Kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amefunguka timu yake haimtegemei mchezaji mmoja kwani imekamilika kila idara na kila anayepewa nafasi anaonyesha kiwango kikubwa.
Fei yupo nje akiendelea kutibiwa majeraha yake ya goti hivyo amekosa mechi mbili ile ya Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, Yanga ikishinda bao 2-1 pamoja na ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Geita ambayo timu yake ilifuzu nusu fainali kwa penalti 7-6 baada ya dakika 90 kutoka sare ya bao 1-1.
“Bado sijaanza mazoezi na sijajua nitaanza lini kwa sababu niliambiwa nahitajika kupumzika kwa muda kidogo kitu ambacho kwangu ni kigumu kutokana na kuzoea kufanya kazi yangu ambayo ndio inanipa kula na kuishi vizuri,” alisema na kuongeza;
“Sifurahii kukaa nje ya uwanja, ninaumia na natamani kucheza mara kwa mara ili kuendelea kuboresha kipaji changu, lakini kuna wakati inakulazimu ufuate kile unachoshauriwa ili maisha mengine yaendelea,” alisema Fei.
Alisema kutokuwepo kwake ndani ya Yanga kipindi hiki cha mechi za lala salama haoni timu ya kuwazuia kufikia malengo ya kutwaa ubingwa huo huku akimtaja kipa Djigui Diarra kuwa hata akikosekana bado timu yao ipo salama.
“Nakosekana timu inapata matokeo mazuri, kwanza mimi nani, Diarra ambaye ndiye kiungo imara ndani ya timu kwa kuokoa mashuti mengi lakini anaweza asiwepo na bado Yanga inakuwa imara na inaweza kumaliza dakika 90 bila kuruhusu bao. Uongozi ulizingatia mengi kuhakikisha msimu huu hatupotezi kitu na inawezekana,” alisema na kuongeza;
“Sijacheza mechi ngumu dhidi ya Azam FC timu imepata matokeo ni timu gani nyingine itatuzuia kutwaa taji.”