Achana na kina Khalid Aucho, Yannick Bangala na Fiston Mayele wanaoimbwa na mashabiki wa Yanga, kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ naye amewasapraizi Wanayanga kwa soka tamu na mabao ya kusisimua, akijitengenezea ufalme Jangwani tofauti na ilivyotarajiwa.
Fundi huyo wa mpira ambaye alitua Yanga kama kiungo mkabaji na sasa kutumika kama kiungo mshambuliaji ameuanza msimu kwa kishindo, kwani kama hafungi yeye, basi ujue atahusika na mabao ya Yanga na namba hazidanganyi buana!
Katika mechi tano ilizocheza Yanga katika Ligi Kuu Bara, Fei amefunga mabao matatu akiwa ndiye kinara wa timu hiyo na kuasisti moja akianza kufunga dhidi ya Kagera Sugar kisha alifunga bao la pili dhidi ya KMC akipiga shuti kali kama alivyofanya dhidi ya Ruvu Shooting juzi jijini Dar es Salaam.
Mabao matatu aliyonayo sasa Feisal ni pungufu na mawili aliyofunga katika msimu mzima uliopita katika mechi 34 za Yanga alipotupia kambani matano, hivyo kuonyesha wazi kama ataendelea na moto huo atafanya maajabu makubwa katika Ligi Kuu Bara.
Juu ya bao lake la juzi, Fei Toto alisema siku zote anapokuwa nje ya boksi huwa anaweka akili na macho yake katika lango la mpinzani na mpira unapofika huwa na kazi moja tu kuhakikisha anapata mpira na kuupiga ili kuifungia timu yake bao.
“Niliangalia kabla ya kuupiga mpira, nikamuona kipa amekaa vibaya, hivyo nilipohakikisha mpira umenifikia nikapiga shuti langoni, ndio maana nikafunga,” alisema Fei Toto.
Alisema anachofurahia ni kuona bao lake liliisaidia kuirejesha timu mchezoni na kuongeza mengine yaliyoendeleza rekodi yao ya kushinda mechi mfululizo hadi sasa katika ligi hiyo.
Bao hilo dhidi ya Ruvu limemfanya kiungo huyo kumpumulia Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania anayeongoza orodha ya wafungaji (kabla ya mechi za jana) akiwa na manne, akitofautiana naye moja.
WASIKIE HAWA
Anachokifanya Fei Toto kimewashtua nyota wa zamani wa kimataifa nchini, akiwamo Edibily Lunyamila aliyesema akiendelea kujituma atafika mbali zaidi kwani jamaa ni fundi mwenye kipaji.
“Ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, unafurahia kumuona anacheza uwanjani, anaburudisha macho ya mashabiki, akiwepo uwanjani anakupa imani lazima atafanya jambo,” alisema Lunyamila, huku kiungo wa zamani wa timu hiyo, Athuman Idd ‘Chuji’ amesema anajiona Yanga kupitia miguu ya Fei Toto.
“Yanga wamepambana sana kusaka kiungo mshambuliaji wa aina hiyo tangu nimeondoka lakini namuona Fei Toto akifanya niliyokuwa nikiyafanya nafurahia kumuangalia,” amesema.
Aliyekuwa kocha wa Simba, Didier Gomes aliwahi kusema Fei Toto anastahili kwenda nje kupata changamoto mpya, baada ya kipaji chake kuonyesha kwa ukubwa nchini.
“Amesema kama makocha wa nje watamuona Fei Toto akicheza, wanamchukua kwa uharaka kwani ana uwezo mkubwa mguuni kwao,” alisema.
MASHABIKI WAPAGAWA
Shabiki kindakindaki wa timu ya Yanga, Anwari Wambura ‘Yanga Kigelegele’ alisema anayoyafanya Fei Toto yanawapa amani na analitambulisha soka la Tanzania kwa nchini zinazotazama Ligi Kuu Bara.
“Fei Toto ni mmoja tu, hao wengine wanaiga, nani anaweza akafanya mambo yake anayoyafanya kwa sasa, nchi jirani zikimtazama zinajua kweli Tanzania kuna vipaji vikubwa,” amesema Fei Toto.
Shabiki mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Frank Yanga alisema Fei Toto anafanya mambo ya kikubwa yasiyoendana na umri wake na kwamba anastahili kujitwalia ufalme mbele yao.
“Kijana mdogo anaitetemesha nchini, nadhani hata wapinzani tunaocheza nao, wakitulia na kukaa chini wanaanza kushangilia kazi zake, Yanga raha jamani,” amesema.