Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei: Kiatu cha Dhahabu? Subirini muone

Fei Toto 9 Goals Fei: Kiatu cha Dhahabu? Subirini muone

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Maajabu katika Ligi Kuu Bara msimu huu yanaendelea ikiwa yale ya karibuni zaidi ni kiungo wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' kumshusha Aziz Ki wa Yanga kileleni mwa msimamo wa wafungaji bora akifikisha bao la 11 - ikiwa ni moja zaidi ya kiungo huyo Mbukinabe wa Yanga.

Lakini wakati ukiduwazwa na Fei Toto, huku nyuma Yusuph Mhilu naye kauona mwezi baada ya siku 442 kupita akiwa hajafunga bao lolote la mashindano.

Unamkubuka Mhilu? Jamaa alipokuwa Simba misimu miwili iliyopita ambapo aliishia kusugua benchi, kabla ya kufunguliwa mlango na kurejea zake Kagera Sugar? Sasa buana huko nako aliishia kusugua benchi kisha akasepa zake kwenda Geita Gold msimu huu na huko ndiko kauona mwezi katika sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC.

Tukirejea kwa Fei Toto, kazungumzia ishu ya kiatu cha ufungaji bora, na ingawa amekiri kwamba anakabiliwa na kazi ngumu, lakini ameimarika zaidi, hivyo lolote linaweza kutokea katika ufungaji bora ifikapo mwisho wa msimu.

Fei Toto amefunga mabao 11 akitoa pasi tano zilizozaa mabao, hivyo akiwa amehusika moja kwa moja na mabao 16 yaliyofungwa na timu yake akimshusha Aziz Ki ambaye ametupia 10 na asisti mbili katika mechi 16.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto amesema vita ya ufungaji bora ni ngumu na anaheshimu uwezo wa Aziz Ki kwani ni mchezaji bora na mzoefu, lakini ameahidi kutapambana naye huku akiipambania timu yake kufikia malengo.

"Sipendi kushindanishwa na mtu naomba nifanye kazi yangu na kwa kutumia kila nafasi nitakayoipata bila kumuangalia nani ananifuata, lakini pia naheshimu uwezo wa Aziz Ki ni mchezaji ambaye pia tutegemee mazuri kutoka kwake," amesema Fei toto na kuongeza:

"Endapo (Aziz Ki) atafunga mabao mengi kunizidi nitampongeza na mimi nikifunga mengi kumzidi nitashukuru na nitakuwa nimeonyeha utofauti na misimu mingine kwa kufunga mabao mengi zaidi."

Akizungumzia siri ya mafanikio yake ndani ya kikosi cha Azam FC, mchezaji huyo amesema ni kujitunza, kufanya mazoezi kwa bidii na kuzingatia maelekesho ya kocha ambaye amekuwa akimuamini na kumpa nafasi ya kucheza.

"Siri ni kujitunza, kufanya mazoezi kwa bidii na kuzingatia maelekezo hakuna kitu kingine cha ziada na pia malengo yangu ni kuhakikisha naipambania Azam FC ifikie malengo," amesema.

"Kazi iliyonileta Azam FC naifanya kama walivyokuwa wanatarajia kutoka kwangu na naamini mambo mazuri zaidi yanakuja. Tuzo za mchezaji bora wa mwezi mzitarajie sana kutoka kwangu."

Rekodi ya Fei Toto kabla ya kutua Azam FC misimu yake miwili ndani ya kikosi cha Yanga alifunga mabao 12 kwenye kila msimu mabao sita.

Katika kikosi cha Azam, Fei ndiye anayeongoza ufungaji wa mabao akifuatiwa na Prince Dube anayeandamwa na majeraha ya mara kwa mara aliyetupia saba, huku Idd Selemani ‘Nado’ na Kipre Junior wakifunga manne kila mmoja.

Msimu huu umekuwa bora zaidi kwa Fei tofauti na alipokuwa Yanga misimu miwili iliyopita kwani hajawahi kuzidi mabao sita.

Katika msimu wa 2021-2022 akiwa Yanga alicheza dakika 2044 kwenye michezo 26 kati ya 30 ya Ligi Kuu Bara ambapo alifunga mabao sita na kuasisti manne, huku msimu wa 2022-2023 akifunga pia sita tofauti.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: