Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fadlu, kuna shabiki wa Simba na kuna shabiki wa Arsenal

Simba Vs Fadlu Fadlu, kuna shabiki wa Simba na kuna shabiki wa Arsenal

Mon, 5 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kama ukinipa dakika mbili za kuongea na kocha mpya wa Simba, Fadlu Davids kutoka Afrika Kusini nitamwambia ukweli mchungu unaoweza kumshangaza. Kwamba kuna shabiki wa Simba halafu huyo huyo ni shabiki wa Arsenal na wanaishi dunia mbili tofauti.

Kwamba kuna shabiki wa Simba halafu huyo huyo ni shabiki wa Arsenal, lakini kuna wakati wanakuwa wanadamu tofauti huku wakitumia kichwa kimoja na moyo mmoja. Wana mishipa ya damu ile ile na wana moyo ule ule lakini viungo vyao vinafanya kazi tofauti pale wanapoizungumzia Simba na wanapoizungumzia Arsenal.

Kuna shabiki wa Simba ambaye huyo huyo pale Ulaya anashabikia Manchester United lakini hao ni mashabiki wawili tofauti katika mwili mmoja. Kuna shabiki wa Simba halafu huyo huyo anashabikia Liverpool lakini ni mashabiki wawili tofauti hata hivyo mwili wao ni mmoja.

Nililitazama pambano la Simba na APR juzi kwenye Uwanja wa Mkapa nikajikuta natafakari kauli hii pamoja na kazi ambayo inamkabili kocha wa Simba rafiki yetu kutoka Afrika Kusini. Ana kazi kubwa ya kufanya mbele yake licha ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya APR pale Temeke.

Tuanzie wapi? Shabiki wa Simba na Arsenal. Huyu wa Simba na Arsenal ana sura mbili tofauti. Kwa misimu miwili ambayo Arsenal wamekosa ubingwa wa England, huku wakiunusa puani bado ameendelea kuwa mfuasi mtiifu wa Mikel Arteta. Anaamini kwamba Arsenal wanakaribia ubingwa wa England. Anajua kazi ya kumtoa Pep Guardiola pale alipo inahitaji akili na nguvu.

Huyu shabiki wa Simba na Arsenal anaelewa wazi mwelekeo wa Arsenal. Jaribu kufikiria kama Simba ingekuwa inakosa ubingwa puani kabisa mwa Yanga. Unadhani angeelewa? Thubutu. Kocha Fadlu angejikuta pabaya kwake. Angeona wazi kocha hana uwezo wa kumfukuza Gamondi na kuchukua taji.

Mpira wa Ulaya huwa tunaelewa malengo yao. Tunajua kazi ngumu aliyoifanya Arteta kutoka kuirudisha Arsenal katika Top 4 hadi kuwania ubingwa na kuukosa kwa karibu mbele ya Pep Guardiola na Manchester City. Shabiki huyu huyu wa Simba na Arsenal haujamsikia akisema 'Arteta out'. Nadhani anaelewa mchakato.

Ni sawa na shabiki wa Manchester United. Anajua namna ambavyo United haiwezi kuchukua ubingwa wa England msimu ujao. Anajua kazi ngumu kwa Erik Ten Hag ni kuirudisha Manchester United katika Top 4. Na wakati shabiki huyu hafikirii sana kuchukua ubingwa bado anawaza sana namna hata ya kuifikia Arsenal kiuchezaji kiasi cha kufikia vijana wa Mikel Arteta katika kusaka mbio za ubingwa.

Shabiki huyu huyu wa Simba hawazi hivyo linapokuja suala la mpira wa nyumbani. Mpira wa nyumbani unataka matokeo ya moja kwa moja. Papo kwa papo. Jaribu kufikiria namna ambavyo kwa sasa Simba inaundwa upya. Hata hivyo, kuna mashabiki wa Simba waliguna katika kipindi cha kwanza tu cha pambano la APR juzi. Hawakuridhishwa na kiwango cha timu yao.

Hadi kipindi cha pili wakati Simba waliporekebisha mambo ndipo walau mashabiki walianza kupumua. Hadi pale Deborah Mavambo na Edwin Balua walipofunga mabao yao ndipo Fadlu alipoweza kushusha pumzi. Fadlu ana wakati mgumu. Inaweza kuwa ameitoa Simba ambako hakujulikana na ilikuwa imeshika nafasi ya tatu msimu uliopita, lakini haitakuwa msamaha kwake kama itashika nafasi ya pili msimu huu unaoanza karibuni.

