Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Filamu nzima ya Ateba kutua Simba

Lionel Atteba Simbaaa Filamu nzima ya Ateba kutua Simba

Fri, 16 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba imeshamshusha straika mpya Lionel Ateba baada ya kufikia makubaliano na USM Alger ya Algeria kwa ajili ya uhamisho wa raia huyo wa Cameroon ili kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Wekundu iliyopo chini ya kocha Fadlu Davids aliyehitaji kuboreshewa zaidi eneo hilo.

Hata hivyo, wakati Simba inafanikisha uhamisho wa mshambuliaji huyo anayetazamiwa kuongeza nguvu eneo hilo, inaelezwa kuwa, haikuwa rahisi kumnasa kutokana na ugumu kiasi cha kocha na skauti wa timu hiyo kuumiza kichwa.

Wakati mchakato huo unaanza skauti wa Simba, Mels Daalder alimpendekeza mshambuliaji wa Red Arrows kutoka Zambia, Ricky Banda, ingawa mchambuzi wa video (video analyst), Mueez Kajee akaweka pingamizi akidai hawezi kuendana na mfumo wa Fadlu.

Baada ya hapo Fadlu akapewa jukumu na viongozi la kuchagua mshambuliaji anayemtaka alipendekeza majina matatu ambayo ni Leonel Ateba aliyekuwa USM Alger, Muethiopia Abubeker Nassir aliyepo Mamelodi Sundowns na Mrundi, Elvis Kamsoba.

Viongozi wa Simba baada ya kuwafuatilia nyota hao wakabaini urahisi zaidi ni wa kumpata mshambuliaji, Nassir kwa sababu hana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambacho kimesheheni nyota wengi wakali.

Licha ya kuona urahisi huo, viongozi wa Simba wakamfanyia tathimini ya haraka mchezaji huyo na ndipo wakajiridhisha kwamba, Nassir ni mshambuliaji mzuri ila ana tatizo la kupata majeraha ya mara kwa mara, hivyo wakasitisha mpango naye.

Uchambuzi ukaendelea hadi kwa Mrundi, Elvis Kamsoba ambaye ni mchezaji huru kwa sasa baada ya kuachana na Perserikatan Sepakbola Sleman ya Indonesia huku akiwahi kuzichezea timu mbalimbali za Melbourne Victory FC na Sydney FC za Australia.

Uzoefu wa mchezaji huyo ukawavutia mabosi wa Simba ila mwishoni ukaachana naye baada ya kujiridhisha hana fitinesi ya kutosha na atakapotua nchini inabidi apewe programu maalamu ya wiki moja hadi mbili, jambo ambalo hawakukubaliana nalo.

Baada ya machaguo hayo ndipo ikafikia makubaliano na USM Alger ya kumpata Ateba ambaye haikuwa rahisi pia japo kitendo cha mchezaji mwenyewe kuomba kuondoka ili akatafute changamoto sehemu nyingine kilirahisisha dili.

Sababu kubwa ya mchezaji huyo kuomba kuondoka ni kitendo cha kuchezeshwa winga na mara nyingine amekuwa akicheza namba 10, nyuma ya mshambuliaji raia wa Mali, Abdoulaye Kanu, jambo ambalo limemfanya Ateba kuomba kuondoka kikosini humo.

Ateba alijiunga na USM Alger Januari mwaka huu akitokea Dynamo Douala FC ya kwao Cameroon huku msimu uliopita nyota huyo alihusika katika jumla ya mabao tisa akiwa na timu hiyo, akifunga moja na kuasisti manane katika michezo 16.

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali za Coton Sport na PWD Bamenda, anakumbukwa zaidi mwaka 2023 ambapo ndiye alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Cameroon baada ya kufunga mabao 21, yaliyomfanya kuitwa katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alithibitisha timu hiyo kushusha mshambuliaji mpya na licha ya kutotaka tu kuweka wazi ila Mwanaspoti linatambua nyota huyo ni Ateba, na muda wowote kuanzia sasa atatangazwa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: