Beki kisiki wa timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' na Klabu ya Simba ya Tanzania, Joash Onyango amefunguka kuhusu mambo mbalimbali ya maisha yake.
Akifanya mahojiano maalum na Wasafi Media, Onyangi ameweka wazi kwamba kando na kucheza kabumbu yeye pia ana mwanafamilia tena kwa ndoa, na kwamba tayari yeye na mkewe wana watoto wawili.
"Mimi niko katika ndoa, nimebarikiwa na mabinti wawili. Wa kwanza ana miaka mitano na wa pili ana mwaka mmoja" Joash alisema.
Joash alisema anaipenda na kuithamini familia yake sana na anaamini kuwa mkewe anaendelea kuwatunza mabinti wao vizuri.
Beki huyo ambaye alihitimu miaka 31 mnamo Jumatatu pia alifichua kuwa yeye sio shabiki mkubwa wa wanamuziki wa hapa nchini. Hata hivyo alisema anamshabikia Otile Brown na msanii mwenzake kutoka Bongo Ali Kiba.
"Hata kama huwa siwashabiki wanamuziki wa huko sana, nampenda Otile Brown. Mimi ni shabiki wa Alikiba, yeye ni mtu mtulivu, anatia bidii. Jinsi huwa anajiendeleza na muziki wake, huwa hana haraka, nampendea hayo" Alisema.