Mjadala wenye utata wa FIFA wa kuandaa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili badala ya mzunguko wa sasa wa miaka minne umerudi tena mezani huku shirikisho hilo la kandanda ulimwenguni likiandaa leo mkutano wa kilele wa kimataifa kwa njia ya video na mashirikisho yake 211 wanachama. Hakutakuwa na kura itakayopigwa lakini rai swa FIFA Gianni Infantino amesema wazo ni kutafuta muafaka.
FIFA inasema utafiti wa kampuni moja unaonyesha kuwa mapato ya ziada ya dola bilioni 4.4 yatapatikana kwa kipindi cha miaka minne huku ada za viingilio, haki za matangazo na ufadhili vikiongezeka kutoka dola bilioni saba hadi bilioni 11.4.
Je, mashirikisho ya kitaifa yanataka kweli kuwa na mashindano ya mara kwa mara ya Kombe la Dunia, au mpango huo unaopigiwa upatu na Arsene Wenger utasambaratika?
Ili kusaidia kuyashawishi mashirika 211 wanachama kukubali pendekezo hilo – ambapo 207 yalishiriki Mkutano wa Jumatatu, FIFA imeapa kutoa dola milioni 19 za ziada kila baada ya miaka minne kwa kila mwanachama. Taarifa ya FIFA imesema “kila mwanachama atapata karibu dola milioni 16” zilizotengwa kutoka “Hazina ya Mshikamano” ya karibu dola bilioni 3.5 katika miaka minne ya kwanza ya kalenda iliyofanyiwa mabadiliko, pamoja na ongezeko la ufadhili kupitia mpango wake wa FIFA Foward kutoka kiasi cha sasa cha dola milioni sita hadi milioni tisa.
Kuna wanaokosoa wakisema mpango huo utakuwa na madhara kwa afya ya wachezaji kutokana na mrundiko wa mashindano. Wenger anahoji kuwa wachezaji wengi hawapati fursa nyingi za kujiendeleza lakini nchi 133 hazijawahi kushiriki katika Kombe la Dunia. FIFA inasema mpango huo utatengeneza faida Zaidi na kusambaza Afrika, Asia na Amerika Kusini.