Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei Toto amejipata Azam FC

Fei Toto 9 Goals Kiungo wa Aam FC, Feisal Salum "Fei Toto"

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Unapozungumzia usajili uliotingisha nchi msimu huu, hutoacha kutaja jina la nyota wa kikosi cha Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Nyota huyo alijiunga na Azam FC Juni 8, 2023 akitokea Yanga, ukiwa ni usajili ulioteka hisia za mashabiki wengi kwani hawakutegemea kama angeachana na klabu hiyo aliyochukua nayo ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo.

Sababu kubwa ya usajili huo kutikisa ni kutokana na mgogoro wa kimkataba uliokuwepo wa muda mrefu kwani Feisal alidai mkataba wake ulikuwa umekwisha na yupo huru huku viongozi wa Yanga wakidai bado ni mchezaji wao hadi mwaka huu wa 2024.

Feisal aliamua kuvunja mkataba kwa kuweka pesa Sh112 milioni kwenye akaunti ya klabu hiyo, ila baadaye Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilieleza inamtambua kama mchezaji wa Yanga.

Baada ya sekeseke hilo ndipo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akatoa agizo kwa viongozi wa Yanga kumaliza mgogoro huo wakati wa hafla ya chakula cha jioni ya kuipongeza timu hiyo kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Samia alitoa agizo hilo Juni 5, mwaka jana baada ya Yanga kufika fainali na kupoteza mbele ya USM Algers ya Algeria kwa faida ya bao la ugenini baada ya mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam kupoteza mabao 2-1, kisha marudiano kushinda 1-0.

“Haipendezi klabu kubwa kama hii kuwa na ugomvi na mtoto mdogo, hebu kamalizeni kisha mje nyumbani kunieleza,” alisema Samia.

Kauli ya Rais, ndiyo ilihitimisha sakata hilo na nyota huyo kutua Azam akiondoka Yanga aliyojiunga nayo Agosti 15, 2018 akitokea Singida United alikodumu kwa siku chache akitokea JKU ya Zanzibar.

Sababu kubwa ya sakata hilo kuchukua muda mrefu ni kutokana na ubora wake kwa sababu Yanga ilikuwa ikimuhitaji sawa na Azam ambayo kiu yao kubwa ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwani mara ya mwisho ilikuwa msimu wa 2013-14.

Kuonyesha ubora wake msimu huu, tayari amehusika katika mabao 14 kati ya 39 yaliyofungwa na kikosi hicho kizima kwenye Ligi Kuu Bara ambapo amefunga tisa na kutoa ‘asisti’ tano huku akipitwa bao moja tu na Stephane Aziz KI wa Yanga mwenye mabao 10.

Kwenye kikosi cha Azam, Feisal ndiye anayeongoza katika ufungaji wa mabao akifuatiwa na Prince Dube anayeandamwa na majeraha ya mara kwa mara aliyefunga saba hadi sasa huku Idd Seleman ‘Nado’ na Kipre Junior wakifunga manne kila mmoja.

Msimu huu umekuwa bora zaidi kwa Feisal tofauti na alivyokuwa Yanga kwa misimu miwili iliyopita kwani hajawahi kuzidi mabao sita.

Msimu wa 2021-2022 akiwa Yanga alicheza dakika 2044 katika michezo 26 kati ya 30 ya Ligi Kuu Bara ambapo alifunga mabao sita na kuchangia manne (asisti) huku msimu uliopita wa 2022-2023 akifunga pia sita tofauti na sasa alipofunga tisa.

HAT-TRICK 1

Katika mabao tisa aliyofunga nyota huyo tayari ana ‘hat-trick’ moja aliyoifunga katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 4-0, dhidi ya Tabora United, mechi iliyopigwa Agosti 16, mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.

Licha ya ‘hat-trick’ hiyo, mchezo huo utabaki katika kumbukumbu ya wanamichezo nchini kwani uliisha ndani ya dakika 18 tu baada ya Tabora United kuanza na wachezaji wanane ila walipoumia wawili na kubaki sita ikabidi uishe kutokana na ishu ya kanuni.

Wengine watatu waliofunga mabao matatu ‘hat-trick’ msimu huu ni aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke aliyefanya hivyo dhidi ya Coastal Union Septemba 21, mwaka jana na Stephane Aziz KI wa Yanga aliyeifunga Azam FC Oktoba 23, mwaka jana.

Mwingine ni mchezaji wenzake wa Azam, Kipre Junior aliyefunga wakati timu hiyo ikiifunga Mtibwa Sugar 5-0, Novemba 24, mwaka jana.

KAULI YA DABO

Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo, anasema nyota huyo amekuwa muhimili mzuri wa kikosi hicho kutokana na ubora ambao anaendelea kuuonyesha kwani mbali na kutengeneza nafasi kwa wengine ila amekuwa akifunga jambo linaloleta manufaa kwao.

“Kila mmoja wetu anatambua ubora wake anapokuwa uwanjani hivyo sisi kama benchi la ufundi tunajivunia sana ila kwangu binafsi ninachoamini hiki ambacho anakionyesha kinatokana na ushirikiano na wenzake kitu ambacho ndio bora zaidi kwetu.”

Chanzo: Mwanaspoti