Kinachohitajika kwake ni kitu ambachi kinaitwa 'Big Results Now'. Kwa lugha yetu ni 'matokeo makubwa kwa sasa'. Ili mradi wamesajiliwa wachezaji ambao wamewapendeza mabosi wa timu pamoja na mashabiki basi kinachohitajika ni matokeo makubwa kwa sasa. Matokeo hayo yanaanza kwa namna yoyote ile ili mradi kuifikia Yanga ilipo.

Kwanza kuna kuifunga Yanga yenyewe. Msimu uliopita Yanga waliinyanyasa Simba vilivyo ikiwemo kupata matokeo makubwa zaidi ambayo wamewahi kuyapata dhidi ya Simba kwa mipngo kama sita iliyopita. 5-1. Na pambano la marudiano la Ligi lilipowasili kila mtu akajua Simba inaenda kufungwa tena na bado ikafungwa kweli.

Fadlu ana kibarua hiki cha kufuta uteja wikiendi ijayo. Baada ya hapo, hata kama Simba wakifungwa atakuwa na kibarua cha kurudisha taji la Ligi kuu. Halafu kuchukua FA. Halafu zaidi kufika fainali za Shirikisho. Ujinga wetu ni ushindani wetu uliopo baina yetu. Kwamba kama Yanga alifika fainali za Shirikisho basi na Simba lazima afike.

Shirikisho ilikuwa michuano iliyodharauliwa baada ya Simba kufika robo fainali za Ligi ya mabingwa mara nne mfululizo. Ghafla Yanga akaingia na kutinga fainali. Ina maana kipimo kwa sasa ni kufika fainali kama ambavyo Yanga alipotinga makundi kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi kupita michuano ya Ligi ya Mabingwa ghafla kipimo kikawa kutinga robo fainali kama Simba wanavyofanya kila mara. Bahati Simba walifaulu.

Na sasa mtihani umeangukia Simba na umeangukia kwa Fadlu. Yeye ndiye amepewa mzigo huo. Analazimika kuifanya kazi hiyo hili kuendelea kutengeneza taswira kwa mashabiki wa Simba kwamba chochote ambacho Yanga anaweza kufanya basi Simba anaweza kufanya zaidi hasa katika michuano ya kimataifa. Kazi anayo.

Vinginevyo Fadlu ana vyakula vingi mezani. Kama akirudisha taji la Ligi Kuu halafu akashindwa kufika fainali za Shirikisho bado mashabiki na mabosi wa Simba watafarijika. Ukizingatia kwa kutofanya hivyo Yanga atakuwa anaenda kuchukua taji hilo kwa mara nne mfululizo bado itakuwa habari mbaya kwa Simba.

Kama alichukua Kombe la Shirikisho na akakosa ubingwa mwingine wowote nchini bado atakuwa na nafasi kubwa katika mioyo ya mashabiki wa Simba popote walipo. Walau jina la 'Wa kimataifa' litakuwa limebeba tafsiri halisi kuliko hali ilivyo sasa.

Mwisho wa siku ujumbe kwa Fadlu ni mmoja tu. Atakuwa amesikia minong'ono mingi kwamba Simba wanajenga timu mpya. Atakuwa amesikia maneno mengi Simba imeingiza wachezaji wengi kwa mkupuo na imeondoa wachezaji wengi. Hasisikilize maneno hayo. Haina maana itakuwa sababu ya kumpa muda ya kuifanya kazi yake sawa sawa. Hana muda huo.

Kinachotakiwa ni matokeo ya haraka na kuifanya Simba isimame juu ya Yanga. Kitu kingine nyuma ya hayo sioni kama kutakuwa na uvumilivu kwake. Imewahi kutokea mara nyingi kwa makocha wengi nchini. Tunahitaji matokeo ya haraka na ni lazima yapatikane. Kinyume cha hapo Juma Mgunda anaweza kuwa anapasha misuli yake nje ya uwanja.

Utasikia tu mashabiki wachambuzi wanaanza kusema ile kauli maarufu ya "wachezaji wamemzidi kocha uwezo". Kama vile wote wanafanya kazi moja. Ukichelewa sana yanaanza mambo ya kurushiana mawe na chupa wakati kocha anaelekea vyumba vya kubadilishia nguo.

Tukiwa tunashabikia Arsenal au Manchester United huwa tunaelewa mchakato wa timu. Tukiwa tunashabikia timu zetu huwa tunapotelewa na fahamu. Sijui ni kwa sababu mawe yetu yanaweza kuwafikia makocha na mabosi au sijui kwa sababu tunaona tunazimiliki hizi timu zetu kuliko hizo za wazungu. Sijui.

Chanzo: Mwanaspoti