Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

FIFA yazibeba Simba, Yanga CAF

Simba X Yanga CAF FIFA yazibeba Simba, Yanga CAF

Thu, 14 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uwepo wa mechi za kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA, ni kama imewarahisishia kazi Simba na Yanga katika maandalizi ya mechi za robo fainali kutokana na wapinzani wao Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Al Ahly ya Misri kuitwa asilimia kubwa ya kikosi cha kwanza kabla ya kuja kuvifuata vigogo hivyo.

Yanga imepangwa kukutana na Mamelodi katika mechi za robo fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Simba ikipewa Al Ahly na timu hizo zimetoa wachezaji walioitwa timu za taifa, lakini kalenda hizo za FIFA na ratiba ya mechi za nyumbani zinawabeba zaidi Simba na Yanga kuliko wapinzani wao watakaocheza ugenini mechi za kwanza.

Ipo hivi. Wakati Yanga ikitoa wachezaji sita hadi sasa katika vikosi vya timu za taifa, wenzao Mamelodi wamechukuliwa wachezaji 10 ili kujiandaa na mechi za kimataifa za kirafiki kwa Bafana Bafana. Wachezaji walioitwa Bafana Bafana ni; Ronwen Williams, Grant Kekana, Terrence Mashego, Aubrey Modiba, Mothobi Mvala, Khuliso Mudau, Themba Zwane, Teboho Mokoena, Thapelo Maseko na Thapelo Morena itakayokuwa na mechi mbili.

Bafana Bafana itacheza michezo hiyo ya kirafiki, mmoja nyumbani dhidi ya Andorra, Ijumaa ya Machi 22 huku mwingine ukiwa ugenini dhidi ya Algeria, Machi 27 baada ya hapo watarejea Afrika Kusini kuendelea na maandalizi yanaweza kuwa ya siku moja kabla ya kuja Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na Yanga. 

Gamondi anaweza kuwa na muda wa kutosha wa kuwa karibu na wachezaji wake muhimu kwa siku tatu hadi nne kabla ya mchezo huo, japo mkakati wa kuimaliza Mamelodi unaendelea kwa wachezaji ambao wamesalia wakiongozwa na Dickson Job. 

Asilimia kubwa ya wachezaji wa Yanga wapo kwenye kikosi cha Taifa Stars ambacho kina michezo miwili kama ilivyo kwa Afrika Kusini, lakini ahueni iliyopo ni itacheza mapema zaidi dhidi ya Bulgaria Machi 22 na Mongolia, Machi 25.

Wachezaji wa Yanga ambao wapo kwenye kikosi cha Taifa Stars ni Aboutwaleeb Mshery, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad, Mudathir Yahya na Clement Mzize, huku Kennedy Musonda akiitwa Zambia. 

Wachezaji ambao wanaweza kuchelewa kurejea kambini kwa Yanga ni Djigui Diarra ambaye taifa lake, Mali litacheza dhidi ya Mauritania, Machi 22 na dhidi ya Nigeria, Machi 26 na Stephane Aziz Ki ambaye Burkinafso itacheza dhidi ya Libya, Machi 22 na dhidi ya Niger, Machi 26. 

Wakati mambo yakiwa hivyo kwa Yanga upande wa wapinzani wa Simba, Al Ahly yenye wachezaji 11 ambao ni Oufa Shobeir, Mohamed Abdelmonem, Rami Rabia, Mohamed Shokry, Mohamed Hany, Akram Tawfik, Marwan Ateya, Ahmed Kouka, Emam Ashour, Afsha Afsha na Hussein El Shahat watasafiri kwenda New Zealand kwa ajili ya mchezo wa kirafiki unaotarajiwa kuchezwa, Machi 22. 

Nyota wa Simba ambao ni sehemu ya kikosi cha Taifa Stars ni Aishi Manula, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Kennedy Juma na Kibu Denis, huku Clatous Chama akiitwa Zambia na Saido Ntibazonkiza na Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha anaonekana kuwa na idadi kubwa ya mastaa wake, akiwemo Che Malone, Freddy Kouablan, kwenye kikosi kwa sasa ambao hawajaitwa katika timu zao za taifa hivyo atakuwa na muda mrefu zaidi wa kufanya maandalizi.

Saido Ntibazonkiza na Clatous Chama wanaweza kurejea mapema kama ilivyo kwa wachezaji ambao wapo timu ya taifa la Tanzania kwa mujibu wa ratiba zao. Henock Inonga Baka alipata dhoruba kwenye mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Singida FG hivyo anaweza kusalia kambini kwa maandalizi ya kuivaa Al Ahly.

WASIKIE WADAU Kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm amemshauri Gamondi kuwa na mpango bora wakati wakiivaa Mamelodi ili kuwa na mwanzo mzuri wakiwa nyumbani kwenye mchezo wa robo fainali ya kwanza. 

"Ubora wa Yanga ni mkubwa sana, wanatakiwa kuwa na mpango wenye mkakati zaidi ya mmoja, hii ni mechi ngumu na kubwa kwa hiyo inahitaji utulivu," amesema. 

Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr amesema, "Muda mwingine inahitajika kuonekana kichaa ili kufanikisha mambo, hakuna mtu ambaye anaweza kuamini lakini kwenye mpira inawezekana, Simba ina nafasi ya kuishangaza Afrika, itategemea sana na maandalizi ambayo watafanya."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: