Imefahamika kuwa, Kocha wa Klabu ya Marumo Gallants, Dylan Kerr alikaa jukwaani kwenye mchezo wa jana dhidi ya Yanga Sc kwa sababu hana vibali vya kufanya kazi nchini Afrika Kusini.
Hayo yamefahamika baada ya wadau wa soka kuhoji kwa nini kocha huyo alikuwa jukwaani badala ya kukaa kwenye benchi la ufundi wakati timu yake ikipoteza katika dimba la Mkapa kwa bao 2-0 katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kikosi hicho kilisimamiwa na kocha msaidizi, Raymond Mdaka wakati Kerr akitoa maelekezo kutokea jukwaani jambo ambalo amesema lilikuwa gumu kwake kwani wachezaji walishindwa kufuata maelekezo yake kwa vile alikuwa mbali nao tofauti na angekuwa pale kwenye benchi.
Kocha huyo tangu asajiliwe na Marumo mwanzo mwa Machi, 2023 hajawahi kukaa kwenye benchi la timu hiyo licha ya kufanya vizuri na kuibadilisha timu yake aliyoikuta ikishika mkia kwenye ligi na sasa ipo nusu fainali ya Shirikisho.
“Nina vibali vitano vya kazi kwenye passport yangu, nipo kwenye mfumo tayari, kwa nini inachukua muda mrefu kupewa kibali cha kufanya kazi hapa nchini.
“Nimefanya taratibu zote, nimefuata sheria, lakini Romain Folz wa AmaZulu amepata kibali ndani ya siku nne tu, mimi mpaka leo ninasubiri, kuna tatizo gani?,” amehoji Kerr wakati akizungumza na vyombo vya habari vya nchini Afrika Kusini.