Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei Toto, injinia Hersi wote wamechemka

Hersi X Fei Fei Toto, injinia Hersi wote wamechemka

Wed, 28 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hakuna shaka sakata la Feisal Salum, maarufu kwa jina la Fei Toto ndilo gumzo la mjini kwa sasa baada ya nyota huyo kutoka Zanzibar kuandika barua ya kuvunja mkataba na klabu yake ya Yanga na kulipa Sh112 milioni kwa ajili ya kununua mkataba wake.

Kwa wengi zimekuwa ni habari mpya, lakini kwa wale wanaofuatilia ‘Za Ndaaani’ watakuwa wameunganisha nukta hadi kufikia hatua ya kuondoka kwa kiungo huyo nyota aliyeibukia kuwa mwokozi wa Yanga katika nyakati ngumu.

Mjadala umekuwa mkubwa kati ya watu wanaounga mkono kitendo chake cha kujiondoa Yanga, hasa anapojenga hoja kuwa “Nacheza ili kujipatia kipato na si kufurahisha watu.”

Hoja yao inaongezewa nguvu na taarifa kwamba Fei Toto alikuwa analipwa Sh4 milioni , wakati nyota wengine, hasa wale kutoka nje, wanalipwa kuanzia Sh10 milioni, baadhi yao wakiwa hawana mchango mkubwa kwenye timu kulinganisha na wake.

Bila shaka hiyo ni hoja kubwa na yenye nguvu ambayo inahitaji maarifa ya hali ya juu kuipangua. Taarifa kwamba kwenye mkataba wake kuna kipengele hicho cha kuvunja mkataba kwa kulipa mshahara wa miezi mitatu na kurejesha fedha ya usajili ya Sh100 milioni, ndiyo kinaongeza nguvu zaidi katika sakata lake.

Kwamba anachotafuta ni fedha na si kitu kingine chochote.

Fei Toto alishajijengea heshima ya kuwa mchezaji wa aina yake Yanga, akiwa na uwezo wa kuchezesha timu, kuzuia, kushambulia na kufunga, hasa nyakati ambazo Yanga inahitaji bao kwa kila hali na uwezekano wa kushinda unaonekana mdogo.

Ni mara chache alifunga mabao ya ‘nyongeza’ kama ilivyo kwa wachezaji wengine ambao hawafungi hadi timu ifunge mabao kuanzia mawili au hawafungi kwenye mechi yenye ushindani mkali.

Wengine wanaona kuwa Fei Toto alikosea kuondoka kwa njia hiyo. Hawa wanajenga hoja kwamba mkataba wake na kwa mujibu wa kanuni za Fifa, hauruhusu kuuvunjwa kwa namna hiyo. Kwamba kipengele kinachoruhusu kuvunjwa mkataba ni kile kinachotaka yawepo mazingira ambayo imefikia wakati hayatatuliki.

Baadhi yao pia wanasema si busara kwa mchezaji tegemeo na mwenye matarajio makubwa kuhama kipindi cha dirisha dogo, ambalo kwa kawaida hutumika kuziba mapengo ya wachezaji majeruhi na hivyo umuhimu wake kuisha wakati msimu unapoisha wakati makocha wanapoanza kupanga mipango ya baadaye.

Kwa mfano, wakati Mbwana Samatta amepata nafasi ya kucheza Aston Villa, wengi waliona ilikuwa nafasi ya pekee maishani na hivyo hakukuwa na sababu ya kuikwepa. Lakini ilikuwa ni wakati wa dirisha dogo na mahitaji ya mshambuliaji yalitokana na mchezaji tegemeo wa Villa kuwa majeruhi.

Hivyo, Samatta aliingia kwa mipango ya muda mfupi na kuendelea kuchezea Villa kungetegemea na kiwango chake kulinganisha na huyo majeruhi na pia mipango ya sokoni ya klabu hiyo wakati wa majira ya joto. Na ndivyo ilivyokuwa. Kocha hakuwa tena na mipango na Samatta wakati wa usajili mkubwa na akalazimishwa kuhama kwa mkopo.

Mazingira hayo yanaweza yasiwepo Azam ambako ndiko ambako Fei Toto anahusishwa nako, lakini mambo ya mpira yanabadilika kila siku.

Na baadhi wanaona kuwa masuala ya mishahara kwenye klabu hayaongezeki kwa sababu tu kuna wachezaji wapya wanalipwa vizuri au mchezaji ameonyesha umuhimu wake, bali taratibu za kawaida za malipo.

Kwa kawaida kwenye ajira, mshahara ni makubaliano binafsi bila ya kuangalia mwingine anapata nini. Lakini kadri utendaji unavyoanza kuwa bora na taasisi inanufaika na kiwango chako ni lazima mkae chini kujadili jinsi ya kuboresha malipo. Na mara nyingi, vikao hivi hufanyika kabla ya mkataba wa awali kuisha, kiasi kwamba mchezaji anakuwa na uhakika mambo yake yatabadilika kwenye mkataba mpya.

