Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei Toto kaiacha miguu ijibu kwa vitendo

Fei Toto Vs Coast Fei Toto kaiacha miguu ijibu kwa vitendo

Thu, 7 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Safari ya kuja Tanzania Bara ilianza baada ya kung’ara na JKU ya Zanzibar aliyobeba nayo taji la Ligi Kuu ya visiwani humo kwa misimu miwili mfululizo 2016-2017 na 2017-2018.

Pia kung’ara kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2018 akiwa na jezi namba 3 enzi hizo, ndio iliyoivutia Singida United na kufikia hatua ya kuzungumza naye, kisha kumpa mkataba wa miaka mitatu asubuhi na kumvusha Bahari ya Hindi kuja Bara.

Hata hivyo, saa chache baadaye siku hiyo hiyo, mida ya jioni akaibukia Jangwani. Yanga ilipindua meza, baada ya kumalizana na mabosi wa JKU waliokuwa na mkataba naye na kumpa dili la miaka minne kabla ya kuuongeza tena.

Hapa tunamzungumzia Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’, mmoja ya nyota bora wa soka wa Kitanzania ambaye mwishoni mwa msimu uliopita aligeuka gumzo akitawala vyombo vya habari hasa vya michezo.

Yaani ni kama ilivyokuwa wakati wa usajili wake alipotua Jangwani 2018, ndivyo alivyoondoka kwa kutawala midomoni mwa mashabiki wa soka na vyombo vya habari.

Ndio, kiungo mshambuliaji huyo aliyejaliwa kipaji cha soka cha kucheza kokote duniani alianzisha mgomo wa kuikacha Yanga ikielezwa alishamalizana mapema na Azam FC.

Aliuangalia mkataba alioingia na Yanga na kuona kuna kipengele kinachompa nafasi ya kuuvunja kiulaini na kusepa. Akaiingizia Yanga Sh112 milioni kwenye akaunti yao. Hizo zikiwa ni Sh100 Milioni za kuvunja mkataba huo uliokuwa umesaliwa na kama mwaka na ushei hivi kati ya mitano aliyoingia Agosti, 2018 na kuongezwa baadaye.

Kisha akaongeza Sh12 milioni ikiwa kama ni sehemu ya mshahara wa miezi mitatu aliotakiwa kuilipa klabu ili awe huru. Yanga wakamgomea.

Kumbuka ilikuwa ni Desemba ya mwaka jana. Sakata likashika hatamu na watu kuburuzana TFF na zikawepo taarifa za kutaka kufikishana Fifa, lakini ghafla ikafanyika pati Ikulu ya Dar es Salaam.

Ilikuwa ni hafla ya kuipongeza Yanga kwa kitendo cha kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Mzizi wa fitina ukavunjwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake fupi kuutaka uongozi wa Yanga kuliangalia upya sakata la Fei, na kama inawezekana ‘mtoto’ aachwe aende apatakapo.

Yanga haikuwa na namna, zaidi ya kuuma jongoo kwa meno na kumuachia. Azam iliyotajwa kuinjinia kila kitu ikiwamo kutoa yale mamilioni yaliyorudishwa, ikawa imemnasa kiulaini. Ikamsajili rasmi kwa dau ambalo limefanywa siri, japo inaelezwa ni zaidi ya Sh250 milioni na kuanza kuitumikia timu hiyo aliyonayo hadi leo na huko anakiwasha.

ZOMEA YA HASIRA

Tangu Fei Toto alipochomoka Yanga, kuliibuka chuki flani kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo. Walisahau mema yote aliyoifanyia timu hiyo, ikiwamo juhudi zake zilizoisaidia timu hiyo kurejesha taji la Ligi Kuu baada ya kulisotea kwa misimu minne mfululizo mbele ya Simba.

Walisahau kama ni yeye aliyeiua Simba kwenye nusu fainali ya ASFC pale CCM Kirumba, Mwanza na kuipeleka timu fainali jijini Arusha na huko, Yanga ilishinda kwa penalti baada ya sare ya 3-3 ndani ya dakika 120 na kulibeba taji hilo ililotetea msimu uliopita.

Pia walisahau kabisa kuwa, Yanga ilifika makundi ya Shirikisho Afrika msimu uliopita na kuanzisha safari ya fainali kwa umahiri wake uwanjani akishirikiana na Fiston Mayele na wengineo.

Ikawa sasa kila anapoonekana uwanjani, mashabiki wa Yanga wanamzomea. Walianzia kwenye Ngao ya Jamii jijini Tanga, Azam ilipolala kwa mabao 2-0. Akazomewa pia hata alipoisaidia Azam kumaliza nafasi ya tatu kwa kuifunga Singida Fountain Gate.

Akaendelea kuzomewa hata kwenye mechi za kimataifa za Kombe la Shirikisho, Azam ikitolewa na Wahabeshi. Akazomewa hata alipopiga hat trick mbele ya Tabora United katika mechi ya Ligi Kuu na kuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat trick kwa msimu huu. Wengi walidai aliitungua timu dhaifu iliyokuwa  pungufu uwanjani.

Kosa halikuwa la Fei Toto kupata mchekea wa kufunga mabao hayo, ila ni kanuni ya soka inayoruhusu mechi kupigwa iwapo timu itakuwa na wachezaji kuanzia saba.

Tabora ikitumia jina la Kitayosce walikuwa wanane uwanjani, kabla ya Ismail Aden Rage kwenda kuwapa ‘akili’ ya kujivunja kwa wachezaji wao wawili na mechi kuvunjika, ikiwa tayari imeshanyukwa mabao 4-0. Fei Toto akipiga hat trick na jingine likifungwa na Prince Dube.

Wakamzomea zaidi wakati Yanga ikishinda 3-2 mbele ya Azam katika mechi ya Ligi Kuu  na utani ulizidi baada ya kusambazwa kwa picha ya Fei akiwa kashika kichwa mbele ya msitu wa nyota wa Yanga, lakini fundi huyo anayemudu kucheza pia kama kiungo mkabaji, aliamua kuiacha miguu ijibu mapigo.

NAMBA ZINAMBEBA

Pamoja na zomeazomea hiyo, Fei Toto aliendelea kuwafunga mdomo mashabiki waliokuwa na chuki za hasira za kuihama Yanga ‘kikatili’ kwa kufunga mabao mengine, huku akisisti na kuifanya Azam iwe tishio.

Hadi unaposoma makala haya, Fei amehusika na mabao 10 kati ya 24 yaliyofungwa na Azam katika mechi 10 iliyocheza. Amefunga mabao sita na kuasisti mara nne, akiwa ndiye mchezaji mzawa mwenye mabao mengi katika Ligi Kuu kwa sasa.

HAIMBWI KIVILE

Tofauti na alipokuwa Yanga, Fei kwa sasa haimbwi sana, licha ya kufanya makubwa katika Ligi Kuu, akiwa nyota mzawa mwenye mabao mengi (6) na akiupiga mwingi uwanjani kwa kila mchezo.

Sio ajabu kwa vile ni kawaida kwa mashabiki na hata vyombo vya habari kuwakaushia nyota walio nje ya Simba na Yanga na ule utamaduni kupenda kushobokea nyota wa kigeni hata wasiokuwa na maajabu.

 Utabisha nini, wakati hata John Bocco alibezwa na kusakamwa alipokuwa, Azam tofauti na alipohamia Simba alipopambwa. Bocco alichukiwa kwa sababu ya kuzitungua Simba na Yanga na alikaushiwa, licha ya rekodi tamu aliyowekwa ya kuwa nyota mzawa kufunga mabao mfululizo ndani ya misimu 16 katika ligi hiyo.

Alipotua Simba tu msimu wa 2017-2018 mambo yalibadilika, kila alichokifanya kilionekana ni dhahabu, ilihali kwa misimu tisa aliyokuwa Azam alikuwa balaa zaidi.

Huenda Fei angeendelea kuichezea Yanga na hiki alichokifanya sasa, hakika jina lake lingetawala kila kona, hata hivyo kwa kuwa yupo Azam, ule msemo wa Nabii hakubaliki kwao unaendelezwa, ila mwenyewe hana habari, zaidi ya kuicha miguu yake ifanye kazi uwanjani.

Iwapo ataendelea na kasi hii aliyonayo ni wazi, huenda huu ukawa msimu mtamu kwa ‘Zanzibar Finest’ huyo anayejua cha kufanya kila anapokuwa na mpira, kwani hajawahi kupoa tangu aanze kufahamika. Ngoja tuone!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live