Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fedha, taaluma chanzo cha makocha 11 kutimuliwa Ligi Kuu

Robertinho 5.jpeg Aliewahi kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Tanzania Bara imeshachezwa wastani wa michezo 14 hadi sasa, ingawa kuna timu nyingine zina michezo michache kuliko hiyo huku ikisimama kwa muda hadi Februari mwakani.

Ni ligi ambayo imekuwa na mvuto wa kipekee huku kila timu ikionesha kuna jambo imejiandaa na inalitaka, ingawa baadhi bado mambo siyo mazuri kutokana na aina ya matokeo ambayo zimekuwa zikiyapata.

Timu za Simba, Yanga na Azam kama ambavyo zimekuwa kwenye misimu kadhaa nyuma zimeendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha zinawania ubingwa, huku nyingine zikitaka kumaliza kwenye nne bora na baadhi kubaki tu kwenye ligi.

Hata hivyo, presha kubwa ya ligi msimu huu imesababisha makocha wa timu 11 kati ya 16 hadi sasa kutimuliwa, jambo ambalo linaleta hofu kwa makocha wengine waliopo kwenye timu zao.

Ni timu tano tu kwenye ligi, Yanga, Tabora United, JKT Tanzania, KMC na Mashujaa ambazo hazijawafurumisha makocha wao.

Kwa upande wa Tabora kocha wake Goran Copunovic, sina imani kama anaweza kubaki hadi Februari kutokana na aina ya kauli zake ambazo alizitoa kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Yanga ambao ulimalizika kwa Yanga kupata ushindi wa bao 1-0.

Kocha huyo alionekana kutoa kauli za kuonyesha kuwa hana maisha marefu kwenye timu hiyo jambo ambalo linatoa shaka kuwa anaweza asiwepo kwenye kikosi hicho mzunguko ujao.

Hata hivyo, kitendo cha kufukuzwa makocha 11 kinaonyesha kuna tatizo kubwa kwenye soka na kama mabadiliko ya haraka hayatafanyika basi hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

ZILIZOFUKUZA:

SINGIDA FOUNTAIN GATE (3)

Singida inaonekana hadi sasa ndiyo inashikilia rekodi ya kufukuza kuliko timu nyingine kwenye ligi hiyo.

Tayari imeshatimua makocha watatu, ilianza msimu na Hans van Pluijm ikamuondoa na kumchukua kocha mwenye uwezo mkubwa Ernst Middendorp ambaye alidumu na timu hiyo kwa wiki mbili tu, baadaye timu hiyo ikamchukua Ricardo Ferreira raia wa Brazil.

Unajua nini kilitokea? Baada ya miezi miwili, Singida ilimkatia tiketi kocha huyo akarejea kwao baada ya kuiongoza kwenye michezo tisa tu.

MTIBWA (1)

Pamoja na kwamba bado ipo mkiani lakini mwanzoni tu iliachana na aliyekuwa kocha wake, Habib Kondo na sasa timu ipo chini ya Zubeir Katwila ambaye aliondolewa Ihefu. Imeshinda michezo miwili tu na kutoa sare miwili kwenye michezo 14.

NAMUNGO (2)

Hii ni timu ambayo kwa msimu uliopita ilionekana kuwa na ushindani mkali na wengi waliamini msimu huu ingekuwa moto, lakini mambo yamegeuka.

Namungo imeshatimua makocha wawili hadi sasa baada ya michezo 14 tu, ilianza na kocha mwenye jina kubwa Cedric Kaze, mambo yakawa hayaendi ikamtimua na kumpa timu kocha wao wa zamani, Denis Kitambi, akaondoka na sasa timu ipo chini ya Mwinyi Zahera ambaye ametimuliwa Coastal Union, hata hivyo, kwenye michezo 14, imeshinda minne tu na kutoka sare mitano.

IHEFU (3)

Kama ilivyo kwa Singida, hali hiyo ipo pia kwa Ihefu ambayo imeingiza kocha wa tatu kwenye michezo 14 ya mwanzo, ikiwa imeshinda michezo mitatu tu hadi sasa.

Timu hii ya Mbarali Mbeya, ilianza na Mzawa Zubeir Katwila akapambana ikaachana naye akatimkia Mtibwa timu akapewa Mganda Moses Basena mambo yakawa magumu, sasa ipo chini ya Mecky Maxime ambaye alijiunga akitokea Kagera Sugar.

GEITA (1)

Geita Gold haina kocha wake iliyoanza naye kwa sasa, Hemed Morocco.

Huyu alianza msimu baadaye akaondolewa na sasa kocha mkuu ni Kitambi ambaye alikuwa Namungo, Morocco ameiongoza timu hiyo kushinda michezo minne tu na kutoka sare minne.

COASTAL 1

Coastal ilianzia kwa Mwinyi Zahera, mambo yakagoma akaondolewa na sasa timu ipo chini ya Mkenya David Ouma. Hata hivyo, imeshinda michezo mitano tu kati ya 14.

