Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei Toto: Simba watusamehe, tunaitaka Ligi ya Mabingwa

Fei Toto Azam Mkd Fei Toto.

Thu, 23 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania, kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Feitoto' amesema wanapambana katika michezo iliyobakia kwa sababu nia na malengo yao ni kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Azam FC yenye pointi 63 sawa na Simba iko katika nafasi ya pili, ikiwa na idadi nzuri ya mabao ya kufunga ukilinganisha na Wekundu wa Msimbazi wakati Yanga tayari imeshatwaa ubingwa.

Fei Toto aliliambia gazeti hili wachezaji wa Azam FC hawataki kuona wanapoteza mechi yoyote katika michezo miwili iliyobakia ili kufikia ndoto za kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitimie.

"Tunashukuru tumepata ushindi katika mchezo wetu dhidi ya JKT, ulikuwa mchezo mgumu lakini ilikuwa lazima tupate ushindi ili tusitoke kwenye mbio zetu za kumaliza katika nafasi ya pili," alisema kiungo huyo.

Aliongeza michezo yote iliyobakia ni ya presha kwa sababu pia Simba wanaihitaji nafasi hiyo ili kujihakikishia tiketi ya kushiriki katika michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

"Hatutaki kuangalia michezo yao au matokeo yao (Simba), kikubwa sisi ni lazima tufanye vizuri katika michezo yetu, kuteleza kwa namna yoyote kutatuondoa kwenye nafasi hii, tutakuwa makini mpaka mwisho wa msimu," alisema Fei Toto.

Wakati huo huo, Fei Toto ameendelea kujiimarisha katika mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu baada ya kufikia mabao 16, moja zaidi ya mshambuliaji wa Yanga, Stephanie Aziz Ki.

"Nashukuru nimefunga na kuisaidia timu yangu kupata ushindi, kwangu mimi kitu kikubwa ni matokeo ya timu, kumaliza nafasi ya pili, kama itatokea nimepata tuzo ya ufungaji bora ni sawa, nitafurahi lakini kikubwa kwa sasa nafunga si kwa ajili ya kiatu cha dhahabu, bali kwa ajili ya timu kupata matokeo mazuri ili kama timu tufikie malengo yetu ya sasa," alisema Mzanzibari huyo.

Yanga itafunga pazia la msimu huu kwa kuwakaribisha Maafande wa Tanzania Prisons kutoka jijini, Mbeya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live