Bila shaka katika mazungumzo hayo kutakuwa na makubaliano ya nini kifanyike wakati wa kusubiri mkataba mpya kwa kuwa gharama za maisha hazisubiri kipato kiwe kizuri, zinakua kila siku.

Mfano mzuri ni kwa Bukayo Saka, winga wa Arsenal ambaye amekuwa na mchango mkubwa kwa klabu hiyo ya London tangu apandishwe kutoka timu ya vijana. Hadi mkataba wake wa sasa utakapokuwa unaisha mwaka 2024, Saka analipwa Pauni 30,000 kwa wiki. Lakini kutokana na klabu kama Liverpool na Manchester City kummezea mate, Arsenal ilianza mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji huyo ili kuboresha maslahi yake.

Imeripoti kuwa mazungumzo baina ya pande hizo ni kama yameshakamilika na huenda Saka akasaini mkataba mpya ambao utamhakikishia Pauni 200,000 za Kiingereza kwa wiki, akiwa mmoja wa wachezaji wanalolipwa vizuri Arsenal. Wengine ni Gabriel Jesus, ambaye ndiyo kwanza amejiunga Arsenal Julai mwaka jana, na Thomas Partey, ambaye huu ni msimu wake wa pili.

Pamoja na hoja za pande hizo mbili, binafsi naona Fei Toto na uongozi wa Yanga wana makosa ambayo yangeweza kuzuia sakata hilo kama yasingekuwepo.

Kwa kutambua sasa amekuwa kipenzi cha mashabiki na wanachama na anaelekea kuvishwa hadhi ya ulegendari, Fei Toto alitakiwa atumie njia za majadiliano na waajiri wake kabla ya kuwastukiza na malipo na barua ya kuwaaga.

Huu ni uungwana unaojenga mazingira mazuri ya baadaye kwa mchezaji ambaye siku zote hatakiwi kuingia kwenye mzozo na waajiri kwa kuwa maisha ni mzunguko kwa waajiri haohao. Tena katika mashirika makubwa (corporate organisations), ni ngumu mfanyakazi aliyeondoka kwa vituko kupata ajira shirika jingine.

Haisemwi, lakini pamoja na mshahara mkubwa, kikwazo kingine kwa Ronaldo kupata timu kubwa ni jinsi alivyoondoka Manchester United. Si rahisi kwa klabu nyingine kumkubali wakati ikiwa imeshaona kilichotokea kwa wenzao.

Suala la kina Stephane Aziz Ki au Fiston Mayele kulipwa mshahara mkubwa kuliko yeye halikuwa hoja kwa Fei Toto. Hoja yake ingekuwa maslahi yake tu. Yaani aitaarifu klabu kuwa ana mpango wa kuondoka kutafuta maisha mazuri zaidi na aone nini kingefanyika kuboresha maslahi yake kuliko kuaga na isitoshe mtandaoni.

Umuhimu wako ndio unaamua maslahi yako na si mshahara wa mwingine. Pengine katika kuboresha mkataba, Fei angeweza kulipwa zaidi ya kina Aziz Ki kulinganisha na jinsi ambavyo upande wake ungejenga hoja.

Kwa hiyo, kucheza mpira kwa ajili ya maslahi ni kwa jinsi hiyo, kwamba ujadiliane na mwajiri wa sasa na ikishindikana basi kukubaliana kutofautiana. Ndivyo ulimwenguiwa leo ulivyo.

Hata hivyo, uongozi wa Hersi Said ulitakiwa uyaone haya mapema. Kiwango cha Fei Toto uwanjani na umuhimu wake ulishaonyesha kuwa thamani yake inaongezeka na klabu zimeshaanza kummezea mate.

Ilikuwa ni muhimu kwa uongozi kuanza mazungumzo mapema na wawakilishi wa Fei Toto, hasa baada ya habari “za ndaani” kuvuja kuwa kuna mchezaji ameshapewa hundi aandike anataka nini.

Hili ni kosa la pili baada ya lile la mwanzo la Bernard Morrison lililosababisha Yanga itumie nguvu kubwa kumrejesha.

Tatizo jingine pia kwa uongozi ni mamlaka ya kushughhulikia maslahi ya wachezaji. Hersi ndiye aliyefanya usajili huu wote kabla ya kuwa rais wa Yanga. Alimfuata mchezaji mmoja mmoja kila alikokuwa, lakini hawa wa ndani hawakufuatwa.

Leo ni nani ana nguvu hiyo ya kujadiliana na mchezaji kuhusu maslahi yake. Bado ni Hersi akiwa rais wa klabu, au kuna mwingine anayeweza kusimama na nguvu alizokuwa nazo Hersi kabla ya kuwa rais?

Na kama ni Hersi, ana muda huo wa kushughulikia yote hayo?

Bado kuna haja ya kuweka muundo sawa badala ya huu ambao unaonyesha nguvu haiku kwenye mfumo, bali kwa mtu.

Haya ya Fei Toto yangeweza kuonwa mapema au yalionwa na wengine lakini hawakuwa na mamlaka ya kuyazuia.

Chanzo: Mwanaspoti