Kiraka wa Yanga anayemudu kucheza kama winga na beki wa kushoto, Fardi Mussa amekiri Kocha Miguel Gamondi anastahili jina la Masta, kwani hana mchezo kabisa na amekuwa akiwasapraizi wachezaji kila inapokuja mechi kiasi mchezaji anayeharibu huwa inakula kwake mazima.
Farid anafichua Gamondi yupo tofauti na Nasreddine Nabi aliyeinoa timu hiyo kwa miaka miwili na nusu kabla ya kutimkia FAR Rabat ya Morocco ambaye amekuwa akiwaandaa wachezaji atakaowatumia kwa kuwaambia siku mbili hadi tangu kabla, kwani Muargentina huyo anawashtukiza wachezaji kuanza gemu.
Tabia ya Gamondi ipo hivi: Kwa mujibu wa Faridi ni kwamba kocha huyo anataka kila mchezaji awe tayari wakati wowote anapotaka mchezaji kumtumia uwanjani, hivyo haonyeshi kikosi cha kuanza mapema wakati wa mazoezi kama anavyosema ilivyokuwa kwa Nabi.
Farid alichambua utofauti wa makocha hao, alisema Nabi ukuiwa kwenye mpango wa kukutumia atakwambia siku tatu kabla ya mechi ili ujiandae kiakili na kimwili tofauti na Gamondi na anafafanua;
“Gamondi ipo tofauti kabisa anataka akili yako na mwili viwe tayari kabisa muda wopte kwa ajili ya mchezo.” Farid alisema mchezaji kuandaliwa kwa kuambiwa kesho utacheza ni nzuri, kwani anakuwa anajiandaa kimbinu na kiakili tofauti na kukurupushwa, ingawa imewafanya wachezaji makini na kujiandaa mapema.
“Ndio kazi yangu ni kucheza, lakini nikiandaliwa kwa kuambiwa nacheza kesho nakuwa katika hali nzuri ya kuuweka mwili tayari tofauti na nikikurupushwa kwani tabia zetu wachezaji tunazijua wenyewe,” alisema Farid na kuongeza;
“Hakuna mtu ambaye anakuwa bora zaidi ya yule ambaye amekuwa akicheza mara kwa mara lakini kwa sisi wachezaji ambao tumekuwa tukianzia benchi muda mwingi ni ngumu kuwa bora siku tukifanyiwa sapraizi ya kuanza kikosi cha kwanza licha ya kufanya mazoezi kila siku.”
Nyota huyo wa zamani wa Azam aliyewahi pia kucheza soka la kulipwa Hispania, alisema saikolojia ya mchezaji inatakiwa kujengwa kuanzia mazoezini hadi siku ya mchezo, hivyo kitendo wanachofanyiwa na Gamondi kinawafanya kijiandaa na kujifunza kwani hawaelewi wanaweza kuanza au kuanzia benchi.
“Mpango wake mwanzo ulikuwa mgumu, lakini sasa kila mchezaji amejijengea imani anaweza akakurupushwa na kuanza amekuwa akijiandaa tayari kwa mchezo wowote ulio mbele yake,” alisema Farid na kuongeza;
“Kwa upande wa Nabi ubora wa kila mchezaji ulikuwa unaonekana hii ni kutokana na kujengwa kimwili na kiakili kuwa kesho jiandae na tuliza mwili wako tunakutegemea. Ukiambiwa hivyo wewe kama mchezaji sasa unajiandaa vizuri na kujiweka tayari kwa mapambano na ndio maana kulikuwa hakuonyeshi nani ameathiliwa na benchi wote tulikuwa kwenye nafasi nzuri ya ushindani.”
“Wote ni bora ndani ya muda mchache wameifanya Yanga iwe bora kimataifa Nabi kaifikisha timu hiyo fainali Kombe la Shirikisho Afrika baada ya miaka mingi huku akiweka rekodi katika Ligi.”