Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fadlu ataka ushindi kila mechi

Fadlu Davids Misriii Fadlu ataka ushindi kila mechi

Wed, 31 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati kikosi cha wachezaji wa Simba kikikutua nchini leo kikitokea Misri ambako kiliweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa mashindano, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids, amesema kikosi chake kimeiva na lengo sasa ni kupata ushindi kila mechi watakayocheza.

Hata hivyo, wakati kocha huyo raia wa Afrika Kusini akisema hayo, Balozi wa Tanzania nchini Misri, Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, amesema katika mechi zote tatu alizoangalia, wachezaji wa Simba wamekuwa wakisakata kandanda la hali ya juu na la burudani kwa mpenda soka yoyote angependa kuwaangalia.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo uliochezwa juzi usiku Uwanja wa New Suez Canal, dhidi Al-Adalah FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Saudi Arabia, kocha huyo alisema ingawa bado hajafika mwisho wa kukinoa kikosi hicho, lakini mwanga unaonekana na vitu vingine vimekwenda kama vilivyopangwa na kuahidi kumalizia mambo machache tu ya kiufundi yaliyobaki.

"Tumemaliza 'pre season' vizuri, bila kuzalisha majeruhi wengi, isipokuwa Kagoma (Yusuph), nadhani wiki ijayo atarejea ni yeye pekee ndiyo nilimkosa kwa wiki mbili, kila kitu hivi sasa kipo vizuri kwa maana ya dakika za kucheza, kila mchezaji amepata dakika kadhaa za kuwa uwanjani, tumepata matokeo leo (juzi) na mechi zote zilizochezwa, ila siyo muhimu sana kwetu, zaidi ilikuwa ni kuangalia namna gani ya kuzuia, kulinda na kushambulia.

"Tayari huko tumeshamaliza, hii wiki ya tatu iliyobaki ni ya kutazama mbinu na ufundi uwanjani, hapa napaswa kuingiza vitu hatua kwa hatua ndani ya kikosi hiki wachezaji waelewe zaidi, lengo mama ni kushinda kila mechi iliyo mbele yetu," alisema kocha huyo.

Katika mechi hiyo, Simba ilishinda mabao 2-1, yaliyowekwa wavuni na Steve Mukwala na Joshua Mutale, ambao wote ni wachezaji wapya katika kikosi hicho. "Kocha huyo alisema kambi ya nchini Misri imemsaidia vitu vingi, kukaa na kufahamiana na wachezaji, pamoja na kufanya mazoezi kwa uhuru na utulivu.

"Kuna vitu vingi tumevifanya na tumevimaliza katika kambi hii, tunajua wiki ijayo ni wiki ambayo tutakwenda kwenye Simba Day ambayo ni siku ya kwenda kuwatambulisha wachezaji mbele ya mashabiki wao," alisema.

Kwa upande wa Balozi Makanzo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mechi zote tatu ilizocheza, aliwataka wachezaji kwenda kucheza soka kama walilolionyesha nchini humo.

"Nawashukuru Simba kwa kuweka kambi nchini Misri na nimefarijika kwa ujio wenu, niwatakie safari njema, nimeona maandalizi ni mazuri, vijana wanacheza vizuri sana, na timu mlizocheza nazo nimeziona ni ngumu na nzuri, lakini vijana hawa wanacheza soka safi mtu hadi unapenda kukaa kuwaangalia, ni burudani kwa kweli, nawatakia msimu bora," alisema.

Simba imecheza mechi tatu ikiwa huko, ya kwanza ni dhidi ya Canal FC, ikishinda mabao 3-0 yaliyofungwa na Jean Charles Ajoua (mawili) na Augustine Okejepha, wachezaji wapya wa timu hiyo, huku ya pili ikicheza dhidi ya Telecom Egypt na kushinda mabao 2-0, yakifungwa na Mashaka Valentino na Ladack Chasambi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live