Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei Toto anaweza kuwa mkombozi wa wazawa

Feisal Feisal Salum

Wed, 28 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Nianze kwa kuwatakia heri ya Mwaka Mpya (New Year 2023) wafuatiliaji wa safu hii ambapo kwa sasa inazidi kushika kasi.

Nimekuwa nikipokea simu nyingi, ujumbe wa kawaida kupitia simu ya mkononi na wengine wamekuwa wakiwasiliana nami kupitia WhatsApp.

Nisema kuwa kila aliyekuwa anawasiliana nami alikuwa anatoa maoni yake huku wengine wakiuliza maswali mbalimbali kuhusiana na masuala ya soka na wengine walitafuta fursa, nini wafanye ili kufikia malengo yao katika soka.

Hapa nazungumzia wachezaji chipukizi au yosso kutoka sehemu mbalimbali ambao wanatafuta nafasi ya kuonesha vipaji vyao ili watimize malengo yao.

Katika kila jambo lina changamoto zake, hapa namaanisha kuwa mbali ya kupokea maoni chanya, lakini kuna wengine walikuwa wanatoa maoni hasi, shutuma mbalimbali na kuna wale walioleta utani mwingi sana.

Nimekuwa nikiyachukulia haya kama sehemu ya mafanikio kwani wote ni wasomaji na ni wazi kuwa wameanza kuwasiliana nami kutokana na kuwa wasomaji wa safu hii.

Kama ilivyokuwa katika matoleo mbalimbali ya safu hii, nitatumia safu au kolamu hii ambayo ni ya mwisho kwa mwaka huu kujadili masuala mbalimbali ya usajili unaoendelea hasa kipindi hiki cha dirisha dogo.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefungua dirisha dogo ambalo linamalizika Januari 15, mwakani.

Ni kipindi ambacho kila timu inafanya usajili kwa ajili ya kuhimarisha timu zake kwa ajili ya ligi ya NBC ambayo kwa sasa imeingia mzunguko wa pili, au lala salama.

Ni kipindi cha ‘kuchanga’ karata zako vizuri ili kujiweka sawa kwa ajili ya kumaliza salama katika ligi inayoendelea na kinyume chake, timu itashuka daraja.

Mpaka sasa, ligi imegawanyika katika makundi matatu, yaani kundi la timu ambazo zinawania ubingwa, ambazo ni Yanga, Simba na Azam FC, lakini kuna kundi ambalo linawania nafasi ya kumaliza katika nne bora ili kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya CAF na pia kuna kundi la timu ambalo linapambana na ‘hali’ zao ili kuepuka kushuka daraja.

Kwa wachezaji ni kipindi cha kuonyesha uwezo wao ili kuweza kubaki katika usajili wa mwakani na kuna wengine lazima waonyeshe uwezo wao ili kupata nafasi katika kipindi hiki kidogo cha usajili.

Mpaka sasa, Simba imekamilisha usajili wa mchezaji, raia wa Burundi, Saido Ntibazonkiza kutoka Geita Gold FC. Ntibazonkiza aliwahi kuichezea Yanga, ni mmoja wa wachezaji wenye historia kubwa katika soka kwani amecheza ligi mbalimbali na sehemu zote alizocheza, yaani Yanga na Geita Gold FC ameonyesha uwezo mkubwa.

Simba pia inahusishwa na usajili wa mchezaji mwingine kutoka timu ya Geita Gold FC, Kelvin Nashoni ambaye bado hajatangazwa na pia imefanikiwa kumbakiza beki wake wa kati, Henock Inonga Baka.

USAJILI WA FEI TOTO

Ukiachana na ushindi wa mabao 3-2 wa Yanga dhidi ya Azam FC juzi usiku (Desemba 25) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, gumzo kubwa kwa sasa ni usajili wa mchezaji Feisal ‘Fei Toto’ Salum ambaye anahusishwa na kujiunga na Azam FC.

Feisal ameandika barua ya kuvunja mkataba wake na klabu ya Yanga kwa mujibu wa sheria huku akirudisha fedha za ada ya usajili (Signing fees) na mshahara wa miezi mitatu. Kwa sasa jambo ambalo limezua utata mkubwa na klabu yake.

Ni wazi kuwa kuna baadhi ya taratibu zimekiukwa, jambo ambalo tunawaachia wanasheria na pia kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji kufanya kazi zake.

Pointi yangu kubwa kwa hapa ni jinsi yale yanayosemwa yaliyo msukuma Fei Toto mpaka kufikia hapa. Madai makubwa ya Fei ni maslahi yake katika kazi yake. Ni wazi kuwa kuna wachezaji wengi hawana uwezo mdogo na hawana nafasi ya kucheza katika timu lakini wanalipwa vizuri zaidi kulinganisha na wale wanaocheza huku kuchangia mafanikio katika timu.

Inawezekana kabisa Fei amekosea, lakini suluhisho la suala lake, ikiwa pamoja na kurekebisha maslahi yake kwa Yanga au huku ambako anatakiwa kwenda, itakiwa mapinduzi makubwa katika soka la Tanzania na hasa wachezaji wazawa kwa upande wa maslahi.

Fei anaweza kuwa mkombozi kwa wachezaji wazawa, hilo halina shaka, ila tatizo ni njia ya kupita npaka kufanikiwa.

Timu zetu za Tanzania zimekuwa haziwapi kipaumbele kwenye maslahi wachezaji wa ndani na kuwathamani sana wale wa nje.

Chanzo: Mwanaspoti