Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei Toto, Bacca kuivaa Kilimanjaro Stars Amaan

Bacca X Fei Fei Toto, Bacca kuivaa Kilimanjaro Stars Amaan

Sun, 24 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo nyota wa Azam FC, Feisal Salum 'Feit Toto', beki Ibrahim Bacca wa Yanga ni miongoni mwa wachezaji walioitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes itakayovaana na Kilimanjaro Stars ya Tanzania Bara kwenye mechi maalumu ya ufunguzi wa Uwanja wa Amaan uliofanyiwa ukarabati.

Mechi hiyo ya kirafiki inatarajiwa kupigwa Jumatano ya Desemba 27 ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 itakayochezwa siku inayofuata kwenye uwanja huo uliokuwa kweenye matengenezo yaliyobadilisha muonekana wake kwa sasa ukiwa wa kisasa zaidi.

Kocha Mkuu wa Zanzibar Heroes, Hemed Suleiman 'Morocco' amewataja wachezaji 29 wa kuunda timu hiyo ya kuivaa timu ya Kili Stars na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mbali na Fei Toto na Bacca, kocha Morocco amewaita nyota kadhaa wanaocheza Ligi Kuu Bara na Zanzibar, akiwamo Mudathir Yahya, Seif Karihe, Matteo Antony na kipa wa Singida Fountain Gate, Ibrahim Abdalla.

Kikosi kizima cha Zanzibar Heroes kipo hivi; Makipa ni Ahmed Ali (Uhamiaji), Ibrahim Abdalla (Singida FG), Yakoub Suleiman (JKU), huku mabeki ni Adeyum Saleh (Dodoma Jiji), Ibrahim Hamad (Yanga) na Suwedi Juma wa JKU, Abdalla Said (Mlandege), Abdul-Malik Adam (Namungo) na Mukrim Issa (Singida FG) na Baraka Mtui wa Mashujaa.

Kwa upande wa viungo wamo Suleiman Ame (Zimamoto), Is-Haka Said, Nassir Sheha (KMKM), Hassan Nassor 'Machezo' wa JKT Tanzania, Mudathir Yahya, Sheikhan Ibrahim (Yanga), Feisal Salum (Azam FC), Suleiman Saleh (Chipukizi), Abdul Aziz Makame (asiye na timu kwa sasa), Muhammed Yahya (KVZ),

Khalid Habibu (Singida FG), Hassan Cheda (Mashujaa) na Khelfin Hamdon anayekipiga Muscut Uarabuni.

Washambuliaji ni Matteo Anthony, Seif Karihe wanaochezea Mtibwa Sugar, Maabad Maulid (Coastal Union), Abdulnassir Assa (Mashujaa), Mohammed Mussa (Simba) na Ibrahim Hamad 'Hilika wa Zimamoto.

Morocco amesema kikosi hicho kinaingia kambini kesho Jumatatu na kitakuwa huko kwa siku mbili kabla ya mchezo huo ambao umepewa heshima kubwa na utatanguliwa na burudani kadhaa za muziki ikiwamo Diamond Platinumz na Malkia wa Mipasho Khadija Omar Kopa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Kibabu Haji Hassan amewaomba viongozi wa klabu kuwaruhusu wachezaji hao kwa sababu jambo hilo ni la kitaifa.

Uwanja wa Aman kwa Sasa kimekuwa na hadhi ya kimataifa takriban maeneo yote ya uwanja huo yameboresha kwa ustadi mkubwa, ikiwamo kuwekwa kwa paa na nyasi bandia za kisasa na kuongezwa kwa idadi ya mashabiki watakaokaa kwenye vitu vya kisasa kutoka 12,000 hadi 16,200.

Chanzo: Mwanaspoti