Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei Toto anavyomshangaa Kibu Denis

Kibu  Simba Kauli Kibu Denis

Sun, 28 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuna watu wana matukio ya kutisha. Fikiria kuna vijana wa miaka 25 tu, walishafumaniwa. Wameshatoa mimba kadhaa. Wameshakataa mimba kadhaa. Wameshakaa jela. Wamemaliza kila kitu.

Ni vitu vya kutisha. Ni kama unavyosikia siku hizi watu wanaiba watoto wa kiume kisha wanawakata sehemu zao nyeti za mwili. Wanawezaje? Inafikirisha sana.

Dunia imekuwa sehemu ya kutisha. Wanadamu wamekuwa na matendo katili hadi shetani mwenyewe anashangaa. Wanawezaje kufanya haya? Sijui.

Kwa kawaida mwanadamu anapaswa kuwa na ujasiri ili kuishinda dunia. Ila ujasiri ukizidi ni hatari. Ujasiri unaopaswa ni kama ule wa Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuwapa Yanga barua ya kuvunja mkataba. Kisha akawapa fedha walizoandika katika mkataba. Lilikuwa ni jambo la kushtua sana.

Yanga ilikuwa ya moto. Yanga ina jeuri ya fedha za GSM. Mchezaji wa Kitanzania angewezaje kuwapa barua ya kuvunja mkataba katikati ya msimu? Ni ngumu sana. Ila kwa ujasiri Fei Toto alifanya hivyo. Watu walidhani anatikisa kiberiti, lakini alisimamia msimamo wake. Akakaa nje ya uwanja kwa nusu msimu. Baadaye akaenda alipopataka.

Hivyo ndivyo mwanaume anapaswa kuwa. Lazima asimamie kile alichokiamini. Ila katika yote hayo lazima ufuate utaratibu.

Fei Toto alifuata utaratibu wa kuvunja mkataba, japo haukuwa muda sahihi. Kisheria alipaswa pia kulipa fidia kiasi kwa kuondoka katikati ya msimu. Sakata la Fei Toto limekuwa kama mfano kwa mambo yanayotokea baada ya hapo.

Lilipotokea sakata la Prince Dube kuondoka Azam katikati ya msimu watu walitaka uamuzi wake uheshimiwe. Azam FC waliheshimu hilo. Wakamwambia Dube afuate taratibu za kuvunja mkataba wake.

Dube alipaswa kulipa fedha za kununua mkataba wake ili awe huru. Akataka kufanya tofauti. Alitaka awape Azam FC kiwango kidogo cha fedha tofauti na mkataba unavyosema. Ikawa ngumu. Ila mwisho wa yote akafuata utaratibu na mambo yakaenda vizuri.

Kwa Dube alikuwa na ujasiri ila hakutaka kufuata utaratibu mwanzoni. Ila baadaye akagundua kila jambo lina utaratibu wake. Akafanya kama Fei Toto na mambo yakawa mazuri.

Sasa kuna hili la Kibu Denis. Linachekesha kidogo. Kibu alisaini mkataba mpya na Simba, Juni, mwaka huu. Mkataba wake ulikuwa na hekaheka nyingi. Alitaka fedha nyingi. Watu wakapiga kelele kuwa anastahili fedha hizo hivyo apewe. Simba wakampa, akasaini.

Alipovuta mkwanja wake akaenda mapumzikoni Marekani. Akala bata la kutosha. Inapendeza sana. Baada ya bata sasa akatakiwa kuripoti kazini. Simba ilikuwa tayari imekwenda kambini Misri. Akapaswa kuungana na wenzake, lakini hakwenda.

Kila Simba walipomtafuta akadai anauguliwa na mzazi wake, hivyo hawezi kumuacha peke yake. Mwishoni hakwenda kabisa kambini. Baadaye Simba wakapata taarifa kuwa anakwenda kufanya majaribio kwenye moja ya timu za Ligi Kuu Norway. Inashangaza.

Mchezaji ana mkataba wenye mwezi mmoja tu anawezaje kwenda kwenye najaribio bila kuwapa taarifa waajiri wake? Huu ni utoro kazini. Japo taarifa zingine zinasema mabosi wa Simba walikuwa wanajua. Ila tuamini kwamba mabosi wa Simba hawakuwa wanajua.

Kama Kibu alikuwa na mipango mingine alipaswa kusubiri kwanza kuongeza mkataba Simba. Angeendelea na mipango yake kwanza. Akafanya majaribio na kuona kama atafaulu. Vinginevyo hivi anavyofanya sasa ni utovu wa nidhamu.

Mfano kama majaribio yake yakifeli itabidi arudi kazini kwake. Atawaambia nini Simba? Alikuwa wapi? Kwanini hakuripoti kazini?

Kuna watu wanafananisha sakata la Kibu na lile la Fei Toto. Ni mambo mawili tofauti kabisa. Fei aliandika kuvunja mkataba wake. Kibu ametoroka kazini kwenda kwenye majaribio.

Utaratibu wa majaribio uko wazi. Kibu alipaswa kuwataarifu Simba na kuomba ruhusa, kisha akaenda kujaribu bahati yake. Akifaulu majaribio watajua cha kufanya ili aende kwingineko. Ila sasa amefanya kinyume. Ndio maana nasema hata Fei Toto anamshangaa Kibu. Anashangaa sakata lake kufananishwa na hili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live