Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Faida na hasara za kufanya mazoezi ufukweni

Beach Faida na hasara za kufanya mazoezi ufukweni

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni kawaida kwa wanasoka au wanamichezo hapa Bongo kuwaona wakijiongeza kwa kufanya mazoezi katika maeneo ya ufukweni wakiamini ni moja ya maeneo mazuri kujenga utimamu wa mwili.

Kujiongeza kwa wachezaji si jambo geni kwani hata mastaa kama Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wamekuwa pia wakifanya mazoezi binafsi hatimaye hupata matokeo mazuri katika viwango na utimamu wa miili yao.

Siri kubwa ya ufanyaji wa mazoezi ya ufukweni kwa wanasoka ni kutokana na mazoezi hayo kuchoma zaidi kiasi kikubwa cha mafuta yaliyorundikana mwilini.

Baadhi ya wachezaji wanaoishi maeneo ya Pwani kama Zanzibar, Dar es Salaam na Tanga hutumia fursa za ufukweni na huwa na eneo kubwa, mchanga mwingi, hewa ya kutosha na utulivu mwingi.

Wanamichezo wengi wa maeneo ya Pwani wamekuwa wakifanya hivyo katika muda wao wa ziada ikiwamo siku ambazo hawana mazoezi ya klabu au wakati ambao hawana mechi yoyote.

Si hapa Bongo tu hata Brazil ni mojawapo kati ya nchi ambayo wanasoka wengi hutumia utamaduni wa wakucheza soka la ufukweni kama njia ya kujenga utimamu wa miili yao.

Uchanganyaji wa mazoezi ya kukimbia ufukweni pamoja na kuogelea baharini yana faida kubwa kwa mchezaji mmoja mmoja kwani anapata utimamu bora wa mwili na hatimaye kulinda kiwango chake.

Ufanyaji wa mazoezi ufukweni ni moja kati ya mbinu ambazo zinatumiwa sana na wanasoka wengi wa maeneo ya Pwani kama utamaduni kwa ajili kujiburudisha na kutengeneza utimamu wa miili yao.

Leo nitawapa ufahamu wa faida na hasara za kufanya mazoezi ufukweni kwa wanasoka.

FAIDA YA MAZOEZI HAYO

Zoezi hili humfanya mchezaji kuchoma kiasi kikubwa cha sukari (mafuta) ya mwilini ambapo wakati anakimbia au anacheza soka misuli ya miguu hutumia nguvu nyingi kukimbia na kucheza.

Ufukweni kuna mchanga mwingi sana wakati wa kukimbia miguu huzama katika rundo la mchanga, hivyo kuipunguza kasi na kuhitaji kutumia nguvu kuinyanyua tena ile kupiga hatua na kikimbia.

Hali hii ndiyo inayochangia mwili kutumia nguvu nyingi sana ili kucheza na kukimbia na hivyo kumfanya mchezaji kupunguza uzito na hatimaye kuwa mwepesi.

Vilevile mchezaji anapokuja katika uwanja wa kawaida huwa na wepesi na kuweza kujiamini kiasi cha kutosha na kutohisi kuchoka kutokana na mazoea ya mwili na akili kutumia nguvu ufukweni.

Faida ya pili ni kuimarisha na kujenga misuli ya miguu, mchezaji soka yeyote uimara wa miguu yake ndiyo kila kitu kwani ndiyo huitumia kucheza soka.

Zoezi la ufukweni huifanya misuli ya miguuni kutumia kiasi kikubwa cha sukari ili kukunjuka na kuweza kuutembeza mwili wakati wa kukimbia na hatimaye huifanya kuwa mikakamavu na kujengeka.

Hali hii pia husaidia kuifanya misuli ya miguu kuwa imara na kuhimili majeraha yatakanayo na michezo huku pale mchezaji anapoumia anaweza kupona haraka na kwa wakati.

Kutokana na kukaa sana bila mazoezi misuli na maungio huweza kuwa na uchovu, hivyo kushindwa kuwajibika kwa ufanisi wakati wa kucheza. Unapofanya mazoezi haya husaidia kulainisha viungo na kuwa vyepesi.

Kutokana na upana wa eneo la ufukweni na kuwa wazi huku likisindikizwa na upepo mwanana uliosheheni hewa safi yenye oksijeni humfanya mchezaji anayefanya mazoezi kupata hewa ya kutosha.

Hii huwa na faida kwa moyo na mzunguko wa damu na mwili kuweza kupata hewa ya oksijeni kwa wingi.

Hali ya ufukweni huweza kumpa burudani mchezaji na kusahau mambo yanayompa msongo wa mawazo ikiwamo hofu ya yeye binafsi, ndugu, jamaa au wazazi.

Ufukwe ni eneo la burudani na hata wanasaikolojia wanashauri kwa mtu mwenye shinikizo la akili au msongo wa mawazo kwenda ufukweni kwani wanaamini mazingira hayo husaidia kupeperusha hasira, huzuni, msongo wa mawazo na shinikizo la akili.

Baadaye mwanasoka anapomaliza mazoezi ya ufukweni na kuamua kuogelea ndipo huzidi kupata utimamu na wepesi kwenye maeneo mengine ya mwili.

Hii ni kwasababu zoezi la kuogelea linashika namba moja kuimarisha kujenga maeneo mengi ya mwili kutokana na zoezi hili kuhusisha misuli mingi ya mwili.

Hivyo mchezaji hupata kasi na wepesi na misuli huwa imara na yenye nguvu anapochanganya mazoezi ya ufukweni na kuogelea.

HASARA ZAKE

Mchezaji anayecheza peku peku maeneo hayo anaweza kupata majeraha ya nyayoni kutokana na uwepo wa vitu vyenye nchi kali ikiwamo nyumba za konokono au mazao mengine ya baharini na miba ya samaki na vitu kama chupa zilizotupwa kiholela.

Kutokana na kuwepo kwa mchanga mwingi unaozamisha eneo la chini la miguuni mchezaji anaweza kupata majeraha ya kifundo cha mguu na magoti.

Kwakuwa mazoezi haya huupa ugumu mwingi sana mwili pale atakapoyafanya kupita kiasi bila kujipa mapumziko anaweza kujipa uchovu na majeraha.

Upepo mkali unaweza kuwa chanzo cha kupata mafua ya muda na vilevile mchanga unaorushwa machoni unaweza kukereketa.

CHUKUA HII

Usifanye mazoezi ya ufukweni kiholela kwani pamoja na hasara hizi chache lakini kuna faida ya kufanya mazoezi katika eneo hilo.

Ni vizuri mchezaji anayefanya mazoezi ufukweni apate ushauri kutoka kwa wataalamu wa mazoezi ya mwili ambao watamshauri kutokana na ufahamu zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti