Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu sababu za mwamuzi huyu kupewa Simba vs Yanga

Jonesia Rukyaaa Fahamu sababu za mwamuzi huyu kupewa Simba vs Yanga

Fri, 18 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii ya watani wa jadi, Simba na Yanga jijini Tanga, imeibua malalamiko kwa waamuzi wananyooshewa kidole, wakidaiwa kutomudu mchezo.

Hoja zinazotawala malalamiko ni pamoja na mtokea benchi Kibu Denis kudaiwa kunyimwa penalti dakika chache kabla ya filimbi ya mwisho ya Refa Jonesia Rukyaa. Kiungo mkabaji Mganga Khalid Aucho anatajwa kumkwatua Kibu ndani ya boksi la Yanga.

Beki wa Kati wa Yanga, Ibrahim Abdallah Hamad, maarufu Bacca, pia anadaiwa kumpiga konzi kisogoni mshambuliaji Jean Baleke. Hivyo, kumekuwa na madai kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa Sheria Na. 12 ya Soka (Faulo na Tabia Mbaya), lakini Refa Rukyaa na wasaidizi wake hawakuchukua hatua stahiki. 

Hoja iliyoteka zaidi malalamiko hayo, ni madai kwamba Kipa wa Simba, Ally Salim Katoro, alikiuka Sheria Na. 14 ya Soka (Pigo la Penalti) wakati wa 'matuta', dakika 90 zilipotimu huku timu hizo zikiwa hazijafungana. 

Sheria inasema "...wakati wa pigo la penalti, walau mguu mmoja wa kipa uwe umegusa mstari wa goli au uko juu ya mstari huo", lakini kumekuwa na madai kwamba Kipa Salim wa Simba alikiuka hilo pasi na waamuzi wa mechi kuchukua hatua.

Vilevile, kuna madai kwamba Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ilimteua Refa Jonesia kusimamia mechi hiyo ilhali amefeli mtihani wa utimamu wa mwili wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, FIFA.

BOSI WA MAREFA  

Katika mazungumzo maalum na Nipashe kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Nassor Hamduni, alisema hawajapata malalamiko rasmi ofisini kutoka kwa klabu zote mbili kuhusu mechi hiyo. Hata hivyo, klabu kulalamikia au kupongeza uchezeshaji wa mwamuzi ni kosa kikanuni. 

Hamduni, refa mstaafu aliyekuwa miongoni mwa waamuzi bora nchini mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, pia aliiambia Nipashe kwamba hadi juzi jioni, walikuwa hawajapata ripoti ya mechi hiyo kutoka kwa wasimamizi wa mashindano.

Alisema kuwa licha ya kutopata malalamiko rasmi, wao kama wadau wa soka wamesikia malalamiko dhidi ya marefa waliochezesha mechi nne za Ngao ya Jamii na watayafanyia kazi, haijalishi watapata ripoti rasmi kutoka kwa wasimamizi wa mashindano au la. Watawaita waamuzi na kuwakumbusha majukumu yao wanayopaswa kuyafanya wakiwa uwanjani.

"Ni kweli kwenye mechi za Ngao ya Jamii kulikuwa na malalamiko kutoka kwa wadau kwamba kuna makosa yaliyojitokeza, lakini Kamati ya Waamuzi kazi yake kubwa ni kuwaita, kuwaelimisha na kuhakikisha wanapata elimu tosha na kuwa fiti wakiwa uwanjani.

"Sisi kama kamati tunawapanga waamuzi na kule wanakokwenda kuna wadau ambao wanasimamia mashindano. Sisi hatujapata malalamiko rasmi kutoka klabu zote ila tunayasikia. 

"Kama yatafika mezani kwangu na kuthibitika kuwa ni kweli, tutachukua hatua au kuendelea kuwaelimisha, lakini mpaka sasa hakuna malalamiko yoyote (rasmi). Tunayasikia na tunayasubiri yaletwe rasmi. Tunawasubiri pia wahusika wa mashindano watatuletea taarifa rasmi yapi yaliyojitokeza na yapi ya kuboresha," alifafanua Hamduni.

