Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei Toto afunguka kurejea Yanga

Feisal Salum Fei Toto Malengo Fei Toto

Wed, 4 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kuona sehemu ya kwanza ya mahojiano ya kiungo wa Azam FC Feisal Salum 'Fei toto' akielezea masahibu aliyokutana nayo wakati akilazimisha uhamisho wake wa kutoka Yanga tunaendelea na sehemu ya pili akianza kwa kueleza mafanikio ambayo ameyapata baada ya kusaini kwa matajiri hao wa Chamazi.

"Namshukuru Mungu nimepiga hatua kubwa sana ya kimaendeleo baada ya tu ya kumalizana na Azam kwanza nilimalizia nyumba yetu ya familia naweza kusema mama yangu na ndugu zangu kwasasa wanakaa sehemu ambayo ina heshima, mimi mwenyewe pia nakaa sehemu nzuri biashara zangu binafsi nazo zinakwenda vizuri siwezi kusema ni biashara gani lakini mambo yanakwenda vizuri.

"Nilikuwa sina gari mimi lakini sasa ninazo mbili hapa Dar es Salaam kuna gari moja ninayotumia huku aina ya Crown (Toyota) lakini nikirudi Zanzibar pia nina gari nyingine Harrier (Toyota) kwahiyo maisha yangu yamebadilika mno, namshukuru sana Mungu kilichobaki sasa niipiganie timu yangu tu.

HUMWAMBII KITU KWA NABI

Fei toto alikuwa akiiva vizuri na aliyekuwa kocha wa Yanga Nasreddine Nabi na hapa anaeleza jinsi alivyokuwa akiishi na kocha huyo kabla na baada ya kuondoka Yanga.

"Nabi ni zaidi ya kocha kwangu, ni baba ambaye alikuwa akiishi na sisi kama mzazi, anakuita anakueleza mambo ya maisha na sio tu soka, alipambana sana kujaribu kunirudisha Yanga wakati wa lile sakata, nakumbuka kuna wakati alinipigia simu akanitaka niende kucheza mchezo wa fainali wa Shirikisho hata kwa dakika 45 lakini nilimkatalia kwa kuwa moyo wangu ulikuwa umeshafanya maamuzi.

"Tunawasiliana sana na Nabi mpaka sasa kama mliona hata tulipokuwa Tunisia alikuja kunisalimia kule mazoezini niliumia kumuacha Yanga lakini unajua kwenye maisha kuna wakati unahitajika kuwa na maamuzi sahihi kwa ajili ya maisha yako binafsi.

UTAMU WA MAISHA YA AZAM

"Azam kuna raha siwezi kusema labda sehemu zingine huwezi kupata lakini nipo hapa naona kila kitu kinakwenda vizuri, mchezaji hata kama utapata matatizo utaweza kusaidika kwa haraka, hapa kuna kadi ambazo hata kama kuna ndugu yako anaumwa atatibiwa vizuri kuna mambo ya makato ya mafao nimekuja kuyaona hapa hata kama utakuja kumaliza mpira kuna kitu chako utakipata.

BADO ANA NDOTO ZA KUCHEZA NJE

"Hakuna mchezaji asiyetamani kwenda kucheza nje, kuja kwangu Azam hakujalifuta hilo bado naishi na hizo ndoto lakini kwasasa nataka kurudisha na kuboresha uwezo wangu zaidi ili huko mbele nipate hiyo nafasi.

AZAM KUTOLEWA MAPEMA SHIRIKISHO

"Iliniumiza sana kama mchezaji kwa kuwa hayakuwa malengo yetu iikuwa kama mshtuko mkubwa kwetu lakini Mungu alitupangia hilo nasisi tumelichukua na kuendelea na mapambano, tulikuwa na malengo ya kwenda mbele zaidi hata kufika hatua ya makundi.

HANA SHIDA NA WATU WA YANGA

"Mimi sina ubaya na watu wa Yanga na wala sijawahi kukutana na lolote baya kutoka kwao ukiacha hili la kunizomea uwanjani ambalo nalo ni kawaida, huwa nikitembea nakutana na mashabiki wao wataniambia tu umetukimbia lakini ndio umeamua maisha yako, wapo wengine wana uchungu sana na lile sakata na mimi nasema sina tatizo nao kabisa wala mtu yoyote kwenye klabu yao maisha yangu yanaendelea na yangu yanaendelea.

KUNA SIKU ANAWAZA KUREJEA YANGA?

Anacheka kidogo kisha anajibu; "Huu ni mpira kila kitu kinawezekana hakuna anayejua Mungu atakupangia kipi huko mbele, leo niko hapa pia kesho naweza kwenda sehemu nyingine.

CHIMBUKO LA JINA FEI TOTO

"Jina la Fei toto lilitokana na kuna mchezaji mmoja kipindi cha zamani nyumbani Zanzibar kuna timu inaitwa Zimamoto, kulikuwa na mchezaji anacheza nafasi kama yangu alikuwa akitumia hili jina la Fei Toto sijaua sasa yuko wapi jina lake mashabiki ndio walinipa mimi na sababu ya kunipa hili ilikuwa ni kutokana mimi nilianza kucheza soka nikiwa na umri mdogo sana alafu nilikuwa sichezi na wadogo wenzangu nilikuwa nacheza na watu walionizidi sana umri,”

UJIO WA BANGALA, DJUMA NDANI YA AZAM

"Ujio wao kuna kitu umeniongezea kwamba watu ambao nilikuwa nao kabla baadhi nimeungana nao nilikuwa nao kule Yanga na wao wamekuja huku Azam maisha yanaendelea, naona kama marafiki zangu nao kama wanakuja huku kwa wingi,”

 SIRI YA JEZI NAMBA 6

"Mimi huwa napenda sana kuwaangalia wachezaji walionizidi nampenda sana Xavi (Hernandez aliyekuwa kiungo wa Barcelona na sasa kocha wa timu hiyo) na huyu ndiye aliyenifanya niipende hii jezi, nilikuwa napenda sana ufundi wake uwanjani ukimuangalia unafurahia mpira na kuona ni kitu rahisi.

JEZI YAKE KUPEWA SKUDU

Baada ya Fei toto kuondoka Yanga jezi yake namba sita ilitua kwa Msauzi Mahalatse Makudubela 'Skudu' na jamaa anasema wala hawaingilii na anakumbali aliyepewa.

"Siwezi kuwaingilia maamuzi yao unajua mimi sasa niko huku Azam, aliyepewa jezi ile mimi namtakia kila la kheri na uzuri aliyepewa ile jezi ni Skudu ni rafiki yangu pia nilimjua kupitia Bernard Morrison na hata alipokuja hapa nilikutana naye siku moja uwanja wa ndege tuliongea vizuri na nikamkaribisha nchini na namtakia kila la kheri apambane tu kufanya mazuri kushinda niliyoyafanya mimi,”

FEDHA ZA MICHANGO YA MASHABIKI WAKE

"Baada ya sakata la kutaka kuindoka Yanga Fei toto aliwaomba mashabiki wanaompenda kumchangia fedha ili apate ada ya kufungua kesi Mahakama ya usuluhishi ya michezo (CAS) na hapa anaeleza fedha zile zilipokwenda; "Zile fedha zilichangwa nyingi sana zilifika kama milioni thelathini au arobaini hivi sikumbuki vizuri na zote nilizipeleka Wizara ya Afya Zanzibar zikatumika kununulia vitu vya hospitali.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: