Kufuatia Taifa Stars kuwa na uhaba wa magoli ya kufunga kwenye michezo yao, Jicho la Nasri Khalfan limemuona Feisal Salum Abdallah kama Muarobaini wa kutibu tatizo hili kwani anauwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza nafasi.
Taifa Stars wanatarajia kuingia Dimbani kesho Jumamosi nchini Morocco kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Niger.
"Feisal ni moja ya viungo ambao kwenye ligi yetu wametengeneza nafasi nyingi sana, zipo ambazo zimebadilishwa na kuwa mabao na nyingine hazikutumika.
"Kwa kuanzia, kama Kocha atamwamini na kumwanzisha Fei Toto anaweza kuisaidia Taifa Stars kiasi fulani kwenye hilo. Fei ni kiungo anayeweza kukaa kwenye misingi yetu ya kuisaidia timu kwenye ulinzi.
"Kila mtu anajua namna ambavyo Fei anajituma akiwa uwanjani, lakini tuna mapungufu kwenye kufunga mabao na Fei ni mzuri kwenye hilo licha ya kwamba ni kiungo lakini tayari amefunga mabao matano.
"Anaweza kufunga kutokea mbali au kumalizia pasi karibu na kipa wa mpinzani ama kufunga kwa kichwa.
"Kuna kitu ambacho Fei Toto amekiongeza hivi sasa. Wakati akiwa Yanga alikuwa akipokea mpira tu kuna maeneo unajua atatandika shuti, lakini siku hizi hapigi sana mbali. Kuna maeneo unamuona unadhania atapiga shuti halafu anatoa pasi.
"Inawezekana mabeki wengi wamezoea kumuona akipiga mashuti, kwa hiyo akishika mpira akili yao inakuwa kumzuia asipige shuti, kumbe yeye akili yake inakuwa ni kutoa pasi kwa mtu aliye huru zaidi na anafunga.
"Ndio kwenye mechi ya Mashujaa alitengeneza mabao mawili na mechi ya Ihefu alimtengenezea nafasi nyingi Kipre Junior lakini hakuzitumia.
"Kwa kuanzia kocha anaweza kumpa nafasi kwenye mechi hiyo, hivyo vitu vitatu kwa maana ya uwezo wake wa kufunga, kujituma uwanjani na kukaba inaweza kuwa na faida kwa Taifa Stars," amesema Nasri Khalfan.