Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu! Kanuni ya 17 ya FIFA ni muhimu katika uhamisho wa wachezaji

Fei Toto Fei Toto

Sat, 14 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kakita baadhi ya makala zangu za mwaka uliopita niliandika juu ya umuhimu wa wanamichezo kuwa na menejimenti za uhakika kama njia ya kuwaletea mafanikio.

Mara nyingi sipendi kuandika kuhusu matukio ya uwanjani au hata kwenye bodi za vilabu na mashirikisho. Napenda kuandika kuhusu mifumo,sera na maendeleo ya michezo.

Hata hivyo,nimelazimika ‘kufuata upepo’ kwa kuandika masuala yanayohusu usajili yakiwa ni masaa machache kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili. Inafika mahali matukio na wakati havikwepeki kuongelewa ikiwa kweli lengo ni kuleta maendeleo.

Nadharia inadhihirika na kupimika kutokana na matukio.Nikiri wazi kuwa sakata la mvutano kati ya mchezaji Feisal Salum na klabu yake ya Yanga kufuatia kile kilichoitwa jaribio la mchezaji kuvunja mkataba au kununua mkataba bila kushirikisha upande wa pili limechangia kwa kiasi Fulani uamuzi wa kuandika makala hii.

Suala la Feisal Salum

Mnamo Desemba mwaka jana kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' aliandika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii uliosomeka kama mchezaji anayeaga baadaya kumaliza mkataba au kumaliza uhamisho kwenda klabu nyingine.

Baada ya hapo klabu ilitangaza mchezaji kutoweka kambini na hivyo kutoshiriki katika mchezo uliokuwa unafuata ambao ulikuwa ni mchezo wa marudiano wa ligi kuu dhidi ya Azam FC.

Baada ya hapo mchezaji alionekana kwenye mitandao ya kijamii akicheza mechi za kirafiki huko Zanzibar akiwa na klabu yake ya zamani JKU na baadaye akaonekana akiwa Dubai anafanya mazoezi na wakufunzi binafsi.

Huku Dar Es Salaam, klabu yake ikatoa tamko kwamba mchezaji huyo aliyekuwa na mkataba wa kuichezea mpaka 2024 alifanya jaribio la kuvunja mkataba kwa kuweka kiasi cha shilingi milioni 100? Kwenye akaunti ya klabu lakini klabu ikamrudishia ikidai hakufuata utaratibu na bado alikuwa mchezaji wa klabu hiyo ya Jangwani.

Kilichofuata ni klabu kupeleka malalamiko kwenye shirikisho la mpira wa miguu kupitia kamati ya sharia na hadhi za wachezaji nayo ikatoa hukumu kwamba Feisal bado ni mchezaji wa Yanga.

Hukumu hiyo haikuwashangaza wengi wanaojua taratibu za ajira ya mpira wa miguu duniani. Hata hivyo wako walio wengi waliolalamika kwamba mchezaji alipaswa kuachiwa kwenda anakotaka ili apate maslahi yake au achezee klabu aliyo na mahaba naye kama alivyosema mwakilishi wa mchezaji.

Wengi nadhani hata menejimenti na wakala wa mchezaji waliamini kwamba uwepo wa kifungu cha kununua mkataba huo, ambao sijui uliandikwa kwa Kiswahili au Kiingereza, ilikuwa ni RUKSA tosha kwa mchezaji kuondoka wakati wowote anaotaka.

Labda kwa uhakika waliokuwa nao, haitashangaza kusikia kwamba mchezaji alivunja kibubu au alipata mkopo wa wahisani kwa vile alikuwa na uhakika kuwa pesa ikishaingia kwenye akaunti basi yeye atakuwa ni mchezaji huru.

Kwamba mchezaji anayedai kupata maslahi kidogo katika mpira wa Tanzania ana uwezo wa kuwa na akiba ya zaidi ya milioni 100 ya kulipa ili aachane na klabu ambayo ameichoka nalo linatuacha na maswali lakini kwa leo sio mahala pake kulijadili.

Maamuzi ya kamati ya TFF hayakushangaza kwa sababu ndivyo ukweli ulivyo kwamba mifumo yote ya usajili yaani ya TFF, CAF na FIFA yote inasoma kwamba Feisal anaruhusiwa kuichezea Yanga na sio timu nyingine labda Zanzibar Heroes na Taifa Stars.

Ukweli mwingine ulio wazi ni kwamba kamati ilikaa kushughulikia malalamiko au mashtaka dhidi ya mchezaji na siyo mchezaji dhidi ya klabu. Hivyo basi, mchezaji alikwenda kama mshtakiwa.

Feisal hakuwahi kulalamikia matendo au makosa ya Yanga dhidi yake kupitia vyombo sahihi. Feisal, labda pamoja na menejimenti yake walitumia muda wote wa mvutano kutoa kauli na picha kwenye mitandao ambayo inatafsiriwa kwamba mchezaji alimkimbia mwajiri bila sababu ya msingi.

Kwa maamuzi ya kamati sasa mchezaji anabaki na machaguo mawili yaani kurudi kutumikia klabu yake au kukata rufaa dhidi ya maamuzi hayo.

Ibara ya 17 ya Kanuni za Fifa za uhamisho wa wachezaji

Ibara hii, ambayo pia huitwa ‘kanuni ya Webster’ inashughulika na matokeo ya mchezaji kuvunja mkataba wa ajira na klabu bila sababu za msingi za kufanya hivyo.

Kanuni hii inaruhusu mchezaji aliyeingia mkataba na timu kabla ya kufikisha miaka 28 kununua mkataba wake baada ya kuutumikia kwa miaka miwili.Mwisho wa siku lazima taratibu za kuachana kati ya mchezaji na klabu zifuatwe.

Kanuni hii imewahi kutumiwa na wachezaji sehemu mbalimbali na kufanikisha kuvunja au kununua mikataba yao.Pia kuna waliojaribu kuitumia lakini wakashindwa kufanikiwa kununua mikataba yao.

Kifungu cha mchezaji kununua mkataba huwa hakisimami peke yake. Kimsingi mkataba hununuliwa na klabu anayokwenda mchezaji kwani baada ya kutimizwa vigezo na masharti ya klabu inayouza, pesa huwekwa na mnunuzi kwenye akaunti ya mchezaji na kisha yeye kutuma kwenye akaunti ya klabu inayomuuza.

Vigezo na masharti vinaweza kuwa vingi zaidi ya pesa. Mara nyingi klabu hukataa kumwachia mchezaji msimu wa mashindano ukiwa unaendelea au kwa klabu wanayoshiriki mashindano pamoja hata kama klabu inayomtaka imefikia kiwango cha pesa kilicho kwenye kifungu cha kununua mkataba.

Mkataba wa mchezaji ni muhimu ukasomwa kifungu kwa kifungu na kueleweka kwa mchezaji na menejimenti yake; hii ni pamoja na kuelewa kanuni za kimataifa na za ndani kuhusu uhamisho na mikataba ya wachezaji.

Mikataba ya mpira inaweza kuwa na vifungu vingi kama vya bonasi kutokana na mafanikio ya mchezaji au timu,malipo kwa timu ya zamani mchezaji anapouzwa, nafasi ya timu ya zamani kumnunua tena na hata vingine unavyoweza kuita vya kipuuzi. Hiyo yote ni kazi ya menejimenti ya mchezaji kuelewa na kuhakikisha wanatenda kwa mujibu wa mkataba.

Menejimenti ya mchezaji ni kinga yake ili asifikwe na mitetemo ya kiutawala, kibiashara, kisheria n.k . Mchezaji anapokuwa na menejimenti nzuri basi yeye hujikita katika masuala ya uwanjani.

Upande wa pili klabu zinatakiwa kuwa na mifumo inayoweza kulinda vizuri maslahi ya klabu na wakati huo ikilinda haki na maslahi ya waajiriwa wa klabu. Uongozi wa klabu za mpira wa miguu unatakiwa kuelewa vema taratibu za uendeshaji mpira kimataifa siyo kukurupuka tu na kutaka kuvunja mkataba kiholela na mchezaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live