Inasemekana kwamba sasa ni rasmi kuwa mshahara aliopewa Fiston Mayele unamhalalisha hatakuwa mchezaji tena wa Yanga msimu ujao baada ya kuomba kwenda kukipiga nchini Saudi Arabia huku Yanga wakilambishwa zaidi ya Bilioni 1.2 kama dau la usajili.
Mbali na hapo, Mayele mwenyewe amepewa Sh Milioni 400 kama fedha ya usajili na mshahara wa dola elfu 25 (Sh mil 60.7) kila mwezi.
“Kwa sasa ninaweza kukuhakikisha kabisa kuwa, Mayele anaondoka kwetu na ataenda kucheza huko Saudi Arabia ambapo amepata moja ya timu na imempa zaidi ya mshahara wa Sh mil 60 kila mwezi.
“Mshahara huo umekuwa ni mkubwa kwetu hivyo tumeshindwa kumbakiza kwani pia wamempa dola 200,000 (Sh mil 486.1) kama sehemu ya usajili wake, huku kwetu wakitupatia hiyo zaidi ya Bilioni moja ili tumuachie,” kilisema chanzo hicho.
Wakati Mayele akijiandaa kusepa, tayari Yanga wameshaanza kusaka mbadala wake na jicho lao limeangukia kwa straika mwili jumba, Sudi Abdallah raia wa Burundi aliyekuwa na ufalme wa kutosha nchini Iraq.
“Tunamshukuru Mungu kwa kutupatia mbadala wa Mayele, ambapo sasa msimu ujao tuna uhakika tena wa kwenda kutamba na bonge la straika wa mabao na mkali wa kuchana nyavu.
“Jamaa amekubali kujiunga kwetu kwa dau la milioni 400 tu huku kila mwezi akiomba mshahara wa milioni 25, fedha ambayo ni nafuu zaidi kwetu baada ya kushindwa kumbakiza Mayele,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika kabisa.