Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei Toto? Aah wapi! Mkataba bado unapumua

Fei Toto Jicho.jpeg Kiungo wa Yanga, Feisal Salum

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa soka wa Yanga wapo roho juu juu baada ya kusikia kiungo fundi wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ yupo kwenye rada za kutakiwa na klabu nyingine ikiwamo Azam FC, lakini mkataba alionao klabuni hapo na baadhi ya mambo yanampa wakati mgumu kiungo huyo kutoka.

Licha ya mwenyewe kukataa kusema lolote akitaka menejimenti ndio itafutwe, lakini mtu wa karibu wa fundi huyo wa Kizanzibar aliliambia Mwanaspoti Fei Toto ana ofa nyingi zikiwamo kutoka nje ya nchi, huku kwa timu za hapa nyumbani ni Azam ndio inayohusishwa naye.

Inadaiwa ni kweli Azam inammezea mate Fei, ila itakuwa ngumu kumng’oa kutokana na mambo kadhaa ikiwamo mkataba wake, sambamba na kuelezwa kwa sasa anasimamiwa na Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Haji Arafat baada ya kutemana na Zubery Kambi anayemiliki Akademi ya Kambiaso.

Fei aliyejiunga na Yanga msimu wa 2018-2019 akitokea JKU ya Zanzibar, awali alishaonekana akaenda Singida United kabla ya kufanyika umafia uliomleta Jangwani na kwa sasa ana mkataba hadi Mwaka 2024 huku ikielezwa kwa sasa analilia kuboreshewa masilahi yake hasa mshahara.

“Sio siri Fei ana ofa nyingi mezani kwa waajiri wake, zikiwamo za nje na kwa hapa nchini hizi taarifa za Azam sio uzushi ni kweli wanamtaka, ila mkataba unambana,” kilisema chanzo hicho cha karibu cha nyota huyo mwenye mabao manne kwa sasa Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, mabosi wa Azam jana walitafutwa ili kufafanua juu ya ofa hiyo ya kumtaka Fei na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’ aliruka kimanga.

Popat alisema kwa kifupi; “Hakuna ukweli wowote kuhusu usajili wa Fei Toto kuja kwetu na hadi sasa hakuna hitaji lolote la usajili kutoka kwa makocha wetu, watakapoleta basi tutafanyia kazi na si vinginevyo.”

Pamoja na Azam kuchomoa kumhitaji Fei, Kaimu Afisa Habari wa Azam, Hashim Ibwe, ndiye aliyeibua sakata hilo kwa kuweka hadharani kupitia akaunti za mitandao ya kijamii kiu ya kumtamani.

Lakini kuna mambo ambayo yanaweza kukwamisha dili la kiungo huyo kwenda Azam hata kama klabu hiyo itakuwa inamtaka aungane na mafundi wengine pale Chamazi ikiwamo;

MKATABA

Mkataba wa sasa wa Fei na Yanga bado unapumua tena kwa pumzi zisizo na mapigo ya kutisha, jamaa ukichukua msimu unaoendelea ongeza na msimu mwingine unaokuja, hii ni ndoa nzuri ambayo Yanga waliingia nayo kwa kiungo huyu. Fei toto amewafanyia uungwana Yanga, akiwakumbusha mapema hatua ambayo Rais wa klabu hiyo, Hersi Said na hata wafadhili wao GSM hawataweza kuruhusu kirahisi kuondoka kwa staa wao huyo mzawa kirahisi.

Anaweza kutingisha labda afanyiwe maboresho ya masilahi yake lakini haitaweza kufika mpaka mwisho wa msimu ujao, hujaiona picha au video fupi ya kiungo huyo akisema ameamua kubaki zaidi.

NAMBA KIKOSINI

Ukipewa kazi ya kuvitaja vikosi viwili tu vya Yanga unaweza kujikuta moyo wako unakulazimisha kila kikosi ukamweka Fei ndani na hata ukiiangalia Yanga iliyo na Fei hasa akicheza nyuma ya fowadi wa mwisho yaani namba 10 anakuwa katika ubora gani na hilo ndilo linalowasukuma mabosi wa Yanga kuwa makini kumaliza sakata lake haraka mbali na kusimamiwa na mmoja wa vigogo wa klabu hiyo.

Pia kuna maelewano mazuri kati ya Fei na kocha Nasreddine Nabi, hivyo huenda sio rahisi kwa kocha huyo kusema hamtaki kiungo huyo katika kikosi chake, japo anaweza kumuacha ndani ya timu hiyo.

Nabi anamkubali Fei kutokana na ubora wake na sio Nabi tu kocha yeyote angefanya hivyo na ebu vuta picha jinsi kocha huyo alivyompuuza hadharani kwa kusema ukweli juu ya Said Ntibazonkiza ‘Saido’ alipodai ni vigumu kwake kumtanguliza Mrundi huyo mbele ya Fei toto kutokana na kijana huyo wa Kizanzibar injini yake bado ina nguvu ya kuipigania timu. Pia Fei ni roho ya mashabiki wa klabu hiyo.

REKODI ZA NGASA, SURE BOY

Yanga imewahi kufanya biashara na Azam ikiwauzia winga Mrisho Ngassa mwaka 2010, hata hivyo baadaye Ngassa alikumbuka nyumbani na Yanga wakatamani sana kijana wao arejee nyumbani kwao tena.

Azam iliweka ngumu kumruhusu arejee licha ya vitimbi vingi alivyovifanya Ngassa, ambaye baadaye alipelekwa Simba na kuifanya Yanga iumie, hivyo huenda hilo ikaifanya Yanga kuweka ngumu kumwachia hasa ikiwa kwa sasa haina njaa kama ilivyokuwa kabla ya kuwanasa GSM.

Kadhalika Yanga inakumbuka namna ilivyobaniwa ilipokuwa inamtaka mapema Salum Aboubakar ‘Sure boy’, hadi ikafikia mchezaji huyo kuanzisha mgomo baridi uliomtia kitanzini na kisha kugoma kusaini mkataba mpya ili kutimiza ndoto zake za kucheza klabu aliyowahi kuitumikia baba yake.

MWANDAMIZI NA REKODI ZA SIMBA

Katika kikosi cha sasa cha Yanga, Fei ndiye mwandamizi kwani tangu alipotambulishwa kwa mara ya kwanza klabuni hapo Julai 13, 2018 hakuwahi kutoka kwenda popote na yeye ndiye amekuwa akipokea na kuwaaga nyota wengine wanaokuja na kuondoka Jangwani tangu mwaka huo.

Fei, pia amepitia nyakati ngumu na huzuni ndani ya Yanga hadi msimu uliopita timu hiyo ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC, mbali na ngao za jamii za msimu uliopita na huu wa sasa, huku rekodi yake tamu ya kuinyanyasa Simba ikizidi kupigilia misumari ya kubakia Jangwani.

Kiungo huyo amekuwa na rekodi ya kuwafunga watani wao Simba tena mabao ya kikatili, likiwemo la nusu fainali ya Kombe la ASFC lililoipeleka Yanga fainali na kubeba mbele ya Coastal Union.

Rekodi kama hii wapo wachezaji wakubwa waliowahi kupita Yanga walishindwa kuishi nayo hata kwa dakika moja akiwemo fundi Haruna Niyonzima na wengine, ni msimu huu aliwagomea kabisa Azam akiingia kipindi cha pili na kuisawazishia mabao 2 na kuifanya mechi kali na ngumu kuisha kwa sare.

Chanzo: Mwanaspoti