Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia za watu wa mpira zenye pesa nyingi Ulaya

Fxtrsrxr Familia za watu wa mpira zenye pesa nyingi Ulaya

Sun, 24 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mwanasoka wa kiume anapoangukia kwenye penzi la mwanamke mjasiriamali, kinachokea ni kutengeneza pesa za kutosha.

Kuna mahusiano hayo ya mwanasoka wa kiume na mrembo mjasiriamali, yamekuwa ya kitajiri sana kutokana na mkwanja wao wa pamoja wanaovuna na kuendeesha maisha yao.

Kama ilivyotarajiwa, pea ya supastaa, Cristiano Ronaldo na mrembo Georgina Rodriguez itakuwamo kwenye orodha hiyo ya mahusiano yenye mkwanja mrefu.

10. Raheem Sterling na Paige Milian, Pauni 37milioni

Raheem alianza uhusiano wa kimapenzi na mrembo Paige tangu akiwa QPR, walipokuwa wadogo kabisa. Mrembo huyo alikuwa akifanya kazi JD Sports, mahali ambako alionekana na mkali huyo wa Chelsea na kuanzisha uhusiano.

Paige anaongoza miradi kadhaa. Wawili hao amefanikiwa kupata watoto wawili, wakati Raheem tayari alikuwa na mtoto mwingine wa kike aliyezaa kwenye uhusiano mwingine. Pacha hiyo inaripotiwa kuwa na utajiri wa Pauni 37 milioni.

9. Thomas Muller na Lisa Trede, Pauni 44milioni

Mke wa gwiji wa Bayern Munich na Ujerumani, Muller, mrembo Lisa ni mbunifu wa mavazi na kampuni yake imekuwa imara sana huko kwao. Ana uwezo wa kuzungumzia lugha mbalimbali kumrahisishia kwenye biashara zake. Wawili hao walikutana mwaka 2007 na miaka miwili baadaye wakafunga ndoa.

Bado hawajafanikiwa kupata mtoto, lakini kwenye akaunti yao ya benki mambo ni matamu kwelikweli, wakiwa na mkwanja unaoripotiwa kuwa Pauni 44 milioni.

8. Mario na Ann-Kathrin Gotze, Pauni 68milioni

Mrembo Ann-Kathrin ni mwanamitindo na mhamasishaji, ambaye pia amekuwa akionekana kwenye vipindi vya televisheni. Kwenye mitindo aliibukia katika mashindano ya Germany’s Next Top Model, na tangu wakati huo amekuwa moto, akipata dili mbalimbali za mavazi ya ndani, hasa mavazi ya kuogelea, ambayo amekuwa akipiga picha na kuposti Instagram. Wawili hao walikutana mwaka 2012. Miaka sita baadaye wakafunga ndoa na wanaripotiwa kuwa na kipato cha Pauni 68 milioni.

7. Bastian Schweinsteiger na Ana Ivanovic, Pauni 85milioni

Kiungo wa zamani wa Bayern Munich na Ujerumani, Bastian Schweinsteiger alifunga ndoa na mkali wa tenisi Ana Ivanovic – ambaye aliwahi kuwa namba moja duniani na kushinda French Open. Wawili hao wote wamevuna pesa zao kupitia michezo, licha ya kuwa na shughuli zao nyingine za kibiashara.

Bastian, ambaye aliwahi kuichezea Manchester United na mrembo Ana, wanaripotiwa kuwa vizuri kiuchumi, wakiwa na kipato kinachofikia Pauni 85 milioni.

6. Robert na Anna Lewandowska, Pauni 104milioni

Robert Lewandowski na mkewe mrembo wa Poland, Anna wote ni wanamichezo. Kila mmoja amefanikiwa kwenye eneo lake, ambapo Robert ni staa maarufu kabisa huko Poland, aliyewahi kuchezea Bayern Munich na sasa anakipiga Barcelona.

