Everton ipo katika hatari ya kupokwa pointi kwa mara ya pili huku wamiliki watarajiwa, kampuni ya hisa ya Marekani ya 777 Partners wakipigwa ‘stop’ mchakato wa kuinunua klabu hiyo kwanza.
Imeelezwa Ligi Kuu England itafanya uchunguzi dhidi ya kampuni hiyo kutoka Marekani baada kampuni hiyo kufunguliwa kesi za kisheria, na endapo itapatikana na hatia Everton ndo itaathirika zaidi.
Kwa mujibu wa Daily Mail, wawekezaji wa kampuni ya 777Partners wamepewa taarifa na Ligi Kuu England kuwa mpango wao wa kuinunua klabu hiyo utasubiri hadi mwisho wa mwaka mpya.
Hofu imezuka kwamba huenda Everton ikaingia kwenye utawala mpya mwezi ujao, kwani kampuni ya hisa ya Marekani imeipatia Everton mkopo wa zaidi ya Pauni 100 milioni kwa ajili ya gharama za uendeshaji.
Uamuzi huo umefuata baada ya makubaliano ya kuinunua klabu hiyo kutoka kwa mwenyekiti Farhad Moshiri tangu Septemba mwaka huu.
Ili Everton itoboe kichumi msimu huu, inatahitaji nyongeza ya Pauni 20 milioni kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi na gharama za uendeshaji.
Kwa sasa Everton inakabiliwa na tatizo la uchumi kutokana na kukiuka sheria za matumizi ya pesa na hivyo kukatwa pointi 10.
Licha ya kupitia kipindi kigumu, kocha Sean Dyche ameendelea kupambana uwanjani kwani wameshinda mechi nne katika ya tano walizocheza baada ya kupokwa pointi 10.
Everton ilipanda hadi nafasi ya 17 kwenye msimamo baada ya kuifunga Chelsea mabao 2-0 na wikiendi ijayo itashuka dimba kumenyana na Burnley katika mechi nyingine ya EPL.