa kucheza mlinzi wa pembeni inategemeana na matakwa ya kocha.

Beki huyo alitambulishwa kikosini hapo mwaka 2022 akitokea Simba Queens na misimu miwili aliyocheza Mexico hakufanikiwa kuchukua ubingwa.

Kiraka huyo ambaye pia ana uwezo wa kucheza kiungo, akiwa na Simba alishinda mataji mawili.

2. Noela Luhala (Asa Tel Aviv, Israel)

Eneo asilia analocheza ni beki wa kati na amekuwa maarufu kwa ukataili wake uwanjani wa kusambaratisha mashambulizi.

Yanga Queens alidumu kwa misimu mitatu ingawa hakufanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi lakini aliisaidia Serengeti Girls kubeba taji la CECAFA kwa wasichana chini ya miaka 18 mwaka 2023.

Ubora aliounyesha kwenye misimu hiyo akiwa na Yanga umezifanya timu mbalimbali nchini hususani Simba kutaka saini yake lakini walishindwa kufua dafu baada ya Asa Tel Aviv kuwawahi.

3. Enekia Lunyamila (Mazaltan, Mexico)

Huyu ni kiraka anayeweza kucheza karibu kila eneo uwanjani ukitaka kukaba anaweza kukufanyia kazi hiyo vyema kabisa na hata kushambulia.

Wengi wamemzoea akicheza eneo la winga na kiungo mshambuliaji ambaye amekuwa akiipatia timu matokeo na kuibuka mfungaji bora.

Lunyamila kwa sasa unaweza kumfananisha na Mkongomani wa Yanga, Maxi Nzengeli ambaye ni msimu wake wa pili kucheza Jangwani lakini ni kama amezaliwa upya baada ya kufanya vizuri msimu uliopita.

Makipa waliokuwa wanashiriki Ligi ya Morocco hawawezi kumsahau baada ya kuwa na msimu bora mwaka 2021 akiifungia AUSFAZ ya Morocco mabao 49.

Kwenye timu alizopita makocha wamekuwa wakimtumia kwenye maeneo ya kushambulia lakini kikosi cha Twiga Stars amekuwa akitumika kama mlinzi.

4. Maimuna Khamis (Zed FC, Misri)

Anaifahamu vyema Ligi ya Wanawake (WPL) akicheza kwa zaidi ya misimu sita na ni miongoni mwa mchezaji waliocheza timu tatu zenye ushindani bara.

Cha ajabu huko kote alikopita ni kama alikuwa na kismati cha ubingwa akichukua mataji matano, matatu akiwa na Simba na mawili dhidi ya JKT lakini Yanga hakufanikiwa kuchukua.

Baada ya kuukosa ubingwa akiwa na Yanga akasajiliwa na Zed FC ya Misri ambako alikuwa na msaada mkubwa kwenye kikosi hicho.

Ni chaguo la kocha kumtumia kama kiungo namba sita, nane na 10 kwa kuwa namba zote anaweza kuzicheza kwa ubora mkubwa.

5. Suzana Adam (TUT FC, Misri)

Majeraha ndio jambo kubwa lililomuweka nje ya uwanja kwa msimu mzima sasa tangu asajiliwe klabuni hapo mwaka 2023 akitokea Fountain Gate Princess.

Kiungo huyo alikuwa na msimu bora mwaka 2022 akiwa na Fountain jambo lililowafanya mabingwa hao wa Misri kuvutiwa na kiwango chake na kumnunua akitokea Tanzania.

6. Diana Msewa (Amed SK, Uturuki)

Pasina shaka kwa viungo bora wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania huwezi acha kumtaja Diana Msewa.

Hakucheza muda mrefu ligi ya Tanzania akizitumikia timu tatu tu, Panama Girls (2016/2018), Ruvuma Queens (2018/2021) na Fountain msimu mmoja 2021. Kutokana na uwezo alioonyesha akasajiliwa na Ausfaz Assa Zag ya Morocco.

Kuna asilimia chache za kiungo huyo kusalia Amed Sk ya Uturuki kutokana na kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita.

7. Hasnath Ubamba

Kwenye kikosi hiki unaweza kumtumia kama winga wa pande zote mbili hata hivyo anaweza kutumika kama mshambuliaji wa kati.

Baada ya kuitumikia kwa misimu mitatu, klabu hiyo imemtoa kwa mkopo kwenda Zed FC ambako ndio msimu wake wa kwanza kuitumikia timu hiyo.

Ni mara ya kwanza kwa Ubamba kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na msimu uliopita kwenye ligi amefunga mabao matano.

8. Opah Clement (Henan Jianye, China)

Ni mara ya tatu kutoka kwenye mipaka ya Tanzania, msimu wa 2022 alitimkia Kayseri Kadın ya Uturuki ambako hakucheza muda mrefu akarudi tena Simba Queens.

Baada ya kurudi Simba, Besiktas ikaona uwezo wake na msimu uliofuata ikamsajili nako alidumu kwa msimu mmoja tu.

Ndani ya mwaka mmoja aliocheza Uturuki, nahodha huyo wa Twiga Stars alifunga mabao 12 kwenye mechi 30 za ligi hiyo na msimu huu tayari katambulishwa Henan Jianye ya nchini China akiwa Mtanzania pekee kwenye kikosi hicho.

9. Aisha Masaka (Brighton, England)

Mshambuliaji huyo wiki zilizopita alishtua vyombo mbalimbali vya habari baada ya kutambulishwa katika klabu ya Brighton & Hove Albion inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake England (Women's Super League) akitokea BK Hacken ya Sweden.

Kwa utambulisho ule anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kuichezea timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya wanawake nchini England ambako atachuana na timu za wanawake za Arsenal, Man United, Chelsea, Liverpool, Man City na kadhalika.

Ni fundi haswa wa kufumania nyavu na msimu wa 2020/21 alishinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara akifunga mabao 35.

10. Clara Luvanga (Al Nassr, Saudia)

Ndio supastaa wa wanasoka wa kike kutokana na umaarufu aliopata akiwa na Al Nassr inayoshiriki Ligi ya Wanawake Saudia ambako pia ni klabu moja na anayochezea staa wa dunia, Cristiano Ronaldo.

Achana na ile picha aliyopiga na staa huyo wa Ureno, lakini wengi wamevutiwa na uwezo wake uwanjani hasa wa kufumania nyavu.

Mshambuliaji huyo ameanza maisha kibabe sana huko akiwa tayari ana medali ya kombe la ligi ya Saudia walilolibeba msimu uliopita akiiwezesha timu hiyo kwa kufunga mabao 11.

11. Fatuma Ibrahim 'Didier Fetty' (Neesatromitou, Ugiriki)

Kiungo huyo wa zamani wa Yanga ni miongoni mwa wachezaji wanaofanya vizuri kimataifa licha ya kutozungumzwa sana lakini utaona maajabu awapo uwanjani.

Aliondoka Jangwani msimu wa 2022 akiitumikia Ligi ya Ugiriki kwa misimu miwili ambayo inatamatika msimu huu lakini amekuwa tegemeo kwenye kikosi hicho.

Chanzo: Mwanaspoti