Wakati Anna akiwa bingwa wa mchezo wa karate, kwa sasa anapiga pesa kupitia kitabu chake cha masuala ya mapishi, migahawa na blogu ya masuala ya mapishi. Wanandoa hao wanaripotiwa kuwa na utajiri wa Pauni 104 milioni.

5. Sergio Ramos na Pilar Rubio, Pauni 120milioni

Sergio Ramos ni mmoja kati ya wanasoka wenye mafanikio makubwa duniani. Ameshinda karibu kila taji alipokuwa Real Madrid, ambako alikuwa maarufu sana na alishinda pia Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Hispania. Mkewe, mrembo Pilar ni mtangazaji wa televisheni ya Hispania. Walianza kuwa pamoja 2012, kabla ya kufunga ndoa mwaka 2019 na wamepata watoto wanne. Familia hiyo ipo vizuri mfukoni, ikiripotiwa kuwa na kipato cha Pauni 120 milioni.

4. Wayne na Coleen Rooney, Pauni 181milioni

Sehemu kubwa ya kipato cha familia ya Wayne Rooney kilivunwa kwa kupitia mishahara na bonasi zake alizokuwa akilipwa kipindi akiwa mchezaji wa Manchester Unuted. Dili zake na kampuni ya viatu ya Adidas na wadhamini wengine walimfanya kuwa na mkwanja mrefu, huku kwa sasa akivuna pesa kwa kazi yake ya ukocha.

Mrembo Coleen naye anapiga pesa kuongezea kitu kwenye familia, kupitia vipindi vyake vya Disney. Familia hiyo inaripotiwa kuwa na kipato cha Pauni 181 milioni.

3. Lionel Messi na Antonella Roccuzzo, Pauni 182milioni

Haina kificho, sehemu kubwa ya kipato cha familia hiyo imechangiwa na mwanasoka Lionel Messi. Supastaa huyo wa Argentina kwa sasa anaripotiwa kuvuna hadi Pauni 16 milioni kwa mwaka huko kwenye klabu ya Inter Miami ya Ligi Kuu England.

Mrembo Antonella ana elimu kuhusu tiba ya meno. Lakini, mwonekano wake bomba umemfanya apate dili nyingi za masuala ya mitindo, akisaini mikataba na wabunifu wa mitindo maarufu kama vile Ricky Sarkany na yeye pia ana mitindo yake.

Kwa pamoja familia hiyo inaripotiwa kuwa na kipato kinachofikia Pauni 182 milioni.

2. Cristiano Ronaldo na Georgina Rodriguez, Pauni 411milioni

Ingekuwa ajabu wangekosekana kwenye tatu bora ya wanafamilia kwenye mchezo wa soka ambao wana mkwanja mrefu. Supastaa Cristiano Ronaldo na mrembo Georgina Rodriguez wanapiga pesa si mchezo.

Supastaa, Ronaldo ni mwanamichezo anayelipwa pesa nyingi zaidi duniani. Mkataba wake huko Al-Nassr unamwingizia Pauni 173 milioni kwa mwaka. Mrembo Georgina, ambaye alikuwa msaidizi wa mauzo kwenye duka la Gucci, anapiga pesa kupitia kipindi cha Netflix cha I Am Georgina –Pea hiyo inatajwa kuwa na kipato kinachofikia Pauni 411 milioni.

1. David na Victoria Beckham, Pauni 412 milioni

Mwimbaji wa zamani wa Kundi la Muziki wa Pop la Spice Girl, Victoria amepiga pesa kabla ya hata kukutana na David Beckham. Pia amepiga pesa kwenye mitindo ya mavazi. Beckham amepiga pesa kupitia soka na filamu, huku akimiliki klabu yake ya soka, Inter Miami ya huko Marekani. Bado ni balozi wa kampuni mbalimbali za mitindo na ana kipindi Netflix kinachoingiza pesa. Familia hiyo ina kipato kinachofikia Pauni 412 milioni.

Chanzo: Mwanaspoti