Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Euro 400m, Ten Hag kajivua lawama

Ten Hag Lawamaa Euro 400m, Ten Hag kajivua lawama

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Erik ten Hag amesema tena kwa msisitizo kwamba hahusiki na matumizi ya Pauni 400 milioni ambazo Manchester United ililipa kwenye kunasa huduma za mastaa wapya kwenye kikosi hicho.

Kocha huyo Mdachi, Ten Hag, ambaye bado hafahamu hatima ya kibarua chake kwenye kikosi hicho cha Old Trafford, alisema dili zote za pesa nyingi zilizofanywa kwenye usajili wa mastaa wapya - Antony, Casemiro, Rasmus Hojlund, Mason Mount na Andre Onana hazimhusu.

Kocha Ten Hag ameshusha lawama kwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa zamani wa Man United, Richard Arnold pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa soka wa miamba hiyo, John Murtough, hao ndio waliothaminisha wachezaji hao kuwa na thamani hiyo.

Ten Hag alisema: “Pesa iliyolipwa ni kubwa sana, lakini sihusiki kwa hilo. Klabu ndiyo iliyohusika kwenye kufanya makubaliano, ikiwamo wachezaji waliokuwa na viwango bora ambao hawakuja.

“Hivyo, si kitu kinachoingia akilini kutokana na taswira iliyopo kwamba sera ya usajili kwenye klabu ipo hovyo. Ni kitu cha hovyo, lakini licha ya matatizo yote, msingi wa klabu bado upo imara.

“Pengine hilo halionekani huko nje, lakini hapa ndani kila kitu kipo vizuri na kinajieleza.”

Winga wa Kibrazili, Antony alinaswa na Man United kwa ada ya Pauni 85.5 milioni akitokea Ajax, mahali ambako alikuwa akifanya kazi yake ya ukocha, Ten Hag.

Kiungo, Casemiro, ambaye pia ni Mbrazili aliigharimu timu hiyo Pauni 70 milioni akitokea Real Madrid, ambapo alikuwa na msimu wa kwanza bora kabisa, lakini sasa hesabu zote zinazopigwa huko Old Trafford ni kumfungulia mlango wa kutokea kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Man United pia ililipa Pauni 47.2 milioni kunasa huduma ya kipa Mcamerooni, Onana.

Kwenye msimu wa Ligi Kuu England, mambo hayakwenda vizuri kabisa kwa Man United baada ya miamba hiyo kumaliza kwenye nafasi ya nane.

Man United itacheza michuano ya Ulaya msimu ujao baada ya kushinda kweye mchezo wa fainali wa Kombe la FA, dhidi ya Manchester City na hivyo itacheza kwenye Europa League.

Tajiri mpya wa miamba hiyo, bilionea Sir Jim Ratcliffe kwa sasa anafanya tathmini ya kikosi hicho kwa msimu mzima kuona kama kocha Ten Hag anastahili kubaki kwenye kikosi au afunguliwe mlango wa kutokea. Tajiri Ratcliffe hakuonekana kumsapoti Ten Hag hadharani tangu alipotua Old Trafford.

Ten Hag aliwajibu wamiliki hao wa Man United baada ya fainali ya Wembley, aliposema: “Wakati naanza hapa, nilisema ‘nipo hapa kushinda mataji na kujenga timu’.

“Nafanya vyote hivyo. Lakini, kama hamnitaki tena, nitakwenda kwingine kushinda mataji. Nipo kwenye mpango wetu na sote tunafahamu tunapotaka kwenda. Tunajenga timu kwa ajili ya baadaye.

“Nilipochukua hii timu hali ilikuwa mbaya. Timu sasa imeendelea vyema, inashinda mechi na inacheza soka linalojitambulisha.”

Graham Potter, Thomas Tuchel, Gareth Southgate, Mauricio Pochettino na Roberto de Zerbi ni makocha ambao wamekuwa wakihusishwa na Man United kwa siku za karibuni.

Lakini, Ten Hag alimaliza nafasi ya tatu kwenye msimu wake wa kwanza Man United na kama atabaki, basi atatumia muda wake kuboresha kikosi hicho kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Ten Hag aliongeza: “Mpango wa mwaka jana ulikuwa wazi: Tumenunus straika na tumepata kipa mwenye uwezo wa kuanzisha mashambulizi yetu kuanzia nyuma na kuwa kama kiungo wa ziada. Hulo limefanyika kuna uhakika mkubwa wa kuwa imara zaidi na kupiga hatua inayofuata.”

Chanzo: Mwanaspoti