Winga wa timu ya Yanga, Farid Mussa amepona majeraha ya nyama za paja yaliyomuweka nje ya uwanja kwa takribani miezi miwili na sasa yupo fiti kwa asilimia 100 kuitumikia timu hiyo.
Farid alipata majeraha hayo wakati wa maandalizi ya mchezo wetu wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya pili dhidi ya Al Merrikh ya Sudan uliochezwa Septemba 30, 2023 jijini Dar.
Taarifa iliyotolewa na Klabu ya Yanga imesema kuwaa, Farid amesema anamshukuru Mungu amepona kabisa na kuanza mazoezi ya pamoja na timu, huku akiwaomba Wananchi kumpokea vizuri.
“Niliumia mazoezini tulipokuwa tukijiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Al Merrikh, baada ya mechi kule Kigali, tuliporudi ndio nikaumia mazoezini.
“Nikaenda kupimwa nikagundulika nimechana nyama za paja, hivyo nikapewa wiki sita, ni mwezi mmoja na takribani wiki mbili.
“Kwa hiyo sasa hivi namshukuru Mungu nimeshamaliza na nimeshaanza mazoezi na timu, niko fiti. Wananchi wanipokee vizuri tuendelee kufanya kazi tulipoishia.
KUHUSU KURUDI KWENYE KIWANGO CHAKE “Unajua kitu kikubwa kwenye mpira ni kuwa fiti, mwili ukiwa vizuri unaweza kufanya kila kitu, mimi sehemu niliyoumia haikuwa inaniruhusu kukimbia kwa hiyo nilikuwa nafanya mazoezi madogo, hivyo kwa sasa ili kurudi kwenye hali yangu, lazima nifanye mazoezi ya ziada,” alisema Farid.
Kwa upande wa Daktari wa Yanga, Moses Etutu, alizungumzia kitaalamu tatizo lililokuwa likimsumbua Farid kwa kusema: “Alichanika nyama za paja, akaendelea na matibabu na kwa sasa asilimia mia yupo fiti kwani ni zaidi ya wiki mbili sasa amepona.
“Baada ya kupona amefanya mazoezi ya kawaida kurudisha fitnesi ambayo naamini tayari ameipata, kwa hiyo tunasema tushasahau kama alikuwa na shida hiyo. Hivi sasa yupo fiti.
USHAURI JUU YA KULINDA UWEZO WAKE “Kwa sasa anatakiwa kupata muda mwingi wa kupumzika baada ya mazoezi na kuwa na ratiba nzuri ya chakula na kuzingatia mazoezi, nadhani hicho kitamsaidia sana.”