MTIHANI WA FIFA

Kuhusu madai kwamba Refa Jonesia alifeli mtihani wa utimamu wa mwili, Mwenyekiti huyo alikiri yana ukweli, lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), lilimtaka kurudia mtihani huo ndani ya wiki sita, wao wakamtaka kurudia ndani ya wiki moja, akafaulu. Jina lake litawasilishwa ngazi za juu ili kupatiwa beji ya FIFA kwa kuwa amekidhi vigezo vinavyotakiwa.

"Jonesia ni mmoja wa waamuzi zaidi ya kumi tulionao ambao wapo katika michuano ya kimataifa na orodha ya waamuzi wa FIFA.

"Awamu ya kwanza tulifanya kozi kwa ajili ya waamuzi wa kimataifa na wengine kwa ajili ya kuwaombea nafasi ili mwakani waendelee kuwa waamuzi ya kimataifa na kweli (Jonesia) hakumaliza mbio zake vizuri kutokana na matatizo mbalimbali, lakini utaratibu wa CAF ni kwamba mwamuzi yeyote wa kimataifa ambaye hakufanya vizuri anapewa nafasi ya kurudia ndani ya wiki sita.

"Sisi kama Kamati ya Waamuzi tuliwaomba waamuzi walioshindwa kufanya vizuri warudie baada ya wiki moja, walirudia na walifanya vizuri. Hata shuleni na vyuoni mwanafunzi anaweza kukosa somo moja, akarudia na akifaulu huwezi kusema alifeli mwanzo. Hivyo, mwamuzi huyo alirudia na kufaulu vizuri zaidi.

"Mwamuzi Jonesia hatuna shaka na uwezo wake. Wadau wa soka wanamfahamu kuwa mmoja wa marefa wazuri na taifa halina shaka na uwezo alionao isipokuwa ni changamoto tu zinazojitokeza kama mwanadamu," alisema.

SABABU KUPEWA 'DABI'

Hamduni alisema Refa Jonesia aliteuliwa kusimamia mechi hiyo ya fainali ya Ngao ya Jamii kwa kuwa ndiye Mwamuzi Bora wa Msimu Uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kanuni inawaelekeza kuwa atakayekuwa bora msimu uliopita ndiye anayepewa kuchezesha mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii.

"Na kwa nini tulimpanga? Kwenye Ngao ya Jamii ndiyo mwanzo sahihi wa ligi kuanza na kanuni zinatueleza kwamba mwamuzi aliye bora msimu uliopita ndiye anatakiwa atufungulie ligi ili kuonesha mfano.

"Ninampongeza sana ameonyesha mfano mzuri kwenye mechi ya fainali japo kuna upungufu ambao wadau wa soka wametaja, lakini tunasubiri wasimamizi watupatie ripoti. Kama kuna upungufu, basi tutakaa naye na kuzungumza, baada ya wiki sita atakwenda kuchezesha soka nje ya nchi," alisema.

Alisema kuwa katika msimu huu wa Ligi Kuu ambo mechi zake zilianza jana, kamati imeandaa vema waamuzi kwa kuwapa mafunzo na kuhakikisha wameiva kwenye nyanja zote ikiwamo utimamu wa mwili, "kama yakitokea makosa, basi wakati mwingine yanakuwa ya mwamuzi mwenyewe".

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, dakika 90 ziliisha kwa suluhu, lakini Simba ilitwaa Ngao ya Jamii kwa mikwaju ya penalti 3-1 dhidi ya wapinzani wao wa jadi Yanga waliokuwa wamehodhi ngao hiyo kwa misimu miwili.

Aliwahakikisha wadau wa soka kuwa wamefanya kila kitu kuhakikisha msimu wa 2023/24 ligi inachezeshwa kwa uangalifu wa hali ya juu, viwango na ubora huku akiahidi kutofumbia macho waamuzi wote watakaovurunda.

"TFF kupitia kamati yake ya waamuzi ambayo mwenyekiti wake ni mimi, tumejiandaa vizuri na ligi, na kujiandaa kwetu ni kuwa na mafunzo. Tulianza na mafunzo ya kwanza Julai 31 kwa waamuzi zaidi ya 35 wanaohusika zaidi na beji ya FIFA.

"Tukapata tena waamuzi 190 kwa ajili ya Ligi Kuu na Ligi ya Championship (Ligi Daraja la Kwanza) na sasa tunaendelea na waamuzi zaidi ya 350 kwa ajili ya ligi zingine za chini," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: