MTAANI mashabiki wa Simba bado hawaamini Kaizer Chiefs walichomokaje kwa Mkapa ndani ya kipigo cha mabao 3-0 kwa jinsi jeshi lao lilivyopiga mpira mwingi wakilaumu kutoingizwa kwa mshambuliaji wao, Meddie Kagere lakini kumbe straika huyo hata angeshuka MO Dewji asingeingia.
Iko hivi, mashabiki wa Simba wanaona mshambuliaji wao, Chris Mugalu alistahili kumpisha Kagere mapema tu wakiamini mfungaji wao bora huyo msimu uliopita kama angeingia asingeweza kupoteza nafasi kama Mugalu.
Simba imelitoloea ufafanunuzi hilo wakisema hata kama ingekuwa vipi Kagere asingeingia au Mugalu kutoka kwa vile tayari Kanuni mpya za FIFA kuhusu sub za Corona zilizuia mabadiliko hayo.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amelifafanulia Mwanaspoti mabadiliko ya kumwingiza Kagere yalizuiwa na mabadiliko hayo ya kanuni za FIFA na bodi ya IFAB na kumfanya Mugalu aendelee kubaki uwanjani.
Mabadiliko hayo ya Bodi ya Soka ya Kimataifa(IFAB) na FIFA katika sheria ya 3 ya mchezo ilibadili nafasi za mabadiliko ya wachezaji kuwa watano kutoka zile za awali tatu sheria iliyoanza kutumia Juni mosi mwaka jana.
Sheria hiyo inaelekeza mabadiliko hayo ya wachezaji watano yatafanyika kwa mikupuo mitatu tofauti ndani ya mchezo mmoja. Rweyemamu alifafanua katika matumizi ya sheria hiyo Simba ilitumia mkupuo wa kwanza kwa kumtoa kiungo Mzamiru Yassin dakika ya 24 kisha nafasi yake kuchukuliwa na winga Bernard Morrison.
“Makocha walifanya mabadiliko yale wakitaka kuongeza kasi ya kutengeneza nafasi za kufunga zaidi na hatukuwa na haja ya kuongeza ulinzi zaidi huo ukawa mkupuo wa kwanza,” alisema Rweyemamu.
Meneja huyo alifafanua shida ilikuja katika matumizi ya mkupuo wa pili na wa tatu na tukio la kuumia kwa mpigo kwa wachezaji wao wawili kiungo Thadeo Lwanga na beki Joash Onyango ndio shida ilipokuja.
Alisema baada ya wachezaji hao kuumia dakika ya 34 madaktari waliona Lwanga hataweza kuendelea na kutakiwa kutolewa haraka na benchi lao lilifanya mabadiliko hayo akaingia Erasto Nyoni.
“Madaktari waliona kama Onyango anaweza kuendelea kwa hiyo hatutaka kumtoa badala yake alitibiwa muda mfupi nje. Baada ya muda tukaambiwa hata yeye hataweza kuendelea na wakashauri atolewe, sasa pale ndipo kila kitu kiliharibika na kama mliona wote tulisikitika sio tu kumpoteza Onyango lakini tuliumizwa kwa kutumia vibaya kanuni hii mpya ya mabadiliko.
“Tulilazimika kumtoa Onyango na nafasi yake akaingia Kennedy (Juma) sasa kwa hesabu za mabadiliko ya kanuni ni mkupuo wa kwanza wa mabadiliko ya wachezaji ulitumika kwa kuingia Morrison, mkupuo wa pili ukawa kwa kuingia Nyoni na tatu kuingia kwa Kennedy.
“Ukiangalia hapo kanuni haikuwaruhusu makocha tena kumwingia Kagere wala kumtoa Mugalu na hapo hesabu zote ziliharibika lakini kubwa ni pale walipoumia kwa Onyango na Lwanga kuliharibu kila kitu,” aliongeza.
Mashabiki wengi wamekuwa wakimlaumu Kocha Didier Gomes kwa kutomwingiza Kagere akitakiwa kumtoa Mugalu ambaye alionekana kupoteza nafasi nyingi za kufunga ambazo Simba waliamini zingewavusha.