Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Faini za Lampard zakumbukwa Chelsea

Lampard 1 Frank Lampard

Mon, 10 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Frank Lampard amerudi kuwashika Chelsea na kinachosubiriwa kwa sasa kama ataleta upya zile faini zake alizoweka kwenye kikosi hicho ili kunyoosha nidhamu ya mastaa wake.

Lampard, 44, amekubali kurudi kuinoa Chelsea kwa muda hadi mwisho wa msimu huu baada ya miamba hiyo ya Stamford Bridge kuamua kuachana na aliyekuwa kocha wao mkuu, Graham Potter. Lakini, kiungo huyo gwiji wa zamani wa Chelsea, amerudi Stamford Bridge baada ya awali kufutwa kazi Januari 2021, alipohitimisha miezi yake 18 katika kuinoa timu hiyo.

Katika awamu yake ya kwanza Chelsea, Lampard alikuja na mpango wa kuweka nidhamu kwa mastaa wake kwa kuweka viwango vya faini kulingana na kosa ili kuweka nidhamu sawa kikosini. Faini hizo zilikuja kufutwa na kocha Thomas Tuchel.

Lakini, Lampard anaweza kurudisha faini hizo baada ya kurejea Stamford Bridge ili kuwanyoosha mastaa wake.

Faini kubwa ilikuwa Pauni 20,000 kwa mchezaji atakayechelewa mazoezini. Mchezaji huyo atatoza Pauni 500 kwa kila dakika atakayokuwa amechelewa. Mchezaji aliyechelewa kutoa taarifa ya kwamba anaumwa au ni majeruhi kwa zaidi ta dakika 90 kabla ya mazoezi, atapigwa faini ya Pauni 10,000.

Mchezaji ambaye atashindwa kutoa taarifa ya kwamba hatasafiri na timu wakati wakitoka kwenye mechi ndani ya saa 48 au kushindwa kuhudhuria kwenye mambo ya kijamii, atapigwa faini ya Pauni 5,000 huku Pauni 2,500 itatozwa kwa mchezaji ambaye atachelewa msafara wa timu kwenda kwenye mechi, kuchelewa kuripoti mazoezini au kwenda kufanya vipimo akihitajika kufanya hivyo. Pauni 1,000 ilitozwa kwa mchezaji aliyechelewa kwenda gym, kuvaa jezi isiyostahili au simu yake kuita wakati wa chakula cha pamoja au kwenye vikao vya timu.

Kama mchezaji atashindwa kulipa faini zake kwa wakati ndani ya siku 14, basi itajiongeza mara mbili. Lampard alipoondoshwa na Tuchel kuletwa, Mjerumani huyo alifuta faini zote na kusema: "Mimi sio polisi", ambapo alikuwa na uhakika wachezaji wa kikosi hicho wamepevuka na watasimamia wenyewe nidhamu kwenye timu.

MAVITU YA LAMPARD KATIKA AWAMU YAKE YA KWANZA CHELSEA

-Siku: 571

-Mechi: 84

-Kushinda: 44

-Sare: 15

-Vichapo: 25

-Ushindi: 52.4%

Chanzo: Mwanaspoti