Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Feitoto afuata nyayo za hawa Azam FC

Feisal Azam VzO.jpeg Feitoto afuata nyayo za hawa Azam FC

Mon, 3 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Sakata la Yanga na aliyekuwa mchezaji wao, Feisal Salum lilifikia tamati wiki chache zilizopita kwa mabosi wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara na Wanafainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kukaa chini na nyota huyo sambamba na Azam FC ambao walihitaji huduma yake.

Jambo hilo lilimalizwa ikiwa ni siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan awatake viongozi wa Yanga kumalizana na mchezaji huyo ambaye alikuwa na mgogoro na timu hiyo kwenye hafla ya chakula cha pamoja Ikulu kufuatia kufanya kwao vizuri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambapo walikuwa washindi wa pili.

Kwa sasa Feisal ni mali ya Azam FC, alitia saini ya kuwatumikia mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara mkataba wa miaka mitatu hivyo amefuata nyayo za wachezaji wengine kibao ambao walitoka Jangwani na kutua Chamazi.

“Nina furaha kuwepo hapa (Azam), ninawaahidi kufanya makubwa mashabiki wote wa Azam FC, ” alisema Feisal kwenye utambulisho wake.

Feisal ambaye alizaliwa January 11, 1998 sio mchezaji wa kwanza kutoka Yanga na kwenda Azam FC hawa hapa ni baadhi ya nyota ambao waliwika wakiwa na jezi ya njano na kijani na baadae wakaenda kukabiliana na changamoto mpya kwa matajiri hao ambao kwenye dili hilo wamemwaga zaidi ya Sh. 100milioi.

FRANK DOMAYO

Wakati ambao Azam FC inamsajili Domayo walikuwa wametwaa Ligi Kuu Tanzania Bara, 2014 walimpa mkataba wa miaka miwili, alikuwa maarufu kama Chumvi ambayo ilivyo ni muhimu na inavyonogesha mboga, alikuwa na balaa akiwa uwanjani.

Domayo alisaini mkataba huo mjini Mbeya, baada ya kumaliza Mkataba wake wa miaka miwili na Yanga SC, ambayo alijiunga nayo akitokea JKT Ruvu.

Katibu wa Azam FC kwa wakati huo, Nassor Idrisa Mohamed ‘Father’ alisema katika kuendelea kukiimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu uliofuata wamepiga hatua nyingine kwa kumsaini kiungo huyo ambaye kwa sasa yupo zake Namungo.

“Kama unavyojua, baada ya kumaliza msimu vizuri tukiwa mabingwa wa Bara, tuligundua mapungufu kwenye kikosi chetu na kwa ushauri wa mwalimu wetu (Joseph Marius Omog) ndiyo tunayafanyia kazi,” alisema Father.

Domayo alikuwa mchezaji wa wa pili ndani ya siku mbili kusajiliwa na Azam FC kutoka mabingwa wa zamani na mabingwa wa kihistoria Tanzania Bara, Yanga SC baada ya mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbangu.

DIDIER KAVUMBAGU

Aprili 29,2014 Azam FC iliingia mkataba wa mwaka mmoja na aliyekuwa nahodha wa Burundi, Didier Kavumbangu wenye kipengele cha kuongezewa mwaka mwingine, iwapo atafanya vizuri katika mwaka wake wa kwanza.

Mshambuliaji huyo aliyemaliza mkataba wake wa miaka miwili na waliokuwa wapinzani wakuu wa Azam FC katika mbio za ubingwa msimu huo, Yanga SC, alisaini mkataba huo makao makuu ya klabu, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Aliyekuwa Katibu kwa wakati huo, Nassor alisema; “Tumepata mshambuliaji mzuri, ambaye tayari ana uzoefu wa kucheza Ligi Kuu ya Tanzania kwa misimu miwili, mchezaji huyu ni chaguo la kocha wetu Joseph Omog, ambaye alivutiwa naye baada ya kumuona akichezea klabu yake zamani, Yanga SC,”alisema.

Kwa upande wake, Kavumbangu alisema; “Mimi ni mchezaji, kazi yangu ni mpira. Nimemaliza mkataba Yanga, lakini viongozi hawaniambii kitu, nimepata ofa nzuri Azam nikaamua kusaini."

Kavumbangu alitua Yanga 2013 akitokea Atletico ya Burundi na katika mechi misimu miwili ya kuichezea klabu hiyo, amefunga mabao 31 katika mechi 63 za mashindano yote, moja tu la penalti.

OBREY CHIRWA

Novemba 2018, Azam FC ilimsajili nyota wa zamani wa Yanga, Obrey Chirwa.

Chirwa ambaye alikuwa mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita tangu atue Azam akiwa na mabao 13, alitua kwa matajiri hao wa Chamazi kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba nchini Misri alikokuwa anachezea timu ya Nogoom El Mostakbal.

Meneja wa Azam FC kwa wakati huo, Phillip Alando alisema kuwa klabu hiyo imemaliza na Chirwa huku akisubiri hatua zaidi za usajili baada ya dirisha kufunguliwa Novemba 15, 2018.

DONALD NGOMA

Mei 2018, Azam FC ilipata saini ya mshambuliaji toka Klabu ya Yanga, Donald Ngoma ikiwa ni maandalizi ya kujipanga kwa ajiri ya msimu uliokuwa ukifuata 2018/2019.

Kwa mjibu wa uongozi wa klabu ya Azam ulisema wapo tayari kumpeleka Donald Ngoma katika hospital ya Vicent Pallot ya Cape Town ya Afrika Kusini ili kujua ni kwa kiasi gani amepona majeraha aliyokuwa akiumwa kwa kipindi kirefu.

Kwao wanaamini kuwa ujio wa Ngona katika klabu hiyo utaisadia Azam kwa msimu ujuo lakini mambo yalikuwa tofauti na hakuwa kwenye ubora ule ambao walikuwa wakiutarajiwa kutokana na kusumbuliwa kwake na majeraha.

MRISHO NGASA

Juni 2010, Azam ilistua kwa kupata huduma ya aliyekuwa supastaa wa Yanga kwa wakati huo, Mrisho Ngassa aliyesaini kuwatumikia kwa msimu mitatu.

Katika mahojiano yake Ngassa ambaye hayupo kwenye soka la ushindani, alisema: "Nitaisaidia klabu yangu na kufanya vyote vinavyotakiwa ikiwa hata zaidi ya nilivyokuwa katika klabu yangu ya Yanga."

Hata hivyo Ngassa hakuwa na wakati mzuri akiwa na Azam FC, iliwabidi mabosi wa timu hiyo kumuondoa kwenye mipango yao kwani alionyesha kuwa bado na mapenzi mazito na Yanga ikiwa ni kipindi kifupi tangu kuondoka Jangwani.

Alipelekwa Simba kwa mkopo kabla ya kurejea zake Yanga.

Chanzo: Mwanaspoti