PRISONS (1)

Mara kwa mara Fred Felix ‘Minziro’ amekuwa akipigiwa debe na mashabiki kuwa arejee kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kufanya kazi ya kuzipandisha timu nyingi, alianza na Prisons mambo yakagoma akaondolewa timu ikiwa imeshinda michezo minne kati ya 14.

DODOMA JIJI (1)

Melis Medo alianza vizuri na timu hii na kuonekana anaweza kufanya makubwa, lakini katikati mambo yakagoma, akapewa barua ya kwa heri, timu ikachukuliwa na Francis Baraza. Kwa jumla imeshinda michezo mitano kati ya 13.

SIMBA (1)

Pamoja na kwamba alikuwa hapewi nafasi kubwa ya kutimuliwa, kichapo cha mabao 5-1 ilichokipata kutoka kwa Yanga kilimuondoa Roberto Oliveira ‘Robertinho’ Simba na nafasi yake ikachukuliwa na Abdelhak Benchikha, timu hiyo imecheza michezo michache zaidi kuliko zote zilizotimua makocha ikiwa ina mechi 10 tu imeshinda saba na kutoka sare mbili, huku ikipoteza moja. Hii ndiyo timu iliyofukuza kocha na kuwa na wastani mzuri.

KAGERA SUGAR (1)

Hii ilikuwa timu ya mwisho kuachana na kocha, baada ya kumalizana na Maxime ambaye amekwenda Ihefu, akiwa hapo alishinda michezo mitatu tu kati ya 13, kwa sasa haina kocha mkuu.

WAGENI WASTAARABU:

Yanga, Azam, KMC, Tabora United, JKT Tanzania, Mashujaa ni kati ya zile ambazo hazijafukuza makocha kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo timu tatu ni zile zilizoopanda daraja msimu huu na zimeonekana kuwa kwenye sehemu nzuri kwenye ligi.

KWANINI WANATIMULIWA?

Imeonekana kuna sababu kadhaa ambazo zimesababisha makocha wengi kutimuliwa mmoja kati ya makocha ambaye aliondolewa kwenye timu moja alisema:

“Ukiisikia Ligi Kuu ya Tanzania ukiwa nje unaamini kila mchezaji ni wa kiwango kile ambacho unafikiri, lakini unapofika kwenye timu unakutana na mambo tofauti, wachezaji wengi ni wale ambao wanahitaji muda zaidi lakini klabu zinakuwa hazina muda wa kusubiri, hivyo utaondolewa tu kwa kuwa huwezi kucheza wewe.”

FEDHA:

Kiwango kikubwa cha fedha ni jambo lingine ambalo lipo kwenye ligi yetu kwa sasa na linawaaminisha baadhi ya mabosi wa timu, wanaweza kuachana na kocha wakati wowote wakamlipa na kuajiri mwingine, tofauti na hali ilivyokuwa hapo nyuma ambapo timu nyingi zilikuwa zikiwa na hofu kwa ajili ya fedha za kuwalipa makocha pale zinapowatimua.

Chanzo cha ndani kinaonyesha kuna baadhi ya makocha wazawa wanalipwa hadi milioni 14 kwa mwezi kama mishahara yao na wana mikataba ya miaka miwili hii imekuwa ikiwapa pia mabosi wa timu wakati mgumu wa kuona wanatoa fedha nyingi lakini mafanikio uwanjani hakuna wanatimua.

TAALUMA:

Baadhi ya makocha ambao wametoka nje, wamekuja nchini wakiwa wameshafundisha baadhi ya timu kubwa, hivyo wamezoea timu zinazoendeshwa kisasa, wakati mwingine jambo hilo kwenye soka letu limeshindikana hivyo inamfanya kocha huyo ashindwe kutimiza malengo yake.

Mfano, kitaalamu kuna kazi za kocha na kazi za viongozi, wakati mwingine kwenye soka letu vitu hivyo vimekuwa havifuatwi sana hadi madai ya wengine wanahojiwa kwanini walimtumia mchezaji fulani na siyo fulani jambo ambalo limekuwa likiwafanya waondoke na kurejea makwao.

WASAIDIZI:

Makocha wengi wamefanikiwa kutokana na kuwa na wasaidizi wao ambao wanafahamiana kuanzia walipotoka, kwenye soka la sasa imekuwa ngumu kwa kocha mkuu kufanya kazi na wasaidizi ambao hawafahamiani, kwetu bajeti imekuwa kikwazo cha makocha kuja na wasaidizi wake.

MATARAJIO MAKUBWA:

Mabosi wengi wa timu wamekuwa wakiwapa makocha timu wakitarajia mambo makubwa kutoka kwao kwenye michezo ya kwanza tu jambo ambalo limekuwa likishindikana kutokana na aina ya wachezaji ambao kocha amewakuta na hivyo huanza kuvurugana na mwisho huachana.

Lakini hapa pia kunachangiwa na ahadi za makocha kwa mabosi baada au kabla ya kusaini mikataba.

Chanzo: Mwanaspoti